Ngeleja: Zitto aliomba na kupewa milioni 30 kutoka kwa Rugemarila

Void ab initio

JF-Expert Member
Mar 1, 2015
5,703
5,635
Mh.Ngeleja wakati akihojiwa na baraza la maadili amesema Mh. Zitto Kabwe alipokea shilingi milioni 30.Amesema kama wanahojiwa waliopokea fedha na Mh. Zitto aitwe kuhojiwa.
====================

Dar es Salaam. Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja jana alimtaja Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na baadhi ya matajiri wanaowafadhili wabunge nchini, kama sehemu ya utetezi wake mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.

Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini alikuwa anajitetea mbele ya baraza hilo kuhusiana mgawo wa Sh40.4 milioni, aliopata kutoka kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engeneering & Marketing Limited, James Rugemalira.

Pamoja na kudai kuwa mgawo huo haukuwa na mgongano wa masilahi, Ngeleja aliibua tuhuma mpya akihoji ni kwa nini Zitto hakuhojiwa na baraza kwa kutuhumiwa kupokea fedha kutoka katika Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP), ambayo pia inahusishwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa ndani ya Benki Kuu ( BoT) wala tuhuma za kufadhiliwa na Mfuko la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mashtaka dhidi ya Ngeleja

Akimsomea mashtaka, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mwanaarabu Talle alidai kuwa Ngeleja akiwa kiongozi wa umma alipokea fedha hizo kwenye akaunti yake namba 0011010265260 katika Benki ya Mkombozi na hivyo kusababisha mgongano wa kimaslahi.

Wakili Talle alidai kuwa kwa kupokea fedha hizo kutoka kwa kampuni hiyo, Ngeleja alikiuka kifungu cha 6(e) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kinachozuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa masilahi.

Pia wakili Talle alidai kuwa Ngeleja alijipatia manufaa ya kifedha kinyume cha kifungu cha 12 (1) (e) cha sheria hiyo.

Ushahidi wa sekretarieti

Baada ya kumsomea mashtaka hayo, Ngeleja alikana na shahidi wa Sekretarieti, Waziri Yahya akiongozwa na Wakili Talle alidai kuwa baada ya kuchunguza walibaini kuwa Ngeleja alipewa Sh40,425,000 kutoka VIP Engeneering & Marketing Februari 12, 2014.

Alidai kitendo cha Ngeleja cha kupokea pesa hizo kumekiuka sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo hairuhusu kuomba, kupata au kupokea fedha.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, walibaini kuwa mwaka 2007 Ngeleja alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na kwamba kuanzia 2008 hadi 2012 alikuwa Waziri wa Nishati na Madini ambapo aliendelea na majukumu ya kusimamia utekelezaji wa mkataba kati ya Tanesco na IPTL ambayo VIP ilikuwa na hisa.

Alidai kitendo cha Ngeleja baadaye kupokea fedha kutoka kwa kampuni hiyo ni kujiingiza katika mgongano wa masilahi na kwamba ni muhimu viongozi wa Serikali wakasimamia misingi ya maadili ya viongozi, vinginevyo itasababisha wananchi wasiwe na imani na Serikali.

Akijibu moja ya maswali kutoka kwa Ngeleja, shahidi huyo alidai kuwa ni si vibaya wabunge kuomba misaada lakini akasema kuwa ni vema iwe katika misingi ya sheria.

Pia alidai kuwa kwa uchunguzi wao msaada kutoka VIP ulikuwa ukichagua baadhi ya viongozi na si wabunge wote waliopewa.

Utetezi wa Ngeleja

Baada ya kusikiliza ushahidi huo, Ngeleja ambaye hakuwa na mwanasheria, alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, akisema zilikuwa ni msaada wa kawaida kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ndani na nje ya jimbo lake.

Alidai kuwa msaada huo hautofautiani na misaada ambayo wabunge wengine wamekuwa wakipewa na marafiki na wafadhili mbalimbali na kwamba jambo hilo si geni na ndiyo maana hata Bunge halijawahi kuona ni tatizo.

Ngeleja aliwataja baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitoa misaada ya fedha kwa wabunge kuwa ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, mwanzilishi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bakhresa Group, Said Salim Bakhresa.

Aliwataja wafanyabiashara wengine ambao wamekuwa wakiwapa misaada wabunge kuwa ni mwenyekiti wa Quality Group, Yusufu Manji na mfanyabiashara Subhash Patel.

Mbali na matajiri hao pia Ngeleja alidai kuwa wabunge pia wamekuwa wakinufaika na ufadhili kama huo kutoka kwa taasisi za umma na kampuni binafsi.

Alizitaja kuwa ni pamoja na mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi za kifedha kama vile NSSF, PPF, LAPF PSPF, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), benki za CRDB, NMB na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).

Ngeleja alizitaja kampuni binafsi ambazo zimekuwa zikiwafadhili wabunge kama vile VIP Engeneering & Marketing, Songas na IPTL, huku akidai kuwa hizo kwa uchache tu kati ya orodha ndefu aliyo nayo.

Tuhuma kwa Zitto

Katika namna ya kujinasua katika tuhuma hizo, Ngeleja alirejea tuhuma dhidi ya Zitto zilizowahi kutolewa bungeni kwa nyakati tofauti za kujipatia msaada kutoka katika taasisi za umma na kampuni binafsi.
Alinukuu taarifa ya Kambi ya Upinzani bungeni wakati wa Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mwaka jana kuhusu uhalali wa Zitto kupata msaada wa jumla ya Sh119 milioni kutoka NSSF na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Alidai kuwa licha ya tuhuma hizo kuwasilishwa bungeni, mbunge huyo ni mwenyekiti wa PAC, na Bunge halikumwajibisha.

Tuhuma nyingine dhidi ya Zitto ambazo Ngeleja alizirejea ni zile zilizotolewa bungeni na Mbunge wa Mtela, Livingstone Lusinde kuwa alipewa zaidi ya Sh30 milioni kutoka kwa kampuni ya PAP, inayohusishwa na escrow kwa nyakati tofauti.

Huku akibainisha tarehe tofauti tofauti na kiasi alichokuwa akipokea Zitto kutoka PAP, Ngeleja alidai kuwa licha ya tuhuma hizo kuwasilishwa mezani kwa Spika, Bunge halikuchukua hatua.

Ngeleja alidai kuwa licha ya Zitto kusema kuwa yuko tayari tuhuma hizo zipelekwe kwenye Kamati ya Bunge ya Maadili, zichunguzwe bado Bunge halikuchukua hatua.

Akizungumzia tuhuma hizo, Zitto alisema alishajibu hilo bungeni na kuitaka tume ifanye uchunguzi wake na ikigundulika amehusika kwenye lolote basi ahojiwe.

"Mheshimiwa Ngeleja yeye alipaswa kujibu hoja zake na kama anadhani kuna tuhuma azipeleke tume. Mimi naunga mkono kwa asilimia 100 kazi inayofanywa na tume na kazi hiyo walipaswa wafanye siku nyingi," alisema Zitto na kuongeza:

"Analosema Ngeleja ni la juu juu tu, hivyo sekretarieti ifanye uchunguzi na kujiridhisha halafu ihoji."

Ngeleja alikanusha


Hata hivyo, Ngeleja ambaye alianza kuhojiwa saa 4.00 asubuhi hadi saa 7.30, mchana alisema hakuomba wala kupokea fedha kutoka katika Kampuni ya VIP Engineering & Marketing Ltd ya James Rugemalira kama ilivyodaiwa kwenye mashtaka dhidi yake bali alimwomba Rugemalira fedha hizo kama mtu binafsi ambaye alimpa Sh40 milioni kupitia akaunti ya VIP TZS Trust.

Vilevile alisema fedha hizo alizipokea kupitia akaunti namba 00110102652601 iliyopo katika Benki ya Mkombozi tofauti na akaunti namba 00110102652660 inayosomeka kwenye hati ya mashtaka.

"Hakukuwa na mgongano wa kimaslahi kwa sababu msaada huo niliupata baada ya wadhifa wangu wa uwaziri kuwa umekoma, hivyo nisingeweza kufanya ushawishi wowote," alisema Ngeleja.

Akifafanua, alisema baada ya kupewa fedha hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilimwandikia barua ikitaka asilimia 30 ya kodi ya kiasi hicho na alilipa Sh13 milioni na kubakiwa na Sh27 milioni.

"Kwa hiyo naomba ieleweke kwamba kiasi nilichobakiwa nacho ni Sh27 milioni, ambazo nimezitumia kwa ajili wa wananchi wa jimbo langu la Sengerema na Watanzania wengine," alisema Ngeleja.

Mahojiano

Mwanasheria: Huoni kwamba kuomba ni aibu?

Ngeleja: Hata Serikali inaomba, haya ni maisha ya kisiasa, tunaomba ili kusaidia wananchi hasa katika maeneo ambayo hakuna Bajeti ya Serikali.

Mwanasheria: Rugemalira alikueleza fedha hizo ni za nini?

Ngeleja: Nilimwomba fedha hizo ili zinisaidie kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wananchi wa Jimbo la Sengerema na nje ya jimbo.

Mwanasheria: Ulipeleka fedha hizo kwenye Kamati ya Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kupanga matumizi ya fedha ulizoomba?

Ngeleja: Hapana, kwa sababu Mfuko wa Jimbo ni fedha ambazo zinatokana na bajeti ya Serikali. Hivyo siwezi kuchanganya fedha hizo kwa sababu kama mbunge nimekuwa nikisaidia shughuli mbalimbali za kijamii kama vile ujenzi wa misikiti na makanisa na fedha za mfuko wa jimbo haziwezi kusaidia katika maeneo hayo.

Mujunangoma aweka pingamizi

Wakati huohuo. Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma ameweka pingamizi katika baraza hilo akisema ana kesi katika Mahakama ya Kisutu inayohusu mgawo wa Akaunti ya Tegeta Escrow.

Mashtaka ya Mujunangoma kwa mujibu wa Talle, ni kwamba mtuhumiwa huyo alitoa ushauri wa kisheria kwa Kampuni ya VIP Mabibo Wines and Spirit uliompatia Sh423.4 milioni kinyume na kifungu cha 12 cha Sheria za Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mujunangoma akiwakilishwa na wakili Jamhuri Johnson, alisema mbali na kesi iliyoko katika Mahakama ya Kisutu pia kuna pingamizi ya Mahakama Kuu linazozitaka taasisi mbalimbali zisijadili suala la Akaunti ya Tegeta Escrow.

Wiki iliyopita Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge alipinga kuhojiwa na baraza hilo akisema Mahakama Kuu ilizuia suala hilo kujadiliwa na taasisi yoyote.

Hata pale mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu wa Hamis Msumi aliposema baraza lina mamlaka ya kulijadili suala hilo, Chenge atakata rufaa Mahakama Kuu.

Akitetea hoja hiyo, Wakili Johnson alisema mteja wake ana kesi namba 11 katika Mahakama ya Kisutu inayohusu masuala hayo ya mgawo wa Akaunti ya Tegeta Escrow.

Alisema mteja wake anapokuwa na kesi ya aina moja katika sehemu mbili tofauti hatapata nafasi ya kujitetea vizuri.

Jaji Msumi baraza hilo litatoa uamuzi wake leo ili kuangalia kama shauri hiyo liendelee au lisimame kusibiri kesi iliyoko katika Mahakama ya Kisutu.

Chanzo:Mwananchi
 
Akijitetea katika Baraza la Maadili la Viongozi wa Umma, mh.Ngeleja amesema si yeye peke yake aliomba msaada wa fedha kutoka kampuni ya VIP, bali alitaja pia baadhi ya watumishi wengine wa umma na mmoja wao ni mwenyekiti wa PAC,mh.Zitto Kabwe ambaye Ngeleja amedai kuwa Zitto alipewa milioni 30 na bwana Rugemarila.

Hata hivyo,ITV hawakuripoti majina ya watumishi wengine waliomba fedha kutoka kampuni ya VIP.

CHANZO:ITV
 
Nimemsikia Ngeleja amesema asihukumiwe yeye kwanza mpaka wabunge wengine waliokula mlugula nao watajwe. Akaamua kumtaja Zitto Kabwe kwamba alikula milioni 30. Ni hatari sana
 
Ngelejaaa Njoo na ushahidi ili tumhukumu Zitto kihalai umesema amepokea zaidi ya milioni 30 za PAP/IPTL Ila nadhani umeleta kwa maneno matupu ila pia umesema pesa uliomba kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo lakini mwanasheria wa tume kasema baadhi ya pesa ulipeleka kwenye kanisa flani lililopo jijini Dar es Salaam wakati huko sio Jimboni kwako
 
Mh.Ngeleja wakati akihojiwa na baraza la maadili amesema Mh. Zitto Kabwe alipokea shilingi milioni 30.Amesema kama wanahojiwa waliopokea fedha na Mh. Zitto aitwe kuhojiwa.

Chanzo;ITV Habari.

nimemsikia na mimi au ndio sababu ya kuipeleka issue kishkaji
 
Back
Top Bottom