NEMC: Kuna ongezeko la kelele kwenye Baa nyingi

Hivi punde

JF-Expert Member
Apr 1, 2017
2,554
8,552
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema kumekuwa na ongezeko la malalamiko ambapo mwaka 2020 yalikuwa 1,197, lakini katika kipindi cha Julai hadi Septemba, wamepokea malalamiko 170.

Imebainishwa kuwa kati ya hayo, 130 ni ya kelele na mitetemo, huku baa na kumbi za starehe yakiwa malalamiko 60.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Meneja wa NEMC Kanda ya Morogoro-Rufiji, Amina Kibola wakati akielezea hali ya uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo, katika warsha iliyowakutanisha NEMC na wamiliki wa kumbi za starehe, bendi, baa na wadau wa muziki.

Soma hapa:Haya ndiyo madhara ya pombe kiafya, kijamii

Alisema malalamiko mengine yalihusu viwanda, matangazo, nyumba za ibada, mashine za tofali na vyombo vya moto.

Awali, akifungua warsha hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Omary Chande aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe, bendi, baa na wadau wa muziki kufuata sheria na kufanya tathmini ya athari ya mazingira kabla ya kufanya uwekezaji.

Alisema wadau hao wana umuhimu mkubwa katika jamii na Serikali kutokana na kodi wanazotoa, lakini ni lazima zifuate sheria na taratibu zilizowekwa.

“Kumbi za burudani tunazihitaji sana kutokana na umuhimu wake, mtu anaweza akapata stress akaenda kupata burudani zikaisha, pia zinatuchangia kodi...lakini zifuate misingi na kanuni za sheria,” alisema Chande.

Alibainisha hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la kelele na mitetemo katika maeneo mbalimbali zinazotokana na shughuli za kijamii na za kiuchumi.

Soma hapa: Pombe kali tishio jipya kwa vijana

Alitolea mfano kuwa NEMC Kanda ya Kaskazini wamefanya utafiti wa kelele na mitetemo katika Mkoa wa Arusha ambazo zimeonesha kuwa ni changamoto katika jamii na watu wameeleza athari wanazozipata.

Alisema katika utafiti huo, maeneo yaliyoongoza kwa kelele chafuzi ni ya starehe kwa asilimia 33 na viwanda asilimia 24.

“Katika kipindi cha Mei 2020 hadi Septemba 2021 jumla ya malalamiko zaidi ya 85 yameripotiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwa upande wa Arusha ni malalamiko 65 yamepokelewa,” alibainisha.

Aliongeza kuwa serikali imeanza kuchukua jitihada mbalimbali, ikiwemo kuandaa mwongozo wa udhibiti wa uchafuzi mazingira utokanao na kelele na mitetemo.

Akitoa mapendekezo katika warsha hiyo, Robert Sabini ambaye ni mmiliki wa baa na kumbi za starehe ziitwazo Mwendokasi, aliiomba Serikali kupunguza gharama ya Tathmini ya Athari za Mazingira (TAM) ambazo si chini ya Sh3 milioni anazopewa mtaalamu mwelekezi.

Alisema gharama za kufanya TAM ni chanzo cha watu wengi kuvunja sheria.

Alibainisha kuwa ili ufanyiwe tathmini gharama yake sio chini ya Sh3 milioni ambayo anapewa mtaalamu muelekezi.

“Kitu kingine ni kuhakikisha wanaweka mazingira bora ya mfumo huu, kwanini kitengo wasikichukue wao wenyewe hao wataalamu elekezi wanaowatumia wana gharama kubwa ziko juu sana.

“Sasa mwingine anafikiri bora apitishe chini chini iende kwahiyo atahonga honga watu wa serikali za mitaa na watendaji kwasababu gharama ziko juu. TAM ni kitu kizuri sana lakini ili kifanyike na watu wafuate njia sahihi ni lazima tuhakikishe gharama zinashushwa,” alisema

Mkurugenzi wa NEMC, Dk Samwel Gwamaka alisema lengo la warsha hiyo ni kutoa elimu kwa watu hao kuhusu athari za kelele pamoja na kuwaomba waboreshe mahusiano kati yao na jamii.

“Pamoja na hayo, NEMC tunaendelea na ukaguzi wa maeneo ya biashara na kutoa maelekezo mbalimbali ikiwemo amri na kudhibiti kelele, kusimamia uainishaji wa ramani za maeneo yenye kelele zilizopitiliza na kuandaa mkakati wa kudhibiti, pia kuanisha na kutangaza maeneo ya ukimya,” alisema Dk Gwamaka.

Sent from my Infinix X680 using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom