Nimekutana na article hii nzuri by Vitali Maembe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nimekutana na article hii nzuri by Vitali Maembe

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Kalambo, Mar 24, 2011.

 1. K

  Kalambo Member

  #1
  Mar 24, 2011
  Joined: Oct 28, 2010
  Messages: 10
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 3
  Hotuba ya mfungwa Mswahili|Na Vitali Maembe, Berlin


  Ndugu waheshimiwa na wote msioheshimiwa!


  Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kuniweka hai na kunitia nguvu. Hii ni hotuba ya kwanza kabisa ya mfungwa Mswahili kwa watu wote, naiandika huku nikiomba Mungu iwafikie ikiwa hivi nilivyoiandika, lakini sijui kama itawafikia wakati bado mwili wangu umeambatana na roho yangu.


  Ndugu zangu, jela inatuumiza! Mimi ni mfungwa, kuwa mfungwa haimaanishi kuwa ni mtu mwovu bali ni mtu aliyeonwa na sheria. Hapa nilipo ni mahala muhimu sana, ni mahala pa kujenga. Ingawa wengi hutoka wakiwa wamebomoka na kuharibika kabisa, wamepoteza afya ya roho, akili na mwili.


  Jela inawaumiza wanetu, jela inawaumiza wazazi na wapenzi wetu ingawa hawapo kifungoni. Jela inaiumiza nchi yetu. Ndugu zangu kuna umri wa kufundishana adabu lakini kwa nafasi hii niliyoipata wacha niitumie kwa kazi hii ingawa umri wenu umeenda! Nafanya hivi makusudi kwa kujua kabisa kwani hata waswahili wamenionya kuwa samaki mkunje angali mbichi, akishakauka utamvunja bure upate lawama.


  Ndugu waheshimiwa, jiheshimuni, waheshimuni na wengine ili muheshimike kihalali! Nanyi msioheshimiwa muwaheshimu wenzenu na mamlaka zilizowekwa, jiheshimuni pia ndipo mdai heshima. Naomba nieleweke nimesema kuwa nimesema kuheshimu, si kuogopa au kuabudu. Nitaongea kwa mipaka ingawa leo nimepewa uhuru wa kuongea. Waswahili wamenionya kuwa Uhuru usio na mipaka ni utumwa. Haki ya nani Sijaona lugha tajiri kama hii.

  Ndugu zangu! Nilikuwa nasubiri kutolewa huku kwa msamaha wa rais nije kuongea nanyi ana kwa ana lakini bahati haijawa yangu labda mwakani. Jamaa zangu chonde nawaomba mseme na roho zenu, Mungu ajaalie tuonane nyumbani tukiwa hai wote, tujenge taifa lililo jema.


  Maisha ya jela ni magumu na ya hatari, lakini kuna wakati tunapata nafuu, hasa pale wanapoletwa wakubwa huku ndani, mlo unabadilika na dawa za mbu zinapulizwa, uji sukari kibao na maji safi kama kawaida, lakini tatizo hawakai sana… hata hivyo msemo wa Kiswahili huwa hauachi kutimia "mgeni njoo mwenyeji apone".

  Nduguzangu! kama nitajaaliwa kutoka tutaonana nyumbani, ila sina matumaini sana maana wenye nguvu wameshaanza kunipiga kwa siri, kama roho yangu ikiachanishwa na mwili basi msisahau kuwaambia watoto wa leo kuwa Tanzania mpya ipo, Tanzania mpya bora ipo, ila wajikaze na waishike vizuri adabu yao.


  Mheshimiwa mwongozaji!
  Sikia sauti ya kilio cha Mswahili tangu kwenye sakafu ya moyo wake. Sikiliza bwana mkubwa, tutazame, nyuso zetu watanzania hazijui kudanganya, zinazungumza hali waziwazi tena kwa lugha nyepesi kabisa!


  kuna kitu tumefanyiwa hapa! Sijui ni kwa ubaya au kwa wema lakini ukweli ni huu. Mmekamata vyombo vya habari, mmetukamata makoo, mnavipa ruhusa baadhi ya vyombo vya habari kuua maadili na utamaduni wetu! Mmeharibu mfumo wa elimu, halafu
  Mnatutishia dini mnafikiri hatujui Mungu anataka nini?


  Mnatutishia madaraka mnatufanya hatuijui siasa safi ikoje? Nakumbuka nilipokuwa shule ya vidudu si chekechea, tulipofundishwa, mwalimu akiingia darasani monita anasema Heshma! Wote tunasimama na kusema, "Ili tuendelee twahitaji vitu vinne, watu ardhi siasa safi na uongozi bora sisi vijana wa ccm tupo tayari kujenga taifa… shkaaaa mooo mwaalimu!" wakati huo ukisema nasema kweli tupu na chama kinilinde chama kinakulinda kweli. Kipindi hicho vtuo vya polisi haba mtuhumiwa akipatikana kwanza anafungiwa kwenye ofisi ya chama unasikia watu wanasema ‘kapelekwa zoni'


  Ulaaniwe kujua, kujua si kwema, maana ningekuwa mjinga nisingepata shida akilini na moyoni kama hivi. Nimeishia darasa la nne tu nateseka hivi, je ninge…. Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo. Tunatarajia elimu ndiyo ituokoe lakini elimu yenyewe mitaala hailingani na maisha ya kweli! Kila kitu mnakitia siasa, mnakifanya biashara.


  Utajiri wa nchi yetu ndicho chanzo cha mateso kwetu. Hatufurahii maisha ndani ya nchi nzuri tuliyoachiwa na baba zetu. Hivi, ni lini mtatupa fursa ya kuishi maisha yetu? Ni lini tutafurahia uhuru wa nchi yetu? Tangu nchi inapata uhuru mpaka leo nchi inafikia nusu kalne, inahitaji uhuru mpya bado pua zetu hazijahisi hata kwa mbali harufu nzuri ya maendeleo. Mnatuonyesha kuwa njia rahisi ya mtu kuendelea ni kuwa mhalifu, sasa mnafikiri tutapungua huku jela?


  Alafu nilitaka kusahau, niliona mambo yanaharibika nikaomba kusaidia mapambano dhidi ya rushwa nikaambiwa si kazi yangu, niliumia sana. Alafu na wewe muweka kanda, nani kakupa kibari cha kazi hiyo wakati hujui unachofanya? Mnaona hii nchi ya kishkaaji sio? Hujakatazwa kupiga muziki wa waswahili redioni lakini nikikuletea ooh nisamehe kaka… maneno ya nyimbo zako hayatawafurahisha waheshimiwa… huu si wakati wa kufurahishana huku nchi inaangamia, unaleta usomi wako wa kishamba bwana! Wamekuambia hawataki kusikia sauti ya kweli ya mswahili?

  Acha kujipendekeza wewe! Unajua kazi ya muziki wewe? Au unafikiri kazi ya muziki ni kujaza ukumbi wa disko na kuvutia watu kwenye kampeni? Ukome kujipendekeza, kama hujui hata wao waheshimiwa wana haki ya kuburudika, kujifunza na kusikia sauti za ukweli. Usiwanyime haki yao ya kupata taarifa, elimu na burudani.


  Viongozi wangu wapendwa!
  Mliniziba mdomo Watanzania wenzangu wasinisikie kwakuwa siendani na matakwa yenu. Mkaweka uadui kati yangu na wenzangu.
  Mkawapa nafasi wanamuziki wanafiki ili wawafichie uovu wenu, nyimbo za matusi zinaimbwa wazi wazi nanyi mnazichukulia poa tu.
  Eti maendeleo, Chuo cha Sanaa Bagamoyo kinakufa mnajifanya hamuoni, Chuo Kikuu Dar es Salaam kinazalisha matakataka mnachekacheka tu! Subirini kidogo muone matokeo ya bomu mnalolitengeneza.


  Mnaandaa mitaala ya elimu ya kuwajaza ujinga watu, mtu amehitimu lakini bado yuko uchi akilini. Heri mimi sikusoma kabisa. Ila najua kuhesabu hela. Wenye makucha makubwa wanatutesa, wanajificha nyuma ya siasa, biashara na dini, watushambulia wanyonge bila huruma.


  Halafu na nyinyi waumini mimi ndio nimewatoa maana kabisa kwa unafiki wenu! Na kwenye nyumba zenu za ibada mnifukuze kabisa mkitaka! Mungu atanipokea na kuwaaibisha wanafiki wakubwa nyie… mtu anasimama kashika katiba na kitabu cha Mungu wenu, anaapa kwa jina la Mungu halafu anaenda kinyume cha kiapo chake kisha nyie mnamkenulia meno tu, mnajua maana ya kiapo nyie? Sawa katiba imepitwa na wakati, biblia na msaafu je? Mnashindwa kusimama kwa ajili ya jina la Mwenyezi Mungu mtasimama kwa ajili ya nani?


  Nitasahau kusema yote lakini hili ntalisema kabla sijafa, Tanzania inataka katiba ya kitanzania, katiba ambayo si ya kikoloni, katiba ya zama hizi, ambayo hata tukiongozwa na bora kiongozi itamfanya aonekane ni kiongozi bora. Katiba itakayo tuongoza kwenye maendeleo ya kweli, kumheshimu Muumba aliyeamua kuusimamisha Mlima Kilimanjaro, akaiweka Ngorongoro na kutuzawadia bahari, akatupa Ziwa Tanganyika, Nyasa, Rukwa, akajaza utajiri ardhini. Katiba itayoruhusu tume huru ya uchaguzi na pia taasisi huru ya kuzuia rushwa.


  Nendeni mtoni mkaoshe akili na roho zenu ubinafsi umewachafua.. nasema mimi mfungwa Mswahili, ashindikene! Mimi si yule msaliti anayesubiri nauli wakati aendapo ameshafika! Wala sina ujamaa naye, mie sitangazi ujomba ili nibebwe. Msinichanganye kwanza nna mwiko wa kuchanganika na watu wanaoupenda sana uhai wao kuliko kuishi kwao.


  Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo. Siogopi maumivu mliyoniandalia, mimi ni marehemu niliyerudishwa kwaajili ya mswahili aliaye shidani? Mtu hafi mara mbili bwana. Ndimi ashindikene bwana, kaulize Bagamoyo, mimi pilipili, mimi dawa chungu.


  Nimetumwa naye mwenye uwezo wa kuumba na kuumbua anasema kwamba huu ndio wakati pekee ambao sauti na na kalamu zetu zinaweza kuiokoa nchi yetu kabla halijachwa jua la amani hii. Ndugu wanafiki wafanyabiashara wa muziki, maadui wa utamaduni wetu wabinafsi na waabudu pesa wote!


  Msijisumbue kunitishia umasikini, mkafikiri mtanibadilisha, mimi vita yangu si ya utajiri na mali, sikuja na mizigo wala sihitaji mizigo katika kuondoka kwangu, nilikuja uchi kutoka tumboni mwa mamaangu nitarudi uchi katika tumbo la nchi. Heshima ya nchi hii ya babaangu itarudi, kwa vyovyote na kwa gharama yoyote, kikiharibika kitu babaangu atarekebisha, na sita kufa tena niwaache wanangu na njaa. Mimi si masikini na kila mtanzania aliyezaliwa baada yangu si mtoto wa masikini.

  Na njaa itamheshimu.
  Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… tofauti ipo. Na wote mliotuibia imekuwa vema hatukufundishwa kushika silaha, na Muumba atunusuru na hilo, lakini ole wao watoto na wajukuu zenu, sijui wataoga wapi hata shombo na vumba la uozo wenu liishe, maana wanakuja watoto wetu hodari, wala nyuki, nyoka waumao usiku.


  Mungu wangu, ulisha ibariki Tanzania Mungu ulishaibariki Afrika Mungu usituondelee Baraka hii. Sina haki sana ya kupewa kila nitakachoomba lakini kwa neema zako naamini utanijaalia kwa ajili ya Tanzania yako. Tofauti ipo! Tofauti kati ya baraka na laana… tofauti ipo. Watie aibu maadui wa mtumishi wako. Amlaaniye uliyembariki laana yake imrudie.


  Vitali Maembe ni msanii wa muziki. Ni mtunzi pia wa nyimbo mbalimbali aliyenolewa katika Taasisi ya Sanaa Bagamoyo. Kwa sasa yuko ziarani katika nchi kadhaa barani Ulaya.
   

  Attached Files:

 2. Mphamvu

  Mphamvu JF-Expert Member

  #2
  Mar 25, 2011
  Joined: Jan 28, 2011
  Messages: 10,708
  Likes Received: 934
  Trophy Points: 280
  Dah, ukweli mtupu! Haya ndio matunda ya sanaa halisi ya Kaole... Sio kina Diamon... Domo kazi kuzunguka na kampeni fulani fulani bila kujua unahitaji nini! Big Up Vitali, Big Up Mwasilishaji!
   
 3. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #3
  Mar 25, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  thank you article imeenda shule sana hongera vitali
   
 4. Raia Fulani

  Raia Fulani JF-Expert Member

  #4
  Mar 25, 2011
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 10,219
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Hongera Maembe. Umelenga ikulu, ila sijajua alikuwa na mood gani wakati anaandika hii article
   
 5. RealMan

  RealMan JF-Expert Member

  #5
  Mar 25, 2011
  Joined: Nov 9, 2010
  Messages: 2,352
  Likes Received: 160
  Trophy Points: 160
  Vitali ni kichwa cha ukweli.
  Maneno yenye ujumbe wa kweli, tatizo watawala wanaumwa maradhi ya kutoona na kusikia. Hili pia hawataliona wala kusikia
   
 6. Wa Ndima

  Wa Ndima JF-Expert Member

  #6
  Mar 25, 2011
  Joined: Aug 13, 2010
  Messages: 1,512
  Likes Received: 39
  Trophy Points: 145
  nimemkubali
   
 7. Ndibalema

  Ndibalema JF-Expert Member

  #7
  Mar 25, 2011
  Joined: Apr 26, 2008
  Messages: 10,916
  Likes Received: 131
  Trophy Points: 160
  Huyu ndiye aliyeimba "sumu ya teja"?
  Naona anapenda sana kuongelea stori za jele jela tuu.
   
 8. Mphamvu

  Mphamvu JF-Expert Member

  #8
  Mar 25, 2011
  Joined: Jan 28, 2011
  Messages: 10,708
  Likes Received: 934
  Trophy Points: 280
  Sure? Naona tofauti kati ya wasanii shule na wasanii wanaotolewa na Sharobaro President...
   
 9. Seto

  Seto JF-Expert Member

  #9
  May 19, 2013
  Joined: Jan 15, 2011
  Messages: 961
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  huyu ni baadhi ya wasanii wachache wanaojielewa....
   
 10. Who Cares?

  Who Cares? JF-Expert Member

  #10
  May 19, 2013
  Joined: Jul 11, 2008
  Messages: 3,465
  Likes Received: 1,950
  Trophy Points: 280
  Hicho kichwa kingine..full harakati za ukombozi wa mtanzania aneyejiona huru ilhali yuko katikati ya utumwa wa kifikra na umasikini wa mawazo chanya unaosababishwa na wahishimiwa wasiojiheshimu ili kulinda heshima kidogo wanayopewa na waheshimia ...big up vitali...nabii asiyekubalika nyumbani kwao.
   
 11. Nyanidume

  Nyanidume JF-Expert Member

  #11
  May 19, 2013
  Joined: Oct 24, 2012
  Messages: 2,156
  Likes Received: 379
  Trophy Points: 180
  Hakika ni hotuba nzuri yenye kuonyesha ni jinsi gani watawala wetu walivyojisahau na kujiona wao ni miungu watu ambao hawapaswi kukosolewa. Vitalis ni mmoja wa wasanii wa ukweli ktk muziki wa Tanzania!
   
 12. M

  Masuke JF-Expert Member

  #12
  May 19, 2013
  Joined: Feb 28, 2008
  Messages: 4,606
  Likes Received: 108
  Trophy Points: 160
  Big up Sumu ya Teja.
   
 13. N

  Ngakayu Senior Member

  #13
  May 19, 2013
  Joined: Apr 26, 2013
  Messages: 109
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Ulikuja uchi kutoka kwa mama yako! Ujumbe fika lakini watawala wetu wanatumia pesa kupata uongozi. Nimekukubali wewe ni nabii wala si msaani. Mabadiliko ya kweli yapo yanakuja. Nguvu na mamlaka ya umma itarejesha raslimali zilizoporwa!
   
 14. B

  Ba Brio Member

  #14
  May 20, 2013
  Joined: Mar 19, 2012
  Messages: 78
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 13
  mzee imekaa sawa hii. hivi ni vinywa vichache sana katika nchi hii vilivyojaliwa kutamka ukweli bila woga. kichwa kizuri na hekima ya ki mapinduzi ndani yake. Big up bro. keep shouting..... paza sauti kwa nguvu usikike. kwa kuwa umeyavulia yafaa uyaoge kabisa. najua utakandamizwa kabla sauti yako haijafika mbali; lakini jaribu kupayuka kwa nguvu zaidi walau wasikie hata walioko jirani ili wapeleke ujumbe! nimegusika sana lkn mzee.
   
 15. ndendi

  ndendi JF-Expert Member

  #15
  May 20, 2013
  Joined: Nov 29, 2012
  Messages: 628
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 35
  jamaaa namkubali sana,ila nyimbo zake sizisikiii redioni,sijui kwa nini?
   
 16. ngalelefijo

  ngalelefijo JF-Expert Member

  #16
  May 20, 2013
  Joined: Jun 26, 2012
  Messages: 1,800
  Likes Received: 761
  Trophy Points: 280
  Asante imesimama
   
 17. r

  rodrick alexander JF-Expert Member

  #17
  May 20, 2013
  Joined: Feb 12, 2012
  Messages: 4,109
  Likes Received: 1,497
  Trophy Points: 280
  Jamaa ni kichwa niliwahi kukutana naye chuo cha sanaa bagamoyo ni msanii mwenye mtazamo wa mbali kuanzia nyimbozake mpaka maelezo yake ndio maana kila siku amekuwa anapata mialiko nje ya nchi badala ya wauza sura kwenye magazeti
   
 18. Denis Kasekenya

  Denis Kasekenya JF-Expert Member

  #18
  May 20, 2013
  Joined: Jan 3, 2013
  Messages: 550
  Likes Received: 73
  Trophy Points: 45
  "SITANGAZI UJOMBA ILI NIBEBWE". . .nimeipenda
   
 19. t

  tizo1 JF-Expert Member

  #19
  May 26, 2013
  Joined: Mar 9, 2011
  Messages: 857
  Likes Received: 47
  Trophy Points: 45
  dah inauma sana?
   
 20. M

  MUME MWEMA JF-Expert Member

  #20
  May 26, 2013
  Joined: May 16, 2013
  Messages: 327
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Mbona mm nina audio ya hotubu hii na imesomwa na Mpoki! Mpoki ndiye Vitali maembe? Au alimpa mpoki aisome? Plz naomba kujuzwa.
   
Loading...