Ningepata nafasi kuongea na Rais

Chereko

Member
Jul 20, 2009
54
16
Siku Rais alijibu maswali
Nilijaribu kupiga simu sikupata, sikupenda kutumia anuani ya yahoo hivyo sikutuma e-mail. Laiti ningepata nafasi nimeguswa sana na ninakerwa na usafiri kwa ujumla na ningemuuliza Mh Rais maswali yafuatayo:

  1. Bandari - Tunaelewa fika kuwa bei ya mafuta hata inaposhuka kwenye soko la dunia, hapa kwetu inaweza kupanda kisa ni meli kusubiri bandarini; Hali ya uchumi inabamizwa na gharama za usafiri Mh tunateseka. Je kero hii mwisho wake ni lini? Wananchi wataendelea kulipia gharama hizo mpaka lini? Kitu fulani inapasa kifanyike pale bandari, wape vipimo kiongozi awajibike kama hafikii malengo. Unaonaje hili?
  2. Barabara - Ajali za barabarani ni kama jambo la kawaida nchini kwetu, magari yanagongana, yanapinduka na ajali zimezidi. Nakupa pole Mheshimiwa wakati ulipotoa amri ya adhabu kali, hakimu mmoja alifunga dereva miaka 30 na madereva wa bara wakagoma. Je si wakati muafaka kwa askari kuzuia ajali? Badala ya kungoja ajali wadhibiti ajali yaani wakamate waendeshao wakiwa wamelewa, wasio na leseni, wanaokatisha njia au "kutanua", waendeshao mwendo kasi n.k. tukiwadhibiti hawa "vichaa" tutaokoa maisha ya watu wengi. Daladala waiothamini vituo na kungoja abiria kwenye kona wakamatwe na kufungiwa. Ninachokuomba Mheshimiwa umpe Mkuu wa Usalama barabarani kipimo cha ajali kwa mwezi, zikizidi kipimo aachie ngazi, unasemaje Mheshimiwa?
  3. Treni - Mheshimiwa, Marehemu Mwalimu aliwahi kukiri makosa kwa mwandishi mmoja wa kijerumani kuwa alifanya makosa kufuta halmashauri za miji. Je serikali yetu haiwezi kukiri kuwa kuipa kampuni ya kihindi kuendesha reli ilikuwa ni makosa?
  4. Kampuni ya Ndege: Twiga wetu ni "nyama gonjwa" Air Tanzania. Je Mheshimiwa kwa nini tunaachia Precision wanatawala viwanja vyetu (ni wakenya wale kupitia Kenya Airways) Air Tanzania amebaki kama mtoto yatima asiye na baba nyumbani kwake. Hili ni ombi tu kwako tafadhali weka mkono wako hapa, wakati wa soko huru la Jumuia bado na pia likija tuwe tumeimarika, tutakaliwa nyumbani kwetu.
  5. Mheshimiwa: Kwa nini ambaye inasemekana ameenguliwa kama Afisa Mtendaji Mkuu wa Air Tanzania bado analipwa mshahara na shirika hilo na bado anatumia gari la shirika hilo, kwani huko aliko hakuna magari? Kazi anayofanya inanufaisha shirika?
  6. Viwanja vya ndege: Hongera kwa kutoa wito kwa wanaanga wa zamani kutumia karakana ya ndege KIA. Hongera zaidi kwa kuwa umerejesha kwa kiasi fulani umiliki wa kiwanja cha KIA chini ya serikali.
  7. Meli Mheshimiwa hivi zile enzi za MV Lindi, MV Mtwara n.k. zitarudi lini? Kwani kuwepo kwa barabara ya lami ndio meli basi?
  8. Waenda kwa miguu: Mheshimiwa hawa pia wanahatarisha usalama barabarani, hawafuati alama za pundamilia, wanajivukia popote. Magari yanaanza kuondoka wao ndio wanavuka. Kuwepo na elimu ya makusudi mashuleni, vyuoni na pahala pa kazi juu ya usalama barabarani kwa waendao kwa miguu. Hawa pia wapewe adhabu wanapokosea. Unaonaje hili Mheshimiwa?
Mheshimiwa kwa heshima na taadhima najua sitopata majibu hapa lakini hakika nategemea majibu toka kwako kupitia vyombo vya habari wakati maafisa wako wanatekeleza yale niliyokuomba. Allah akipenda siku moja nitapata nafasi ya kuongea nawe, mola na mja wetu atakapokujalia kukupa uhai na utashi wa kupokea maswali toka kwetu wananchi wako.

Wasalaam, Chereko.
 
Last edited:
Back
Top Bottom