Monasha
JF-Expert Member
- Apr 2, 2011
- 561
- 422
Tafsiri hii ya kujivua gamba ilianza kutolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akihutubia katika kilele cha sherehe za miaka 34 ya CCM mnamo Februari 5 mwaka huu.
Akieleza haja ya CCM kujivua gamba, Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho, alibainisha kuwapo kwa mchakato wa mageuzi ya ndani ya CCM ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kushindana na kushinda katika uchaguzi ujao.
Kutemwa kwa baadhi ya viongozi wa CCM kunatokana na viongozi hao kuhusishwa na baadhi ya kashfa za ufisadi kitu ambacho kimekuwa kikichafua chama hicho kwa muda mrefu sana.
Kashfa hizi zimekuwa zikileta mpasuko ndani ya chama na hata kama hawatakuwa makini na kuendelea kujivua magamba mpasuko utazidi kuongezeka na hatimaye si ajabu miaka ijayo tusione CCM. Kashfa ni nyingi kwa kweli,kwa mfano sijui richmondi, Epa, Dowans n.k. Hizi zooote zinawahusu viongozi wa CCM.
Mwalimu Nyerere aliyoana haya.
Hali ya ufisadi ndani ya CCM iliyosababisha kutokea kwa mabadiliko hayo ilitabiriwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alikionya CCM kutoendekeza rushwa.
Katika kitabu chake cha Nyufa chenye hotuba aliyoitoa Machi 13, 1995, Mwalimu Nyerere ametaja nyufa tano zilizoikumba nchi ambapo alisema kuwa ufa wa nne ni rushwa ndani ya CCM na serikali yake.
Mwalimu Nyerere amebainisha kuwa chanzo cha mpasuko ndani ya CCM ni kutokana na viongozi wa chama hicho kukosa maadili na hasa pale kilipoikana misingi ya Azimio la Arusha.
Kuna miiko ndani ya Azimio la Arusha , viongozi wetu walikutana Zanzibar wakaona Azimio la Arusha halifai, wakatutangazia na hawakuzungumzia kwamba tumekutana Zanzibar tumeona Azimio la Arusha halifai. Walikuja kimyakimya tukaona wanaanza kufanya mambo ambayo hayafanani na Azimio la Arusha. Wenye akili tukajua limekwisha hilo, anasema Mwalimu Nyerere.
Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, hakuna serikali popote duniani inayoendeshwa bila miiko. Anazitaja nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Japan na kusema kuwa zinaendeshwa kwa miiko.
Kwa hiyo nchi zote zina miiko. Hapa sasa hatuna. Wameacha miiko ya Azimio la Arusha, hawakuweka miiko mingine, sasa ni holela tu, anasema.
Kutokana na hali hiyo, Mwalimu Nyerere anasema kuwa imefungua milango ya rushwa ambayo awali ilikuwa imebanwa. Anakumbushia enzi za TANU ambapo licha ya kuwa na miiko ya uongozi, kulikuwa na kanuni za TANU. Moja kati ya kanuni hizo ni ile iliyorithishwa CCM inayosema, Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala sitapokea rushwa.
Usije ukadhani kwamba wakati wa awamu ya kwanza palikuwa hapana rushwa, ilikuwapo lakini tulikuwa wakali sana. Siku za mwanzo kabisa tulitaka watu wajue hivyo. Tukapitisha sheria kwamba mtu akila rushwa, eh kiongozi wetu anakula rushwa: anayetoa, aliyepokea wote wanapata msukosuko, anasema Mwalimu Nyerere.
Akieleza sifa ya kiongozi anayepaswa kuiongoza Tanzania, Mwalimu Nyerere anasema kuwa kiongozi bora si yule anayechukia rushwa tu, bali pia awe na uwezo wa kuwaambia rafiki zake kwa kauli ambayo wataiheshimu na hawatarudia tena.
Sasa Tanzania inanuka rushwa. Tunataka kiongozi atakayesema; rushwa kwangu ni mwiko, mwaminifu kabisa hawezi kugusa rushwa na watoa rushwa watamjua hivyo.
Ikulu ni mahali patakatifu, mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kupageuza kuwa pango la wanyanganyi, anasema Mwalimu Nyerere.
Akizungumzia rushwa katika uchaguzi Mwalimu Nyerere anakumbushia enzi ya utawala wake ndani ya TANU na CCM akisema kuwa mali ingeweza kumkwamisha mgombea;
Zamani katika CCM na katika TANU, tunapochagua mgombea wetu kama ana mali tunamuuliza hii umeipata wapi?. Mali ilikuwa kigezo cha kupoteza sifa ya kuwa mgombea, anasema.
Kwa misingi hiyo kujivua gamba pekee hakutushi, tunapaswa kuwa na viongozi wenye uadilifu wa kweli, wanaochukia rushwa na jamii iwaelewe hivyo.
Kimsingi rushwa ikiendekezwa italimongonyoa taifa.
Nimeona niwaletee hili wana JF ili mjue na tujue sote pamoja na kuona maoni yenu pia.