Nyani mjengoni

MR NDEE

Member
Aug 2, 2011
54
21
NYANI MJENGONI

Salamu natanguliza, Bara nako visiwani
Mezani nako baraza, Salamu zikufikeni
Mwaloni na viambaza, Salamu ninakupeni
Nyani huko mjengoni, Hivi atafuta nini?

Hivi atafuta nini, Nyani huko mjengoni
Asiliye ni mwituni, Mjini katafutani
Anijaza tafarani, Nayo maswali kichwani
Nyani huko mjengoni, Hivi atafuta nini?

Nyani huko mjengoni, uchao yuko hewani
Habarize gazetini, Runinga na redioni
Habarize mjengoni, Za viza matumaini
Nyani huko mjengoni, Hivi atafuta nini?

Hivi atafuta nini, Nyani huko mjengoni
Atendacho siamini, Anena kihayawani
Hasiraze zi pomoni, Sumuze zi mdomoni
Nyani huko mjengoni, Hivi atafuta nini?

Nyani huko mjengoni, Amuwakilisha nani
Uchao hoja kinzani, Fujo nazo tafarani
Kejeli na ya nguoni, Abwabwaja mdomoni
Nyani huko mjengoni, Hivi atafuta nini?

hivi atafuta nini, Nyani huko mjengoni
Dharau za duniani, Ama laana za karni
madafu ya mfukoni, Laa ana Mashetani
Nyani huko mjengoni, Hivi atafuta nini?

Nyani huko Mjengoni, Juma la tatu lifika
Alichofanya sioni, Sikuzo za puputika
Zikitimu sabini, Tisini atazishika
Nyani huko mjengoni, Hivi atafuta nini?

Nyani huko mjengoni, Kikao kajikalia
Ni wake utamaduni, Vikao kujikalia
Hata akae tisini, Tamati hatofikia
Nyani huko mjengoni, Hivi kafata nini?

Nyani huko mjengoni, Hivi kafata nini
jawabu nawaombeni, Bara nako Visiwani
Nitoke goigoini, Na ushamba wa kichwani
Nyani huko mjengoni, Hivi kafata nini?


 

Similar Discussions

Back
Top Bottom