NEEC, TSN kushirikiana kuelimisha umma uwezeshaji

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,599
9,529
yonazi-neec_210_120.jpg


BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limesaini mkataba wa ushirikiano na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa ajili ya kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa mapana zaidi.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji NEEC, Beng’i Issa alisema kampuni hiyo itakuwa mshirika wao na mchapishaji rasmi wa shughuli zote wanazozifanya katika masuala ya uwezeshaji.

“Mwaka huu katika Kongamano la Pili la Uwezeshaji, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi linashirikiana rasmi na Kampuni ya TSN ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo, SpotiLeo na Sunday News kama mshirika rasmi katika uchapishaji wa habari za kongamano hili,” alieleza Issa.

Alisema baraza linaamini katika mtandao mpana, uzoefu na uimara wa taasisi hiyo kupitia mitandao yake ya habari, litawafikia Watanzania wengi zaidi ndani na nje ya nchi katika kuhamasisha kuhusu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Aidha, alisema Juni 10, mwaka huu watafanya Kongamano la Pili la NEEC mjini Dodoma, ambalo litakutanisha wadau wa sekta ya umma na binafsi nchini, kujadiliana kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia atakuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

Pia alisema katika kongamano hilo watapokea ripoti ya utekelezaji wa utaratibu wa masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ngazi ya Taifa sanjali na kutambua wizara, idara, taasisi, serikali za mikoa na wilaya nchini zinazofanya vizuri katika kuratibu masuala ya uwezeshaji katika maeneo yao.

Alisema kongamani hilo litachochea kasi ya utekelezaji wa mikakati ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kujifunza kutoka kwa wadau mbalimbali namna bora zaidi ya kusukuma mbele gurudumu la uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini.

Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi aliishukuru NEEC kwa kuona fursa ambayo ipo kwa kutumia Kampuni ya Magazeti ya Serikali na kuwahakikishia kuwa wamepata chombo muafaka ambacho kitapeleka taarifa za uwezeshaji kwa mapana kwa ajili ya kuwezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla.

“Kwa wadau wengine niwaambie kwamba mfumo huu tuliouanzishwa unaweza kufanywa na taasisi mbalimbali na zinaweza kuja kujiunga na magazeti ya serikali ili kuhakikisha kwamba shughuli zao zinawafikia wananchi pale walipo…

TSN imejipanga kuhakikisha kwamba shughuli kama hizi zinafanikiwa,” alisema Dk Yonazi. Alisema kwa sasa dunia imekuwa ni kijiji taarifa zinafika kila mahali, changamoto ambayo iliyopo ni namna ya kufikisha taarifa hizo kwa wadau ambao wanahusika, hivyo TSN imelitambua hilo na kuona kwamba hiyo ni fursa nzuri ya kupeleka taarifa kwa wananchi kwa kadri inavyowezekana na kwa muda unaotakiwa.

“Ushirikiano huu ambao tumeanzisha utafanikisha kupeleka uwezeshaji kwa watu ambao wanahitaji kujua taarifa za kifedha, taarifa za kiuwezo na kiutendaji na namna ya kubuni biashara na namna wanavyoweza kushiriki katika uchumi wao kwa mahali walipo na uchumi wa dunia nzima,” aliongeza Dk Yonazi.

Alimshukuru Katibu Mtendaji na baraza kwa kuchagua kushirikiana na TSN, na kusema wamefanya maamuzi ambayo ni sahihi na mradi ambao utakuwa wa faida.

SOURCE; HabariLeo
 
Back
Top Bottom