NEC itupe uchaguzi huru Arumeru

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
Edtume.jpg

Maoni ya Katuni


Juzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilikutana na vyama vya siasa kujadili pamoja na mambo mengine maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki pamoja na kujaza nafasi za madiwani katika kata kadhaa zilizo wazi kutokana na sababu mbalimbali.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa na walitoa maoni mbalimbali juu ya uendeshaji wa uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na haja ya kufanyiwa marekebisho daftari la kudumu la wapigakura, utaratibu mzima wa utoaji wa elimu ya uraia na vyama kuridhia maadili ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

Kwa ujumla ulikuwa ni mkutano wa kupeana taarifa kabla kipenga cha kampeni kupulizwa mwezi ujao kisha uchaguzi kufanyika Aprili mosi mwaka huu.

Huu utakuwa ni uchaguzi mdogo wa pili wa kiti cha ubunge tangu kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambao ulishuhudia joto la kisiasa na mwamko mkubwa wa wananchi ukiwa juu katika kufuatilia mambo ya kisiasa na kujua wale wote waliokuwa wanatafuta nafasi za uongozi walikuwa wana ajenda gani katika kipindi cha miaka mitano watakaokuwa madarakani.

Uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge ulifanyika katika jimbo la Igunga, kama ilivyotokea kwa joto la kisiasa kupanda mwaka 2010, pia lilipanda sana, ni hali kama hiyo inatarajiwa kutokea pia katika jimbo la Arumeru Mashariki hasa ikizingatiwa linapakana na jimbo la Arusha Mjini ambalo limekuwa

na siasa za ushindani mkali miongoni mwa vyama viwili, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tunajua kuwa taifa letu linafuata mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi, kwa maana hiyo ni haki ya kila chama cha siasa chenye usajili wa

kudumu kushiriki katika uchaguzi wowote kuanzia wa rais, wabunge au wawakilishi, udiwani hadi wenyeviti wa serikali za mitaa au vijiji. Haki hii ni ya kisheria na hakuna mwenye mamlaka ya kuipokonya.

Nasi tungependa kuvichagiza vyama vya siasa vishiriki uchaguzi huo kwa kusimamisha wagombea wao kwa nia ya kuwapa wananchi fursa ya kuchagua miongoni mwa wagombea mwakilishi wao, nia ni kupata mwakilishi bora ambaye atawaunganisha wananchi na bunge katika kutunga sheria na kuisimamia serikali.

Tunaelewa pia kuwa uchaguzi ni mchakato, huanza na uandikishaji wa wapigakura, kuteua wagombea, kufanya kampeni, kupiga kura, kutangazwa kwa matokeo na mshindi kupatikana. Huu ni utaratibu wa kisheria na ni haki ya kila chama kinachoshiriki uchaguzi husika.

Ni matarajio yetu kwamba huko Arumeru Mashariki, haki hizi hazitapokonywa wala kukanyagwa na mamlaka yoyote au mtu yeyote kwa kisingizio chochote.

Ni kwa utambuzi huo basi kwanza tunavipongeza vyama ambavyo hadi sasa vimekwisha kuonyesha nia ya dhati ya kushiriki uchaguzi huo, tunaamini vitaingia katika uchaguzi huu vikitafuta kura kwa kujenga hoja; hatutarajii hujuma, kampeni chafu, matumizi yasiyofaa ya vyombo vya dola

katika kukwaza uhuru na haki ya wagombea kujinadi kwa wananchi katika mikutano ya hadhara.
Kadhalika, hatutarajii kwamba vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi litatumika vibaya katika mchakato mzima wa uchaguzi huu, kama vile

kuvuruga mikutano ya kampeni ya vyama, au kukubali kwa njia yoyote ile kutumiwa kinyume cha sheria na taratibu za sheria ya uchaguzi.
Tunasema haya tukiwa na kumbukumbu ya hali iliyotokea katika uchaguzi mdogo wa ubunge Igunga mwaka jana, ambako hali ya hewa ilichafuka

kiasi cha kufikia hatua ya kutaka kuvunjika kwa amani, tatizo likiwa ni kujiingiza kwa watendaji wa serikali katika shughuli za uchaguzi wakati hawatambuliwi na sheria ya uchaguzi.

Tunafikiri, uzoefu wa Igunga utatumika kufanya uwanja uwe sawa kwa vyama vyote vya siasa vitakavyosimamisha wagombea, ili wajinadi kwa nguvu na uwezo wao wote, wajenge hoja kadri wanavyoweza na mwishowe wananchi wafikie maamuzi sahihi juu ya nani anastahili kuwawakilisha bungeni.

Kwa kusema haya tunaamini kila chama kitaheshimu chama kingine, kitaacha kuhujumu mikutano ya wengine, mabango na kila aina ya kipeperushi cha kujitangaza cha chama kingine kwa nia ya kuufanya uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki kuwa huru na wa haki.

Hili litawezekana tu kama NEC itakuwa huru bila kuingiliwa na yeyote, polisi nao watafanya kazi kwa weledi na vyama vitaheshimu sheria ya uchaguzi. Tunautakia mchakato wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Arumeru Mashariki kila la heri.

CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom