Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
NISIKIZE RAIS.
1.
Kuna mambo kiongozi,
Nataka kukuusia,
Hiyari kuzingatia,
Ama kuyapuuzia.
2.
Kuna mambo kiongozi,
Usiseme waziwazi,
"Imekuwa kubwa kazi"
"Sina namna siwezi"
3.
Kuna mambo kiongozi,
Kutamka hutakiwi,
"Tuendapo sipajuwi"
"Nimekwama sielewi"
4.
Kuna mambo kiongozi,
Siyanene iwe vipi,
"Sijuwi nifanye lipi"
Na "tufate njia ipi"
5.
Kuna mambo kiongozi,
Kuyajuwa ni lazima,
Siwe wa kwanza kusema,
Na sikiza madhuluma.
6.
Kuna mambo kiongozi,
Vema uyapime kwanza,
Siyo kurupu wafanza,
Taifa utaliponza.
7.
Kuna mambo kiongozi,
Yataka kuyachunguza,
Pamwe na kupeleleza,
Kabula ya kutangaza.
8.
Kuna mambo kiongozi,
Kuyafanya ni laana,
Kuwasha taa mchana,
Thama futa jingi sana.
9.
Kuna mambo kiongozi,
Yaepuke fanya hima,
Kula huku ukisema,
Kwenda haja 'mesimama.
10.
Kuna mambo kiongozi,
Yatie mwako kitwani,
Ulokuwa nao ndani,
Waamini kwa wastani.
11.
Kuna mambo kiongozi,
Yataka uyamaizi,
Mepewa wasaidizi,
Katu siyo vijakazi.
12.
Kuna mambo kiongozi,
Kuyajuwa ni hekima,
Wakati wa kuchutuma,
Sijaribu kusimama.
13.
Kuna mambo kiongozi,
Yataka kuzingatia,
Jihimize kusikia,
Jiepushe kuchukia.
14.
Kuna mambo kiongozi,
Muhimu uyatambuwe,
Mti upigwao mawe,
Una matunda ujuwe.
15.
Kuna mambo kiongozi,
Kuepuka si rahisi,
Kutajwa kwenye tetesi,
Na kutukanwa matusi.
16.
Kuna mambo kiongozi,
Huwezi kuyakataa,
Kuwa wewe ndiye jaa,
Katika wetu mtaa.
17.
Kuna mambo kiongozi,
Yafahamu siku zote,
Huwezi pendwa na wote,
Hivyo kufura uwate.
18.
Kuna mambo kiongozi,
Yataka uwe mkali,
Lakini si ukatili,
Haufai tafadhali.
19.
Kuna mambo kiongozi,
Yataka uwe rahimu,
Ila si wa kibahimu,
Huo utatugharimu.
20.
Kuna mambo kiongozi,
Kuwa nayo ni hasara,
Kuongozwa na papara,
Na kutumwa na hasira,
21.
Kuna mambo kiongozi,
Yataka ukose haya,
Kusema walokoseya,
Hata iwe familiya.
22.
Kuna mambo kiongozi,
Kuyafanya ni hatia,
Kuzikanyaga sheria,
Na katiba 'loapia.
23.
Kuna mambo kiongozi,
Tangu kae yana ma'na,
Uongozi ni dhamana,
Kwa sheria twapeana.
24.
Kuna mambo kiongozi,
Ukiyafanya ni vita,
Kuvunja uloyakuta,
Kwa jasho tuloyapata.
25.
Kuna mambo kiongozi,
Kuyavunja ni rahisi,
Kuyajenga si mepesi,
Hata uwe mwenye kasi.
26.
Kuna mambo kiongozi,
Yataka kujiandaa,
Kiyafanya kwa tamaa,
Utatuletea baa.
27.
Kuna mambo kiongozi,
Ninaomba uyashike,
Cheo kina mwisho wake,
Hivyo usihadaike.
28.
Kuna mambo kiongozi,
Uchao uyakumbuke,
Walokufanya ucheke,
Usije wapigateke.
29.
Kuna mambo kiongozi,
Ukiyafanya 'tatisha,
Gari hovyo kuendesha,
Bila breki ya kutosha.
30.
Kuna mambo kiongozi,
Miye yanisikitisha,
Usia kuukatisha,
Kwa wino wangu kuisha.
23 February 2017 Alhamisi.
[HASHTAG]#JiniKinyonga[/HASHTAG]
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.