Nilivyomjua Jerry Solomon Sumari-Ulimwengu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nilivyomjua Jerry Solomon Sumari-Ulimwengu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by THE WHITE ELEPHANT, Jan 26, 2012.

 1. T

  THE WHITE ELEPHANT Member

  #1
  Jan 26, 2012
  Joined: Jan 15, 2012
  Messages: 93
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Jenerali Ulimwengu
  [​IMG]  Marehemu Jeremiah Solomon Sumari
  KATIKA mambo mazito yaliyonielemea siku hizi chache ni kwamba nilishindwa kumuaga marehemu Jeremiah Solomon Sumari, Mbunge wa Arumeru Mashariki, aliyefariki wiki iliyopita na kuzikwa juzi Jumatatu. Pamoja na utashi wangu na uchungu niliouhisi nilipopata taarifa ya kifo chake, bado sikuweza kuhudhuria itifaki ya heshima za mwisho Karimjee kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.


  Itoshe, basi, kwamba nimeamua kumuuga kwa staili yangu, kama ambavyo nimekuwa nikiwaaga wenzetu wengine ambao wamenigusa katika maingiliano niliyokuwa nayo nao. Jerry Solomon ni mmoja wa watu hao ambao wamenigusa, hata kama sikumjua kwa muda mrefu sana.


  Kwa mbali nilimfahamu Jerry kama mmoja miongoni mwa wasomi wa nchi hii wenye ujuzi mkubwa wa masuala ya fedha, mitaji na hisa. Huo si uwanja wangu, na hivyo kwa muda mrefu tulipokuwa tukikutana tuliamkiana kwa taratibu za uungwana wa kawaida usiodhihirisha mazoea ya ziada. Hata hivyo alionekana kuwa mtu mchangamfu na mwepesi kukaribiwa watu.

  Nilikuja kumjua vizuri zaidi pale nilipochaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB Bank, mjini Arusha, katika kikao cha mkutano mkuu wa benki hiyo ambaye alikuwa mwenyekiti wake, miaka ya mwanzo ya 2000.

  Kikao cha kwanza tu cha bodi hiyo kilinionyesha taswira ya kweli ya Jerry, kama mtu mwenye ujuzi wa kina wa masuala ya fedha, mitaji, ukopeshaji na usimamizi wa amana na mikopo, na, muhimu zaidi kwangu, mjuzi ambaye hakuona ni adha kurudia maelezo kwa mjumbe asiyeelewa kimsingi masuala haya. Nilihisi kwamba alikuwa akiona raha alipoombwa kurudia jambo alilokwisha kulieleza alimradi mjumbe ‘mugya’ alielewe vyema ili bodi iweze kwenda mbele kwa pamoja. Na mara nyingi aliweza kutoa maelezo hayo kwa kutabasamu na kutoa mifano mingi iliyorahisisha uelewa hata kwa mtu kama mimi.


  CRDB Bank ni benki ya ‘wananchi’ kwa maana kwamba msingi wa mtaji wake unayo sehemu muhimu inayotokana na fedha za wananchi wadogo wadogo, na wengine wakubwa, walizowekeza humo. Hii haiondoi ukweli kwamba, angalau kwa wakati ule, benki hiyo ilikuwa imeimarishwa kwa mitaji mikubwa (nadhani asilimia 30) iliyotokana na uwekezaji wa Denmark, ambayo kwa sababu hiyo ilikuwa na wakurugenzi wawili kwenye bodi.


  Pamoja na hali hiyo kila mara lilipotokea suala la kuwaambia ‘wawekezaji’ hao, hata kama liliwaudhi, Jerry hakusita kuwaambia kinagaubaga, bila kutafuna midomo wala kumung’unya maneno. Isipokuwa tu, kwamba lugha yake ilikuwa ya staha na heshima.

  Ilipofika wakati wa kuwataka wawekezaji kutoka Denmark watathmini kiwango cha ufanisi kilichofikiwa na benki na waangalie uwezekano wa kuanza kuachia ngazi katika kiwango cha hisa zao, napo hakusita kuwaambia hivyo, ingawa jambo hilo hawakulipenda hata kidogo, na baadhi ya wenzangu waliniambia kwamba msimamo wake huo ndio uliofanya aondoke wakati hatukutaraji aondoke. Kwa bahati nzuri kwangu, nami nilikuwa naondoka.

  Alikuwa na uhusiano mzuri na utendaji ndani ya benki, ukiongozwa na Dk. Charles Kimei, na alikuwa mwepesi kuuelekeza, kuukosoa, na wakati mwingine kuukemea kwa lugha ilioyokubalika. Mara nyingi si rahisi kwa bodi kudhibiti mwenendo wa timu ya utendaji iliyokaa katika nafasi kwa muda mrefu kiasi kwamba inaanza kuonekana kama ya kudumu. Hata hivyo alituhimiza tuwatendee haki watendaji lakini wakati huo huo tudai kwamba na wao watimize wajibu wao.


  Kwangu mimi, Jerry alikuwa mjuzi wa masuala ya fedha kuliko watu wengi ninaowajua; angalau aliweza kuyaeleza kwa ufasaha hata mimi nikayaelewa, kidogo. Alifanya hivyo kwa ucheshi na tabasamu, kwa lugha fasaha, na bila kuchoka.

  Alipoingia kwenye siasa mimi nilishangaa, kwa sababu sikumuona kama angeweza kumudu mikikimikiki ya wababaishaji walioiteka medani hiyo, kwa sababu nilimuona kama mtu ‘genuine,’ lakini kwa upande mwingine nikasema ni heri watu ‘genuine’ wengi iwezekanavyo waingie humo na wajaribu kuikomboa sekta hiyo. Kwa kweli sijui, nakiri.

  Baada ya kuwa amechaguliwa kuwa mbunge na akateuliwa kuwa “naibu waziri’ hapo ndipo nikajua kwamba hisia yangu ya awali ilikuwa sahihi. Haikuwa mara yangu ya kwanza kujiuliza maswali juu ya watu wenye uwezo mkubwa ‘wanaodhalilishwa’ kwa kuwekwa katika nafasi za “unaibu” na vitu kama hivyo, lakini nilihisi vikali kwamba hakustahili kuwa ‘naibu’ wa kitu chochote. Lakini
  wako wengine pia, matunda ya mfumo unaotaka kile ambacho mimi sikielewi, na labda wengine wengi hawakielewi.


  Ni masikitiko makubwa kwamba Jerry, ambaye alijali sana afya yake kwani nilimwona akiwa ‘gym’ mjini Arusha na Nairobi tulipokwenda kikazi, na nikashuhudia jinsi alivyokuwa ‘akijipelekesha’ kwenye ‘treadmill.’ Kwamba ndani kwa ndani alikuwa anatafunwa na saratani, nani angeweza kujua muujiza kama huo?


  Bila shaka familia yake itamkosa sana, sana. Wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki watamkosa sana, sana. Nasi tuliomjua huku kiwandani tutamkosa sana, sana. Najua kwamba Jerry Solomon atadumu mahali pema mioyoni mwetu.
   
 2. bucho

  bucho JF-Expert Member

  #2
  Jan 26, 2012
  Joined: Jul 13, 2010
  Messages: 4,541
  Likes Received: 424
  Trophy Points: 180
  R.i.p mzee sumari .
   
 3. TODO

  TODO JF-Expert Member

  #3
  Jan 26, 2012
  Joined: Jul 14, 2011
  Messages: 219
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  RIP Mh sumar
   
 4. B

  Bulesi JF-Expert Member

  #4
  Jan 26, 2012
  Joined: May 14, 2008
  Messages: 6,447
  Likes Received: 414
  Trophy Points: 180
  Very deserving tribute. So long friend rest in peace!
   
 5. K

  KIFILI Member

  #5
  Jan 27, 2012
  Joined: Jan 23, 2012
  Messages: 87
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  R.i.p.mzee sumari
   
Loading...