Napenda kukupa pole kwa hayo yaliyokukuta kwani ni sehemu ya maisha. Mshukuru sana Mungu kwa kuruhusu maamuzi hayo kufanyika, huwezi jua angefanya nini hapo baadaye. Kuna wachumba wanatambulishwa, vikao vya harusi vinakaa na michango inakusanywa kisha binti anaghairi ama anatoroshwa na mwanaume mwingine si hivyo tu kuna wengine wanaingia mpaka kanisani kufunga ndoa kisha inashindikana na kubakia historia, kibaya zaidi kuna wengine mpaka wanaoa na maisha huendelea lakini mwishowe ndoa huvunjika, naomba uyatafakari hayo.
Ninachotaka kukuambia ni kwamba maisha yapo na yataendelea, hata mapenzi pia yapo na yatendelea kuwepo. Unatakiwa kukubali matokeo pale inapotakiwa kufanya hivyo ili uweze kuendelea na mambo mengine yenye manufaa kwako. Jiulize uliishije kabla ya kukutana naye stendi na kwanini ushindwe wakati huu? tambua kuwa wanawake wapo wengi sana tena wazuri wa sura na tabia hata kumzidi huyo aliyekuacha, usikubali kuumiza moyo wako kwa mtu ambaye unajua fika kuwa si lazima uwe naye wewe ndo maisha yaende.
Nahitimisha kwa kusema kuwa wewe una thamani kubwa sana katika ulimwengu huu na upo kwa sababu, hivyo usikae na kupoteza furaha kwa mambo ya kupita. Andaa maisha yako kwanza kwa ajili ya manufaa yako binafsi, familiya, jamii na taifa kwa ujumla, ukiendekeza mapenzi hakika unaweza changanyikiwa na kujikuta hujafanya chochote cha maendeleo na mwishowe hata mke mzuri utamkosa maana hata kujiamini utashindwa na yeye atashindwa kukuelewa. Usiruhusu mpenzi wako wa sasa asababishe uishi maisha ya taabu na mkeo iwe ni kwa matatizo ya kisaikolojia ama kimaisha. Msamehe bure songa mbele utampata wako na maisha yatakunyokea.