Neno La Leo: Essau, Yakobo Na Bakuli La Dengu! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Neno La Leo: Essau, Yakobo Na Bakuli La Dengu!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, May 22, 2011.

  1. m

    maggid Verified User

    #1
    May 22, 2011
    Joined: Dec 3, 2006
    Messages: 1,084
    Likes Received: 397
    Trophy Points: 180
    Ndugu zangu,


    WAKRISTO na hata wengine wasio Wakristo wanakitambua kisa cha Essau na Yakobo. Na tafsiri zaweza kuwa nyingi; hii ni ya kwangu. Tunasoma, kuwa Essau na Yakobo walikuwa ni wana wa Isaka.

    Essau alikuwa ni mkubwa akifuatiwa na Yakobo. Essau Yule alikuwa ni mwindaji. Naye Yakobo alikuwa akipenda sana kushiriki shughuli za mapishi jikoni akiwa na mama yake.


    Biblia inasema, kuwa siku moja Essau alikwenda katika mawindo yake. Alirudi mikono mitupu, hakupata kitoweo. Aliporudi nyumbali Essau alikuwa ni mwenye njaa kali, kwani, aliwinda siku nzima mwituni pasipo kula.


    Nyumbani alimkuta Yakobo akiwa amepika dengu. Essau alimuomba Jakobo ampatie bakuli la dengu ili ale na kutuliza njaa yake.

    Yakobo alimwambia kaka yake Essau; ” Kama unataka bakuli la dengu, basi, ukubali kuwa mdogo kwangu.” Yaani, Essau akubali kuwa, kuanzia siku hiyo, yeye Yakobo ahesabike kuwa mkubwa (mzaliwa wa kwanza) wa Isaka baba yao, na Essau awe ni mzaliwa wa pili.


    Kwa vile Essau alikuwa na njaa sana, alikubali kuwa mdogo kwa Yakobo. Ndipo akapewa bakuli la dengu amalize njaa yake. Naam, tunaona, kuwa njaa ilimfanya Essau auze haki yake ya uzaliwa wa kwanza.


    Na ya akina Essau na Yakobo tunayaona sasa. Kuna hata wanaouza haki za Wananchi kwa sababu ya njaa zao. Na wengine si kwamba wana njaa kali hivyo. Ni wenye njaa ya kutaka shibe kama ya mbwa mwitu. Ni watu wenye kuendekeza tamaa.


    Na akina Yakobo wa sasa wenye bakuli la dengu baadhi yao ndio hao wanaoitwa wafanyabiashara. Masharti yao ya kutoa bakuli la dengu ni pamoja na kusamehewa kodi au kupewa upendeleo katika kupata tenda mbali mbali. Wamefikia hata kutoa masharti ya kutuchagulia viongozi wetu.


    Na nguvu hizo tumewapa wenyewe kwa baadhi yetu kuendekeza njaa na kutaka shibe za mbwa mwitu. Na wenye bakuli la dengu wa siku hizi, hawakupi bakuli la dengu likajaa. Kwamba ule ukashiba. La, watakupa dengu kiduchu ili urudi tena kuomba bakuli lingine. Uwe tegemezi kwao.


    Ndugu zangu,


    Kuna wengi mlio kwenye jiko lenye giza huku mkiwa na njaa kali. Mnachohitaji kwanza ni ukombozi wa kifikra . Ukombozi huo utawapelekea kwenye kuepuka kufa na njaa. Kuepuka kuwa watumwa kwenye nchi yenu mliyozaliwa. Kwenye ardhi ya mababu zenu. Anzeni sasa kuuwasha moto. Moto huo utawapa pia mwanga kwenye jiko hilo lenye giza nene.


    E nendeni mkayatafute majani makavu. Kisha muyaweke katikati ya mafiga. Tieni moto kiberiti muyawashe. Yakishawaka, anzeni taratibu kuweka vijiti na vibanzi vikavu juu yake. Na vitakaposhika moto, endeleeni kuweka kuni kubwa huku mkipulizia.


    Moto utakaowaka hapo hautazimika kirahisi. Utawapa shibe ya boga au muhogo. Utawapa mwanga pia. Ni mwanga wa ukombozi wa kifikra na kiuchumi. Na hilo ni Neno La Leo.


    Maggid
    Iringa, Jumapili, Mei 22, 2011
    MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
    0788 111 768
     
  2. itnojec

    itnojec JF-Expert Member

    #2
    May 22, 2011
    Joined: Mar 31, 2011
    Messages: 2,191
    Likes Received: 223
    Trophy Points: 160
    ohh yes.
     
Loading...