Ni siku ya kifo cha karume.

anewarick

Member
Jan 17, 2017
19
6
Mauaji ya Sheikh Abeid Karume


Kutoka kitabu Cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi.

(Misheni ya Tatu)

Baada ya kuona namna mwanamapinduzi halisi, Field Marshal John Okello, alivyoondolewa Zanzibar na kupokwa mamlaka na jinsi alivyoongoza Mapinduzi ya mwaka 1964, na kuundwa kwa Serikali ya Mseto kati ya vyama vya ASP na Umma, kuliibuka lengo la Karume la kuzivunja nguvu za wanaharakati wa Umma Party na za wakomunisti wa ASP walioshabihiana kimawazo na kimtazamo wa kitaifa na wana-Umma Party, na hivyo kumnyima Karume usingizi wa pono katika muda mfupi wa utawala baada ya mapinduzi hayo. Lakini, tofauti na matarajio ya Karume, hatua hiyo iliwaleta karibu zaidi wanamapinduzi hao na kumnyima zaidi usingizi kwa hofu ya kupinduliwa, akituhumiwa vikali kushindwa kuongoza na kusimamia madhumuni ya Mapinduzi Visiwani.

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulikuwa nguzo muhimu kwa Karume kujijenga mamlakani. Ili kusafisha njia na kuondoa uchafu aliyoona unamghasi, aliona ni vyema awasambaratishe kwa kuwatafutia nafasi za uongozi Tanzania Bara ambako wasingeweza kufurukuta. Waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Abdulrahman Babu (Umma Party) na Uwaziri wa Mipango na Uchumi kwenye Serikali ya Muungano, Kassim Hanga (ASP) akateuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri, na Mambo ya Muungano na Salim Ahmed Salim (Umma Party) aliteuliwa kuwa Balozi nchini Misri. Wengine ni Othman Sharrif (ASP) aliyeteuliwa Balozi nchini Marekani, lakini Karume akampinga Mwl. Nyerere akidai hastahili, uteuzi ukafutwa. Badala yake akateuliwa kuwa Afisa Mifugo katika moja ya mikoa ya Kusini Tanzania, Mbeya au Mtwara, na Kanali Ali Mahfoudh (Umma Party) akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Operesheni/Mazoezi katika Jeshi la Wananchi (JWT).

Kwa wale wenye maoni tofauti na ya kukosoa serikali hasa kwa waliobaki Visiwani, hasira ya Karume aliyetawala kwa mkono wa chuma iliwashukia. Wengi walikamatwa na kutiwa kizuizini na pengine kupotezwaa au kuuwawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha. Mmoja ya waliouawa kikatili kizuizini ni Mzee (mwanaharakati timamu) Mohamed Hamoud, baba yake Luteni Hamoud Mohamed ambaye baadaye alikuja kumuua Karume.

Juu ya mapinduzi ya Zanzibar na kuuawa kwa Abeid Karume, kumekuwapo na mitazamo mingi kwa watu mbalimbali, lakini nitumie mitazamo ya wanamajumui kadhaa kama vile: Prof Harob Othuman ambaye yeye alilieleza hili katika mtazamo wake; Prof Issa Shivji, naye amelisemea katika jicho tofauti; wakaja wazee wangu wa fikra za near, Mohamed Said na Dr Harith Ghassany katika kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru. Marazini hawa wanarandana kimitazamo, ambamo kwa undani, zinabeba dhanna ya kidini, lakini mawazo tanzu na fikra tunduizi ya Joseph Mihangwa katika andishi lake kwenye gazeti la Raia Mwema la tar. 11 Aprili, mwaka 2012, Toleo Na. 234 – 237, na Toleo la tar. 2 Mai, mwaka 2012 ndio yanabeba dhanna yangu juu ya tukio hili.

Tangu Mapinduzi ya tar. 12 Januari, mwaka 1964, Zanzibar haikuwa na Katiba wala Sheria. Kinyume chake, iliongozwa kwa Amri za Rais Presidential Decrees kwa kadri Rais alivyoona inafaa. Na, kwa mujibu wa Gazeti la The Tanganyika Standard la tar. 9 Machi, mwaka 1968, Karume aliapa kutofanya uchaguzi wala kuwa na Katiba Kisiwani kwa miaka 50, tangu mwaka 1964-2014, kwa madai dhaifu kwamba chaguzi zote ni vyombo vya mabeberu kuwakandamiza wananchi. Na, kadiri kalamu ya Karume ya wino wa damu ilipozidi kuandika historia ya ukatili, udikteta na umwagaji damu kwenye kurasa ngumu za kutu ndivyo alivyojichongea na kujiongezea upinzani mkali na uadui kwa jamii ya Kizanzibari.

Kwa namna fulani, kuanzia mwaka 1964,kulikuwa na vuguvugu ama tuseme harakati za hapa na paleza kupinga utawala wa Karume, harakati ambazo Utawala wa Karume ulitumia mwanya huo kuziita ni majaribio laanifu ya hapa na pale ya kutaka kuiangusha Serikali ya Karume. Thabit Kombo Jecha katika Simulizi anayataja majaribio baadhi, likiwamo lile la Disemba 1964, lililoongozwa na Amour Zahorwa Unguja, la mwaka 1967 likiongozwa na Suleiman Hamad Suleiman wa Pemba, la mwaka 1967 tena, likiongozwa na Saleh Ali Nassor wa Unguja, na la mwaka 1968, likiongozwa na Salim Mohamed Abdullah wa Pemba.

Kufikia mwaka 1967 hofu ya Karume dhidi ya wenzake na kwa nafasi yake ilitia fora kiasi cha kuogopa kivuli chake mwenyewe. Na ili kuendelea kuwamaliza wenzake, mwaka huo, zilitungwa tuhuma za uongo dhidi ya watu kumi na wanne (14) ambao ni makada waandamizi wa ASP, kutaka kumpindua, zikiwalenga hasa wenye fikra za kikomunisti.

Walioingizwa kwenye tuhuma hizo ni pamoja na Mawaziri wa Serikali yake mabwana Abdallah Kassim Hanga, Salehe Saadallah Akida, Abdul Aziz Twala; Makatibu Wakuu wa Wizara, Aboud Nadhif na Mdungi Ussi; na baadaye Othman Sharrif. Wote waliokuwa Visiwani walikamatwa, kisha wale waliokuwa bara, Karume akamuomba Mwl. Nyerere kuwarejesha Zanzibar ambapo ombi hilo la lazima liliwakumba ndugu Othman Sharrif na Kassim Hanga ambao walitakiwa hima fa hima warejeshwe Zanzibar ili wakahojiwe lakini wote wakaishia kuuawa kikatili baharini bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mmoja wa Mashahidi Bandia walioandaliwa dhidi ya watuhumiwa kwa vyombo vya Karume, alikuwa Ahmada ambaye kwa uongo wake uliokubuhu, watu wanne akiwamo Hanga, Twala, Saadallah na Othman, walinyongwa mwaka 1969. Kwa uongo huo, Ahmada alizawadiwa Cheo cha Kapteni, jeshini. Ni Kapteni Ahmada huyu, aliyeshiriki kwenye mauaji ya Karume miaka mitatu baadaye. Kwa hofu ya jamii ya Kizanzibari kufikiwa na fikra na mawazo mapya ya kimaendeleo, Karume alipiga marufuku vijana wa Kizanzibari kwenda nje, kwa masomo ya juu, ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Hakuishia hapo, pia alipiga marufuku ya ujenzi wa Chuo Kikuu Visiwani.

Mbali na kutokuwapo kwa utawala wa sheria enzi za Karume, unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa misingi ya historia na kisiasa ulitia, ulipewa kipaumbele kama ilivyokuwa kwa Makaburu huko Afrika ya Kusini. Kwa mfano, mwaka 1966, Karume alitoa amri kuwanyima wazazi haki ya kuwakataa wanaume walioposa binti zao kama njia ya kuondoa ubaguzi wa rangi. Kwa sababu hii, wasichana, hasa wale wa Kiarabu walilazimishwa na Serikali, kuolewa kwa nguvu.

Wakati huo, Karume mwenyewe, akiwa na umri wa miaka 65, aliwania kuoa kwa nguvu, wasichana wanne wa Kiajemi, na alipokataliwa, aliamrisha wazazi wao watiwe kizuizini na kuchapwa viboko kwa kosa la kuzuia mpango wa ndoa mchanganyiko, na baadaye kutimuliwa Zanzibar. Chini ya mpango huo, raia wa kigeni waliotaka kuchumbia wasichana wa Kizanzibari walitakiwa kuilipa Serikali kiasi kikubwa cha fedha bila hivyo hawakuruhusiwa kuwaoa. Yaani ni sawa na kusema, wanawake wa Kizanzibari walikuwa sehemu ya rasilimali mbichi za nchi ambao walipaswa kuuzwa au na kutozwa kodi kama zilivyo mali nyingine za asili kama samaki, n.k.

Kiburi cha madaraka kilipokolea, Karume alianza kuwa mwiba kwa Mwl. Nyerere, hasa juu ya Muungano. Kwa mfano, alimkatalia Mwl. Nyerere kwa lugha ya dharau na bezo juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha kutumika Zanzibar. Na kuhusu akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar iliyofikia dola milioni 80 mwaka 1972, alimpa Mwl. Nyerere onyo kali, asithubutu kuitolea macho, akamwambia: “Fedha ya kichwa cha Malkia si yako na usiniulize, labda niulize juu ya hii (sh.) yenye picha ya kichwa chako.” Na kuhusu Muungano, Karume alianza kuchoka nao. Siku moja alisema, “Muungano ni kama koti tu; likikubana unalivua.”

Ufa huu kati ya viongozi hao wawili juu ya Muungano, ndio uliosababisha Kamati ya Kupendekeza Katiba isiundwe na Bunge la Katiba lisiteuliwe ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu Muungano, kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa Sheria ya Muungano ya mwaka 1964. Wadadisi wa mambo ya siasa wanakubaliana kuwa, kama Karume angeendelea kutawala miaka kadhaa baada ya mwaka 1972, Muungano ungefikia kikomo kwa njia ya kutisha na kusikitisha.

Kufikia mwaka 1972, upinzani kwa Serikali ya Karume ulikwisha chukua harakati za uasi wa umma, chini kwa chini, kwa mara ya kwanza tangu Hanga na wenzake wanyongwe mwaka 1969. Kwa vigezo vyovyote vile vya utawala na uongozi, Karume alitawala kwa mkono wa chuma cha pua. Alitawala kiimla (utawala mkavu wa unyama) katika nyanja zote za maisha ya Wazanzibari kisiasa, kiuchumi na kijamii!―, pia alikuwa kero kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwl. Nyerere dhidi ya Muungano.

Kwa kusema haya, kitabu hiki hakitafsiri kwamba Karume hakutenda mema kwa Zanzibar na kwa Wazanzibari, bali kinajaribu kutafiti tu kuona ni mazingira na sababu zipi zilizochochea na kuharakisha kuuawa kwake. Ama huenda kati ya sababu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimuungano ndizo zilizoharakisha kifo chake. Tunajua kwa mfano, kwa baadhi ya Wazanzibari, Karume alitawala kikatili, mzandiki asiye na huruma wala hakujua kusamehe. Kwa upande mwingine, alikuwa na sifa za pekee nzuri kama kiongozi na binadamu; alikuwa mhimili na mtetezi wa Waafrika wa Kizanzibari na hakuyumbishwa na siasa za migogoro Visiwani. Alikuwa mwenye fikra zenye kujitegemea, alifanya maamuzi yake bila woga wala kuhofia matokeo; alikuwa kiongozi mwenye kuthubutu na mwenye kujituma.

Licha ya Karume kuitawala Zanzibar kwa mkono wa chuma cha pua, na namna alivyowaengua wote aliodhani hawakuwa upande wake ama kwa kuwahamishia kwenye Serikali ya Muungano, ama kwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, jamii ya Kiarabu wasio Wazanzibari, iliamriwa kuondoka, na wale Waarabu raia waliobaki, waliishi chini ya jicho kali la Serikali; waliweza kukamatwa, kama Wazanzibari wengine na kutiwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka. Walifanyiwa jinsi serikali ilivyofikiri inafaa; mashamba na mali zao zilitaifishwa bila kufidiwa. Wapo waliohukumiwa na Mahakama ya wananchi, kifungo na kuchapwa viboko. Kuonesha kwamba Serikali ya Karume haikuwa ya mchezo mchezo, akaionya jamii ya Ki-Athnasheri wa Kiajemi kwamba kama wangeendelea kuleta mgogoro, wangefukuzwa wote Zanzibar licha ya kuwa raia.

Karume alitangaza utawala wa chama kimoja cha ASP na kuamrisha kila Mzanzibari mtu mzima, kuwa mwanachama. Kila familia ilitakiwa kutundika picha ya Karume nyumbani, na ambaye angekaidi, alikuwa amefanya kosa la jinai lenye kustahili adhabu kali. Kikosi cha Usalama wa Taifa chini ya Kanali Seif Bakari, kilichopewa jina la Viwavi Jeshi, kilichofunzwa Ujerumani Mashariki kikaiva kwa mbinu za utesi na mauaji, kilipewa mamlaka ya kukamata, kutesa, kutia kizuizini na hata kuuwa bila mashitaka (yaani sheria iliwapa haki ya kua kama haki nyingine). Yeyote aliyelalamika, hata juu ya upungufu wa chakula tu, aliitwa adui (au mchochozi kama ilivyo sasa) wa Mapinduzi na hivyo mhaini. Enzi hizo, nduguyo akigongewa mlango usiku na kutakiwa kwa mahojiano na Serikali, usingemwona tena milele na milele.

Wakati wa Karume, wakati wa mkono wa chuma, hapakuwa na utawala wa Sheria wala Katiba. Amri za Rais ndizo zilizotawala nchi. Mapema mwaka 1966, mfumo wa mahakama wa kawaida ulipigwa marufuku; na Oktoba 1966, Rais alijipa madaraka ya kuteua mahakama maalumu za watu wasiozidi kumi na wanne (14), wenye mamlaka ya kusikiliza kesi za makosa ya kisiasa kama vile uhaini, uhujumu uchumi na wizi wa mali ya umma.

Mahakama hizi hazikufungwa na kanuni zozote katika kusikiliza kesi; huduma za kisheria kwa watuhumiwa zilifutwa na mawakili kupigwa marufuku Zanzibar. Upande wa mashitaka ndio uliokuwa upande huo huo wa utetezi. Yaani, mwendesha mashtaka wa serikali alipomaliza kuwasilisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa, aligeuka kuwa mtetezi wa mtuhumiwa huyo huyo. Ilikuwa vichekesho vya kutamausha. Mahakama hizi zilipewa uwezo wa kutoa hukumu ya kifo, iwapo waliona adhabu nyingine ni nyepesi kwa mtuhumiwa.

Mwaka huo huo (1966), Baraza la Mapinduzi lilipiga marufuku haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki [EACA] na rufaa zote zikawa kwa Rais Karume pekee. Mwaka 1970, Karume alipitisha amri ya kuanzishwa mahakama (za kienyeji) za watu watatu. Mahakimu wapya wa mahakama hizo waliteuliwa na Karume mwenyewe kutoka miongoni mwa makada wa ASP. Moja ya sifa ya kuteuliwa ni kutokuwa msomi wa sheria, na ikiwezekana uwe hujui kusoma na kuandika. Adhabu ya kifo ilipanuliwa kuingiza makosa kama vile utoroshaji wa karafuu, uhaini na utoaji mimba. Matumizi ya vidonge vya uzazi wa majira, nalo lilikuwa kosa kubwa.



Mwaka 1971, Karume alichochea hasira na chuki kubwa ya Wafanyibiashara wa Kiasia pale alipowapa agizo la mwaka mmoja, kufungasha virago kwa madai ya kuonekana kudhibiti uchumi wa Zanzibar. Hasira yao iliungana na ile ya Waarabu ugenini waliofukuzwa mwaka 1964, na kupokonywa mali na mashamba yao bila kulipwa fidia, achilia mbali wale ambao mabinti zao waliozwa kwa nguvu kwa Wazanzibari Waafrika. Wakati huo huo, Karume aliendelea kuwaachisha kazi na kuwatimua Visiwani, watumishi wa serikali waliojulikana au ndugu zao kuwa wafuasi wa zamani wa vyama vilivyopigwa marufuku vya ZNP na ZPPP na nafasi zao kujazwa na watiifu viherehere kwake. Hata hivyo, kwa huruma ya Mwl. Nyerere, walipewa utumishi serikalini Tanzania Bara.



Kwa mara nyingine, mapema mwezi Januari, mwaka 1972, Waziri mdogo, Ahmed Badawi Qualletin, na Afisa mwingine wa Serikali, Alli Sultani Issa, walifukuzwa kazi. Kisha, Februari, mwaka 1972, ujumbe mzito wa watu sita ulitumwa kwa Mwl. Nyerere kumwambia awarejeshe Zanzibar, Abdulrahman Babu na wenzake kadhaa wakahojiwe kwa tuhuma za kutaka kuiangusha Serikali. Babu ambaye alikuwa bado mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa Zanzibar, na aliyeamua kutorejea Zanzibar ya Karume kwa kuhofia usalama wake, kivuli chake na mzimu wa wahanga wa ukatili vilimtisha na kumnyima usingizi Karume, mithili ya Macbeth kwa mzimu wa Mfalme Duncan na Banquo, aliowaua kwa upanga ili atawale.



Mwl. Nyerere, kwa kuhofia yaliyompata Hanga, Twala, Othman Sharrif na wengine tokea alipowarejesha Zanzibar mwaka 1967, safari hii alikataa kumrejesha Babu Zanzibar, ingawa alikubali shinikizo la Karume la kumwachisha uwaziri katika Serikali ya Muungano. Hatua za kuwakosa wakina Babu na wenzie zilipodunda, Karume aliwatimua wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufunga Kituo chao cha Utafiti na Udhibiti wa Malaria Visiwani, kwa madai kwamba, Wazanzibari walikuwa malaria proof, yaani hawaguswi wala kuugua malaria.



Kwa hatua hiyo, ugonjwa wa malaria uliongezeka kwa asilimia arobaini na tano (45&). Na ingawa Zanzibar ilikuwa na akiba kubwa ya fedha za kigeni, zaidi ya pauni za Uingereza 14 milioni, kwenye Benki ya Urusi mjini London, (taarifu nyingine zinadai dola 80 milioni), Karume hakuwa tayari kutumia fedha hizo kudhibiti malaria wala kuagiza chakula. Badala yake akaona umuhimu zaidi kuanzisha Kituo cha Utangazaji cha Rangi na ya pekee barani Afrika, wakati huo. Mwaka huo huo (1971), katikati ya mrindimo wa njaa Visiwani, Karume alipiga marufuku uagizaji wa chakula (mchele, sukari, unga wa ngano) kutoka nje, kama hatua ya kujitegemea kwa chakula.



Hatua hii ilizua tafrani na malalamiko na kusababisha biashara ya magendo ya chakula kushamiri. Hapo cheche za Viwavi Jeshi na mahakama za kangaroo zililipuka, yaani wahanga walikamatwa, kushitakiwa na kunyongwa. Watu wengi wakaikimbia Zanzibar. Aprili, mwaka 1972, ukosefu wa chakula ulikithiri. Ni wakati huo huo, Karume alipouawa ghafla.



Kwa yote hayo, pamoja na tabia yake ya kutoamini wasomi na kuchukia wataalamu, hatimaye Karume alianza kuchukiwa na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, wenye siasa za mrengo wa ki-Karl Marx. Mwl. Nyerere alikuwa ameyatoa sadaka mambo mengi ya Tanganyika kwa Zanzibar, ilimradi tu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ufikiwe. Kwa mfano, Tanganyika ilipoteza hadhi ya kuwa nchi na baadaye jina lake, pale Muungano ulipobadili jina kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tan-zan-ia, huku Zanzibar ikabakia kuwa Zanzibar, na Karume akabakia Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.



Si hivyo tu, Wazanzibari watano walipewa uwaziri kamili katika Baraza la Mawaziri kumi na wanne (14) la Muungano. Na, ingawa idadi ya Wazanzibari ilikuwa asilimia tatu (3%) tu ya Watanganyika, lakini Zanzibar iliruhusiwa kuwa na Wabunge hamsini na wawili (52) katika Bunge la Muungano, wakiwamo Wajumbe wote thelathini na wawili (32) wa Baraza la Mapinduzi. Licha ya upendeleo huu, Mwl. Nyerere hakufanikiwa kudhibiti mhimili wa kisiasa Zanzibar chini ya Karume. Mfano, Zanzibar chini ya Karume, ilikataa kuhamishia kwenye Muungano mambo mengi yaliyopaswa kuwa chini ya Serikali ya Muungano mathalani Zanzibar iliendelea kudhibiti Jeshi lake la Ulinzi na Idara ya Uhamiaji, Karume akiwa amiri jeshi wake Mkuu. Ndiyo kusema, aliuawa na wanajeshi wa jeshi lake la Zanzibar, si Wanajeshi wa JWTZ? Karume alikataa Serikali ya Muungano kugusa akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar, japokuwa fedha lilikuwa jambo la Muungano.



Aidha, Karume na Baraza lake la Mapinduzi walikiuka mara nyingi mapendekezo ya kisera kutoka Bara kiasi kwamba Mwl. Nyerere hakuwa na kauli tena juu ya sera za kiserikali. Aidha, Karume akakataa mazungumzo zaidi ya kikatiba kwa hofu ya Zanzibar kupoteza hadhi na mamlaka yake. Karibu kila alichopendekeza Mwl. Nyerere, alipata jibu la mkato kutoka kwa Karume: “Kama hivyo ndivyo (basi), tuvunje Muungano.”



Mitazamo hasi ya viongozi hawa wawili juu ya Muungano, ndio iliyosababisha mchakato wa kupata Katiba ya Muungano ndani ya mwaka mmoja kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, usifanyike, na Muungano kuongozwa kwa Katiba ya Muda kwa miaka kumi na mitatu (13) hadi mwaka 1977 na baada ya Karume kufariki. Mwl. Nyerere alipowasilisha na kupitishwa kwenye Bunge la Muungano, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano, na kutangaza nia yake ya kuona unatumika Visiwani, Karume aliupinga. Akaja na mpango wake tofauti wa Miaka Mitatu kwa Zanzibar, ulioandaliwa na mchumi kutoka Ujerumani Mashariki. Kwa yote hayo na mengine, Mwl. Nyerere alianza kuonesha dhahiri chuki yake kwa utawala wa kimabavu wa Karume. Naye (Karume) alipotambua hilo, alizuia mwingiliano huru wa watu kati ya Visiwani na Tanzania Bara kwa hofu na kwa sababu zisizofahamika.



Si mara moja, hofu na wasiwasi wa kimaasi vilipojionesha Zanzibar, mamlaka za usalama zilimshauri Mwal. Nyerere kufuta ziara zake Visiwani. Hofu hizi zilijidhihirisha zaidi pale Othman Sharrif, baada ya uteuzi wake wa Ubalozi Marekani kufutwa kwa shinikizo la Karume na kurejea Zanzibar, alipokamatwa na kutiwa kizuizini kama si nguvuni bila kosa bainifu. Kuonesha jinsi alivyochukizwa na kitendo hicho, Mwl. Nyerere aliingilia kati na kumwita Karume Ikulu. Hata hivyo, kwa kiburi cha beberu, Karume alimkatalia katu, kuonesha kwamba Mwl. Nyerere hakuwa na mamlaka kwake. Sharriff aliachiwa baadaye kwa hiari ya Karume; na Mwl. Nyerere akamteua kuwa Afisa Mifugo Tanzania Bara. Hata hivyo, Oktoba, mwaka 1969, wakati Mwl. Nyerere akiwa ziarani nchi za nje, Sharrif alikamatwa Tanzania Bara na kurejeshwa Zanzibar alikouawa.
 
Back
Top Bottom