Hearten
Member
- May 17, 2016
- 46
- 54
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Mhe Jaji Mstaafu Damian Lubuva na Mkurugenzi wa uchaguzi Bw.Kailima Ramadhani Kobwey wakikabidhi mfano wa hundi ya shilingi Bilioni 12 kwa Rais John Magufuli.
Fedha hizo zimeokolewa katika fedha zilizopangwa kutumika na Tume ya Uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka 2015.
======================
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi Sh bilioni 12 kwa Rais John Magufuli zilizobaki baada ya Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva alikabidhi hundi ya kiasi hicho cha fedha kwa Rais Magufuli jana Ikulu jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa bakaa ya fedha hizo haikuathiri kwa namna yoyote Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
“Mheshimiwa Rais fedha ambazo tunakukabidhi, tulijibanabana sana, japo muda wenyewe ulikuwa mfupi lakini tulijibanabana sana bila kuathiri utendaji wa shughuli za uchaguzi, isije ikawa inatoa sura kwamba iliathiri, haikuathiri, na katika hali hiyo kama ambavyo wengi ni mashahidi, hatujisifii, lakini uchaguzi ulienda vizuri,” alisema Jaji mstaafu Lubuva, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu jana.
Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo, Rais Magufuli aliipongeza NEC kwa kuokoa fedha hizo na kuzirejesha serikalini ili zipangiwe majukumu mengine na ametaka taasisi nyingine za serikali ziige mfano huo wa uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa.
“Kitendo hiki ambacho mmekionesha leo, kinaonesha ni kwa namna gani Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya uongozi wako Mheshimiwa Mwenyekiti ilivyo na watu makini na waadilifu sana, kwa sababu hizi fedha ambazo kwa lugha uliyotumia ni bakaa, kutokana na zile ambazo mlipewa zaidi ya shilingi bilioni 270, mkatumia shilingi bilioni 261.6, mkabakiza shilingi bilioni 12…
“Mngeweza kuamua kusema hamkubakiza na hakuna mtu yeyote ambaye angewauliza, na saa nyingine pengine hakuna mtu yeyote ambaye angejua, mngeweza pia kusema kiasi mlichotupa hakijatosha, tunaomba mtuongezee ama mngetengeneze maneno mazuri mazuri ya matumizi, bado nina uhakika serikalini wasingejua,” alisema rais.
Pamoja na kukabidhi hundi ya bakaa ya Sh bilioni 12, Jaji Lubuva alimuomba rais aisaidie tume hiyo kupata jengo lake la ofisi kwa kuwa hivi sasa tume inatumia majengo ya kupanga yanayoigharimu takribani Sh bilioni 1.4 kila mwaka kwa kulipia kodi ya pango, usafiri na gharama nyingine za uendeshaji.
Rais Magufuli amelikubali ombi hilo na kuamua kuwa fedha ambazo NEC (Sh bilioni 12) kutoka kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka jana zitumike kujenga ofisi ya tume, na amependekeza ofisi hiyo ijengwe mkoani Dodoma.
“Na mimi ningefurahi zaidi kama hilo jengo lingejengwa Dodoma, kwa sababu Dodoma ndio makao makuu ya nchi hii, na hasa kwa sababu Dodoma ni katikati ya Tanzania,” alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amelikubali pendekezo la tume hiyo la kuanzishwa kwa mfuko wa tume ya uchaguzi ambao utakuwa unakusanya fedha kila mwaka kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaofuata, badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo zitengwe fedha zote za kugharamia uchaguzi huo.