"Njaa" na heshima au "Mkate" na dharau?

Samahani

JF-Expert Member
Oct 29, 2018
222
335
Rasilimali ni msingi muhimu kwa maendeleo. Maendeleo yanahitaji uwepo wa rasilimali, na kisha zitumike kwa uadilifu, mpangilio na usimamizi makini. Rasilimali zinasimama kama ‘chanzo cha nishati’ katika maendeleo. Mojawapo kati ya rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa ni “watu”.
___

Katika miaka ya mwanzo ya utekelezaji wa falsafa “ujamaa na kujitegemea”, serikali na jamii vilijibidiisha katika kuitambua na kuiinua rasilimali hii muhimu, sambamba na utoaji wa elimu hadi kwa watu wazima. Tulifunga mikanda, tukaruhusu uchumi wetu uzorote ili tuongeze idadi ya wasomi katika taifa. Katika hili, tulifanikiwa.
___

Waliopewa fursa ya kusoma hadi vyuo vikuu walikuwa ni rasilimali hasa. Walipikwa wakawa wataalamu katika taaluma zao. Walipohitimu, walikuwa tayari kukabiliana na changamoto zilizo mbele yao pamoja na kuzikamata fursa zilizokuwepo kwa maslahi ya taifa. Walinyooka kwanza wao, kasha tukawapa kazi ya kulinyoosha taifa.

Kiongozi mmoja mkubwa (apumzike kwa amani), wakati huo akiwa chuo, aliwahi kuandaa mgomo! Akaalikwa Ikulu, naye akawahi akifikiri ameandaliwa kifungua kinywa. Aliambulia viboko vikali vya makalio na onyo kali. Maadili yalikuwa kielelezo cha usomi wa taifa.
___

Sasa tumeteleza pahala. Vyuo vikuu sasa vinatia aibu! Madhila yanayoletwa na wasomi wa vyuo vikuu leo hayafai kusema hadharani. Unahitaji kuwa na ufahamu wenye athari fulani ili uweze kuyabainisha ama kuyazungumzia haya waziwazi. Pahala pekee tunapotegemea patupe rasilimali watu ya kusimamia taifa sasa imekuwa ni kiwanda cha kuzalishia uhuni, ufuska, utapeli na mengine mengi.
___

Kashfa ya mabinti wa vyuo vikuu kujihusisha na upigaji picha za uchi, kurekodi video za ngono, kujihusisha na biashara ya ukahaba na mengine yanayofanana na hayo vinazidi kushika kasi kila siku. Unapotembelea mitandao ya kijamii, unakutana na makundi maalumu ambapo “wasomi” wetu wa vyuo vikuu wanaweka wazi picha zao za utupu kwa lengo la kujitangaza.
___

Wengine wanaweka pia namba zao za simu na majina ya vyuo wanaposoma ili wateja waweze kupata unafuu wa kuwapata.
Ufikapo katika “laptop” za wanachuo, simu zao na vifaa bebeshi vingine walivyonavyo, ambavyo kimsingi vingepaswa kutumika kwa shughuli za mawasiliano na kitaaluma, unakutana na picha na video za utupu zilizorekodiwa na wanachuo wenyewe!

Hata katika kumbi maarufu mijini ambapo shughuli haramu ya ukahaba zinafanyikia, leo unakutana na makahaba ambao kimombo kwao sio haba, na wanajikuta wanateka sana soko kwa elimu yao ya lugha.

Wasomi wa chuo kikuu wanateka soko la kuuza uchi!!
___

Kwao, viungo vyao vya mwili navyo vinauzwa kwa bei ya kuchuuza. Awali nilianza kuamini kuwa hawa wanayafanya kutokana na ugumu wa maisha, na ilibaki kidogo nianze kuwakumbusha sirikali wajibu wao. Iwe ni kutokana na ugumu wa maisha au la, huu ni wendawazimu!
___

Hivi darasani mwanafunzi anafundishwa nini juu ya maisha? Mwalimu gani anafundisha kuwa maisha ni tamthilia za marehemu Charlie Chaplin ambazo zimetawaliwa na vicheko vya kila mara? Wasomi wetu mpaka sasa hawajui kuwa maisha ni aina ya changamoto ambayo inahitaji jitihada za kipekee kuitatua?

Kwanini wanasahau kuwa kujiuza au kujishughulisha na ukahaba wa aina yoyote ni kujipotezea heshima na staha kwa jamii huku wakijipatia mkate ambao shukrani yake ni kuomba hifadhi chooni? Hivi leo ukiolewa, na maisha yakawa magumu, suluhisho la kwanza unalolipata ni kuuza uchi wako ili upate hela ya kula?
___

Hakuna anayefika chuo kikuu bila kuwa anayafahamu madhara ya muda mfupi na muda mrefu ya ukahaba, HAKUNA! “Wasomi” wetu hawa wanajua kabisa kuwa, shughuli ya kuuza mwili kama maandazi zinawaweka katika hatari ya maambukizi ya magonjwa ya ngono, UKIMWI ukiwepo.

Pili, zipo mimba zisizotarajiwa, ambazo zinaweza kupunguza kasi ya kujisomea kutokana na mawazo na kutokujiandaa. Tatu, kwa mwanafunzi anayeutumia muda wake wa mchana vema, usiku ni muda mzuri wa kupumzika ili apate nguvu kwa siku inayofuata.
___

Unapokaa kwenye vilabu vya usiku hadi saa kumi na moja alfajiri, unategemea kweli siku inayofuata unakuwa makini darasani? Lakini zaidi ya hayo yote, heshima yako unayoipoteza mbele ya jamii utaifidia vipi? Leo umekuwa Waziri mkuu halafu zinaibuka picha na video zako za uchi ukiwa binti!!! Mola tunusuru!!
___

Umaskini wetu uko bayana kabisa, hata mwalimu alishasema umaskini ni mojawapo kati ya maadui wa nchi. Lakini pamoja na hili, hivi tukisema leo kila mwanamke mwenye shida awe kahaba mama zetu nao si wote watakuwa makahaba? Ndiyo, wapo akina mama wana shida mpaka wanavaa mashati ya waume zao ili waende sokoni.

Mbona hawa hawaiuzi miili yao? Wapo wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wameamua kupambana na ugumu wa maisha kwa kujifunza matumizi mazuri ya pesa. Hawa wanajua kuwa, ugumu huu ni wa muda tu, kisha watakipata wanachokihitaji.

Maisha yenye staha na amani.
___

Kupambana na hali duni, wapo ambao wameanzisha ushirikiano, wakiishi pamoja, kula pamoja na kusoma pamoja ili kupunguza gharama za maisha. Huyu akitoa chumvi, huyu dagaa yule unga, ugali haujaiva? Wengine wamejianzishia “vibiashara” ili kujikimu, na wanasonga mbele. Baadhi walianza kwa utani lakini leo ni wajasiriamali wazuri. Wako tayari kujiajiri wamalizapo masomo. Huu ndio Usomi!
___

Lazma mwanafunzi uliye chuoni ujitofautishe na wasiosoma kwa matendo yako. Elimu unayo, na taifa linategemea makubwa kutoka kwako. Kwanini unatutia aibu? Hivi wazazi wako wanajua kuwa siku hizi umekuwa kahaba? Waambie ili wakupe baraka zao, na wao si wanajua una hali ngumu ya kimaisha na umechagua kujiajiri?
___

Kuna baadhi ambao bodi ya taifa ya mikopo ya elimu ya juu inawapa mkopo, lakini bado wamekuwa maarufu katika biashara ya ukahaba, si mnamkumbuka yule mtoto wa kigogo wa serikali aliyepiga picha za utupu pale “Chuo cha Taifa”? (sitaki maswali, kama hukijui basi hujasoma). Hivi na yule tuseme kuwa alikuwa na maisha duni?

MAKINIKA KWA HAYA

MOSI, Ni busara kubwa kwa wasichana kujifunza kukataa kabisa kuweka kumbukumbu ya aina yoyote katika mfumo wa picha au video, hasa zile zinazowaonesha wakiwa katika hali ya utupu.

PILI, Kwa kuwa mahusiano ni jambo la binafsi na si rahisi kuingilia uhuru huu, walioko kwenye mahusiano kukataa kabisa kujirekodi wakiwa kwenye hali za utupu. Kutokana na uzoefu, mara nyingi usambazaji wa picha hizi huja kama adhabu baada ya mahusiano kuvunjika.

TATU, Inapotokea kuna vitisho vya usambazaji wa picha zenye maudhui ya utupu, ni vema mhusika akatoa taarifa mapema kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kupata msaada wa kisheria.
Wasimamizi wa maadili hasa vyuoni wanapaswa kuwa na ukaribu zaidi na mabinti kwakuwa wao mara nyingi ndio waathirika wakubwa wa matendo haya.

NNE, Sheria zinapaswa kuboreshwa zaidi ili kuwa na “meno” makali zaidi kwa wanaothubutu kuhusika kwa namna yoyote ile katika usambazaji wa picha za utupu.

TANO na muhimu zaidi; tunazo mamlaka za uthibiti wa kimawasiliano. Ni wakati muafaka wa kuamua kwa dhati kukomesha biashara ya ngono mitandaoni.
___

Uchi wako una thamani kubwa na una uhusiano mkubwa na elimu na utu wako. Unapoupiga picha na kuusambaza hadharani unaharibu taaluma yako na mustakabali wa taifa. Huu sio uungwana. Umesoma ili uelimike na kuelimisha jamii.

___

Unapoonesha dalili za kutokuelimika, unatupa hofu kuwa, hata sisi tusioelimika huwezi kutusaidia. Sasa wewe ni wa kazi gani? Na tukikuita “msomi uchi” utajisikiaje?? Kama ni ugumu wa maisha, siku utakapomkuta mama yako mzazi akijiuza kwa kisingizio cha ugumu wa maisha utajisikiaje? Unajifunza hayo kutoka kwa nani?

Wasalaam.
 
Back
Top Bottom