singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
- Kama taifa, mwaka jana tuliumaliza na ugomvi mkubwa, mwaka huu tunaumaliza na matumaini makubwa.
Ndugu zangu,
" Kamwe Tanzania Haitakuwa ' Congo Nyingine'. Hayo yalipata kusemwa na Mwalimu Julius Nyerere miaka ya mwanzoni mwa Uhuru. Unaweza kuyasoma kwenye kitabu kilichoandikwa na Sir Andy Chande, A Knight In Africa, Ukurasa wa 77.
Alichokiona Mwalimu miaka ile ya 60 ndicho ambacho, baadhi yetu, kwa kutanguliza maslahi yao binafsi, na hata kwa kusingizia kuwa wao ni Wazalendo zaidi kuliko wengine, hawataki kukiona.
Congo ya MwanaMapinduzi Patrice Lumumba imeangamia kutokana na laana ya rasilimali zake.
Patrice Lumumba alikuwa ni mwanamapinduzi wa kweli. Alisimama upande wa umma. Alitaka rasilimali za Congo ziwanufaishe Watu wa Congo. Mabepari hawakuupenda mtazamo huo wa Lumumba ambao ulijielekeza zaidi kwenye itikadi ya Ujamaa.
Mabepari walimtumia kibaraka, Joseph Mobutu kumsaliti nduguye Lumumba. Mobutu akachukua madaraka ya nchi. Lumumba aliuawa kinyama. Mobutu hakuwahi kuwa Rais wa Watu, bali, kibaraka na zaidi Wakala wa Matajiri walio nje ya Congo.
Ndio, Watanzania tuliumaliza mwaka 2014 na ' Ugomvi Mkubwa'. Kilichoitwa sakata la Escrow kimsingi ulikuwa ni ugomvi wenye kuhusu rasilimali. Ndio maana ya kuhusu zaidi sekta ya Nishati na Madini.
Kuna makosa yalifanyika, wenye kuhusika waliwajibishwa, lakini, pamoja na Rais wa Nchi aliyekuwa madarakani kulishughulikia tatizo na hata kuchukua hatua, kilichoogopesha ni uwepo wa nguvu za kumshinikiza Rais kuchukua hatua nyingine bila hata kuzingatia kuwa Rais kwenye nchi ni kielelezo cha Haki na Utu. Kwamba Rais wa Nchi kwenye kuyafanyia kazi yenye kuwahusu raia wake, hapaswi Kuonea wala Kupendelea. Ndio maana leo tunamwona Profesa Muhongo na Eliakim Maswi wamerudi na kupewa nyadhifa kwenye wizara nyeti.
Watanzania tulipaswa kujiuliza; Je, nguvu za mashinikizo yale zilikuwa ni za ndani tu, au kuna zilizotoka nje? Na kama hilo la pili litakuwa na ukweli, tujiulize, je, wenye kushinikiza hayo ni wenye mapenzi mema na nchi yetu, au ni wenye kujali maslahi yao?
Ndio maana tunaona, hata hii leo, kuwa kwenye hili la makampuni ya nishati ya Umeme, si IPTL tu, kuna wengine; Symbion, Agreko, Songas... . Hawa ni washindani kibiashara. Isije ikawa ni ya ' Ugomvi wa Tembo'. Tunajua kinachoumia ni nini.
Ndugu zangu,
Hii ni Nchi Yetu. Katika yote tuyafanyao, tutangulize kwanza maslahi mapana ya nchi yetu. Maana, mengine tunayoyafanya, na kwa kutanguliza maslahi binafsi, yaweza kuwa mwanzo wa nchi kuparaganyika. Tunayaona kwa wengine.
Na tumuunge mkono Rais aliye madarakani sasa, kwa ayafanyayo kwa maslahi ya nchi yetu.
Na kama Mwalimu alivyosema, nasi tuseme; " Tanzania Should Never Be ' Another Congo'.
Happy New Year!
Ni Neno Fupi La Kufungia Mwaka.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
mjengwa blog