Imetolewa mara ya mwisho: 29.03.2007 0142 EAT
Majambazi 10 wateka mabasi
Habari Zinazoshabihiana
Majambazi wateka gari lenye maiti 14.04.2006 [Soma]
Majambazi wateka abiria, wawavua nguo na kuwaibia 19.10.2006 [Soma]
Majambazi wenye mabomu wateka abiria 02.11.2006 [Soma]
*Wavua abiria nguo, wawapora fedha
Na Mashaka Mhando, Lushoto
MAJAMBAZI 10 wenye silaha wameteka mabasi mawili yaliyokuwa yakitokea katika kijiji cha Mlola wilayani hapa, kwenda Dar es Salaam, na kujeruhi kwa risasi abiria watatu wa magari hayo na kuwapora sh. milioni saba.
Tukio hilo lilitokea jana saa 11.30 alfajiri wakati mabasi hayo yenye namba T765 ADD la kampuni ya Kwekanga Line ambalo lilikuwa likitoka Mlalo kwenda Tanga na namba T510 AJU la kampuni ya The Queens Class ambalo lilikuwa likienda Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kondakta wa basi la Kwekanga, Bw. Kitoi Daud, waliondoka Mlalo saa 11 alfajiri kwenda Tanga na walipofika katika Mlima Mandeni kati ya kijiji cha Mlola na Ungo, waliona mtu akimulika kwa tochi akisimamisha ili apande.
Tuliposimama walijitokeza watu porini kila mmoja ameshika panga mkononi wakaamuru tuzime taa za gari, tulipokuwa bado tunashangaa walivunja vioo vinne vya madirisha ya gari na kuingia ndani, wakatuibia kila kitu, mimi nilikuwa na sh. 86,500 zote zilichukuliwa, alidai kondakta huyo.
Alisema abiria wao mmoja aliyemtaja kwa jina la Hamisi Mzava, ambaye ni mfanyabiashara aliyekuwa akienda kuchukua bidhaa, aliporwa sh. milioni nne na alipofika kijiji cha Mbwei aliteremka na kurudi nyumbani Mlola.
Kondakta huyo alisema kuwa baada ya kuchukuliwa fedha alivuliwa nguo na kuachwa uchi baada ya kukutwa katika kiti cha mwisho cha basi amejificha na aligundulika baada ya simu yake kudondoka ambapo jambazi mmoja alimpiga panga mbavuni na kumtaka atoke haraka.
Wakiwa wameibiwa kila kitu, dereva aliporuhusiwa kuondoka, gari liligoma kuwaka na majambazi hao wakatoa amri asubiri baada ya kuona mwanga wa basi lingine likifika katika eneo hilo na kuwataka abiria watulie ili waliteke kabla ya kuruhusiwa wao.
Tulisikia zima taa, vuta hand brake, kuangalia tukaona basi la Kwekanga Line likiwa limesimama tukajua limeharibika, mara akatokea huyo mtu mwenye tochi akitutaka tuzime taa na tuteremke tukiwa uchi na kila mtu ashike fedha zake mkononi kwa wakati huo, walisema hizo si pesa zetu tena ni mali yao, alisema kondakta wa Queens, Bw. Muba Ally 'Muhogo'.
Alisema kabla hawajatafakari nini kinatokea katika eneo hilo, alipanda jambazi mmoja jirani na kiti cha dereva akiwa na bunduki na kuwaamuru: "Hamtaki kushuka na kutoa hela, ngoja tuwaoneshe, hii bunduki ina risasi 30 na kila moja tumenunua sh. 20,000, akapiga risasi ikapiga juu ya keria ya basi, iliwajeruhi watu karibu watatu, abiria kuona hivyo kila mmoja aliteremka na kutoa fedha.
Alitaja waliojeruhiwa kuwa ni Bw. Daud Mamba ambaye amejeruhiwa begani na hali yake si nzuri amefikishwa kwenye hospitali ya wilaya Lushoto, mwingine ni Mzee Ally Binda mkazi wa Korogwe ambaye alikwenda kununua maharage na aliibiwa sh. 520,000 na kukatwa panga kichwani na Bibi Salima Hamisi ambaye baada ya kupigwa na kukatwa mapanga alipotelea msituni hadi sasa haijulikani alipo.
Kondakta huyo alisema kwa ujumla katika gari lake walichukua fedha kadhaa ambapo yeye na kondakta mwenzake waliporwa sh. 350,000 na abiria wengine walichukuliwa kati ya sh. 70,000 na sh. 500,000 huku akina mama wengine wakiporwa nauli zao za kati ya sh. 200 na sh. 1,500.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto, Dkt. Samwel Mgema, alikiri kupokea majeruhi hao wawili ambao wanaendelea kupewa matibabu hadi jana, walikuwa bado hawajaruhusiwa kutoka hospitalini kutokana na Bw. Mamba kuwa na gololi ya risasi, hivyo walikuwa wakimfanyia utaratibu wa upasuaji ili kuitoa.
Mwandishi wa Habari hizi ambaye alizungumza na abiria waliokumbwa na janga hilo wakiwa katika kituo cha Polisi Lushoto, alishuhudia mabasi hayo mawili yakiwa hayajaondoka kuendelea na safari hadi saa nne asubuhi jana.
kazi bado ipo...............