Ndege mjanja hunaswa na tundu bovu

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
Ndege mjanja hunaswa na tundu bovu

Na Ahmed Rajab

SIJUI kwa nini hasa, ingawa nina hakika sababu ninazo, lakini tangu juzi akili yangu imetekwa na ndege na kasisi. Imekuwa ikivutwa na kuvutiwa na viumbe hivyo.

Nimekuwa nikiufikiria ujanja wa ndege na nikiyakumbuka maneno ya Martin Niemöller, kasisi wa Kijerumani aliyepata umaarufu katika zama za udikteta wa Adolf Hitler na siasa zake za Unazi.

Siasa hizo za kibaguzi zilisababisha mauaji ya halaiki ya Wayahudi pamoja na wengine ambao Hitler na wafuasi wake wakiamini walikuwa na “damu chafu”, yaani hawakuwa na ile waliyoifikiria wao kuwa ni damu safi ya Kijerumani. Wao walikuwa wakijinata kuwa asili yao ni kabila la “Aryan,” ambalo wakiamini kuwa ni kabila la tabaka la juu kabisa duniani.

Miongoni mwa hao wengine walikuwa Wajerumani waliokuwa na damu ya Kiafrika. Idadi yao haijulikani lakini inadhaniwa kuwa hawakupungua elfu kadhaa. Wengi wao walikuwa na wake wa kizungu waliozaa nao. Kwa muda mrefu watoto wao walikuwa wakibaguliwa, wakidharauliwa na kufanywa vinyago kwa sababu walikuwa na ngozi nyeusi.

Mnamo 1941, serikali ya Hitler ilitangaza rasmi kwamba watoto hao hawatoruhusiwa kusoma katika skuli za serikali. Ubaguzi ukiendekezwa hufika kwenye mipaka kama hiyo ya umajununi.

Sera kama hizo za kiwazimu zikimuudhi sana Niemöller.

Kasisi huyo, aliyefariki 1984 akiwa na miaka 92, alikuwa mtu wa ajabu. Kama walivyokuwa makasisi wengi Wakiprotestanti wa Ujerumani, alikuwa muhafidhina na alimuunga mkono Hitler aliposhika madaraka 1933. Akiamini kwa dhati kwamba utawala wa Hitler utaufufua utaifa wa Ujerumani.

Lakini, polepole Niemöller akabadilika. Akaanza kuupinga ubaguzi wa rangi na wa kikabila kwa kuipinga ile iliyokuwa ikijulikana kama “Ibara ya Aryan” iliyowabagua watu wote wasio Waaryan huko Ujerumani. Ibara hiyo ilikuwa lazima iingizwe katika katiba za jumuiya, mashirika au mikataba ya upangishaji wa nyumba.

Ibara hiyo ilitumiwa kwa mara ya kwanza katika sheria kuhusu ajira za serikali iliyopitishwa Aprili 1933. Baadaye hata mtu akifunga ndoa na asiye “Mu-Aryan” kulimfanya anyimwe ajira serikalini.

Waliobaguliwa walikuwa wakinyimwa ajira za kila aina, nyumba za kukodi, uanachama wa jumuiya na wa taasisi na hata wa klabu mbalimbali. Kila ubaguzi ulivyokuwa ukishamiri ndipo Niemöller alipozidi kuupinga.

Mwaka huohuo wa 1933 aliposhika madaraka Hitler, Niemöller alianzisha jumuiya ya makasisi kupinga ubaguzi uliokuwa ukizidi kuongezeka dhidi ya Wakristo wenye asili ya Kiyahudi.

Kuna baadhi ya wasomi wanaosema kwamba ingawa Niemöller alikuwa akiupinga ubaguzi, hata hivyo baadhi ya matamshi yake mwenyewe yalikuwa ya kibaguzi kwani yaliwadharau na kuwabagua Wayahudi. Kufikia 1934, alikuwa miongoni mwa waliojiengua kutoka madhehebu ya Kiprotestanti kwa sababu wakipinga kuingizwa dhana za Kinazi katika mafundisho ya madhehebu hayo.

Badala yake Niemöller akawa mmoja wa waasisi wa madhehebu mapya au tuseme kanisa jipya waliloliita Kanisa la Ungamo. Wakati huohuo, akiendelea kumpinga Hitler na siasa zake za kibaguzi. Alitiwa nguvuni Julai Mosi, 1937 na akafikishwa mbele ya “Mahakama Maalum” akishtakiwa kwa kufanya harakati dhidi ya Dola. Alipigwa faini ya marki 2,000 na akapewa hukumu ya kifungo cha miezi saba gerezani. Kwa vile alishakaa kizuizini kwa kipindi kilichopindukia miezi saba, mahakama ikamwachia huru.

Lakini alipoteremka tu mahakamani, polisi wa siri walimkamata tena na akapelekwa kwenye kambi maalum za wafungwa wa kisiasa. Wafungwa hao wakiteswa kila aina ya mateso katika kambi hizo. Niemöller alifungwa kwenye kambi mbili tofauti kutoka 1938 hadi 1945. Aliyapata mateso kwa sababu alithubutu kusimama na kuupinga udikteta wa Hitler na siasa zake za kibaguzi.

Ninamdhukuru Kasisi Niemöller kwa sababu ya matamshi yake kwenye hotuba moja aliyoitoa mwaka 1946 na iliyogeuzwa baadaye kuwa shairi. Matamshi hayo ni juu ya woga waliokuwa nao wasomi wa Ujerumani baada ya Hitler kushika madaraka nchini humo na kuanza kuyashambulia na kuyanyanyasa makundi mbalimbali, moja baada ya moja.

Kwenye hotuba yake Niemöller alisema: “Kwanza waliwakamata wakomunisti, na nilikaa kimya kwa sababu sikuwa mkomunisti. Halafu waliwakamata watetezi wa wafanyakazi, na nilikaa kimya kwa sababu sikuwa mtetezi wa wafanyakazi. Halafu waliwakamata Wayahudi, na nilikaa kimya kwa sababu sikuwa Myahudi. Halafu walinijia mimi, na hapakubaki mtu wa kunitetea.” [Tafsiri huru ya maneno ya Niemöller.]

Hayo ni matamshi ya majuto. Niemöller akiyaelezea majuto yake na ya wasomi wenzake wa Ujerumani waliokuwa wakigeuza uso wenzao walipokuwa wakinyanyaswa. Ni wale waliokuwa wamefunga macho yao na walioiziba midomo yao wasiwatetee wenzao walipokuwa wakinyanyaswa na udikteta wa Hitler.

Mwishowe wakajikuta nao pia wanawindwa na kuandamwa na polisi wa siri wa Hitler. Wakajikuta wako peke yao kwa sababu hapakuwako tena wa kuwatetea na kuwapigania.

Hivyo ndivyo inavyokuwa pale jamii inapokuwa inatawaliwa na hofu katika mazingira ya kutishwa na watawala. Watu huingiwa woga wasiseme wanayopaswa kusema. Huyaona mateso ya wengine kuwa ni mambo yasiyowahusu. Huyapa mgongo na huyageuzia uso.

Watawala wenye muelekeo wa kidikteta mara nyingi wanapokabiliwa na upinzani mkali huwa na tabia ya kulenga kundi baada ya kundi. Kwa mfano, huenda wakaanza kuwaandama wanasiasa wapinzani au wa mrengo fulani. Halafu huenda wakawalenga waandishi wa habari au wapashaji habari wa mitandaoni au wanasheria au wanafunzi.

Jamii itafanya dhambi kubwa endapo itakaa kimya kila pale kundi baada ya kundi linapokuwa linashambuliwa na utawala wa kimabavu. Inapokuwa haipazi sauti kulaani vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na watawala wa kimabavu jamii huwa katika hatua za mwanzo za kujiangamiza yenyewe.

Tabia nyingine waliyonayo watawala wa kimabavu ni ile ya kudanganya. Huwadanganya wananchi ili wasiwe na tabu ya kuwaburura.

Watawala wa aina hiyo, bila ya kuona haya, huwadanganya wananchi mchana kweupe, siku hadi siku, mpaka mwisho wao wenyewe huuamini uongo wanaouzua. Tena hufanya hivyo kwa kibri wakidhani kwamba wananchi hawana uwezo wa kufikiri. Ndio maana wananchi wanawajibika wajitahidi kufikiri wenyewe, wasikubali kuwaachia watawala wafikiri kwa niaba yao.

Wajibu mwingine walio nao wananchi ni kuelimishana kuhusu haki zao za kikatiba katika mfumo wa kidemokrasia. Wawe na hakika ya haki zao na namna katiba ya nchi inavyowakinga wanapozipigania haki hizo.

Tunapowasikia, kwa mfano, mashekhe wa Uamsho wakieleza jinsi walivyofanyiwa mambo ya kinyama wakiwa jela au tukiwaona wanasiasa wa Chadema au waandishi wa mablogi wakiandamwa na vyombo vya dola, tukasema mambo hayo hayatuhusu na tukakaa kimya, tukumbuke kuwa iko siku huenda zamu ikawa yetu. Na zamu itapokuwa yetu huenda pasiwepo na wa kututetea.

Itakuwa ni kosa letu sote endapo tutazinyamazisha sauti zetu zisilalamike pale utawala unapozidi kuendeshwa kimabavu. Dhima ni ya jamii nzima, kwa jumla, kuhakikisha kwamba tuko macho saa zote kuzilinda haki za wananchi.

Hiyo si kazi rahisi kwa sababu watawala huwa wepesi wa kuvitumia vile waviitavyo vyombo vya dola ili kuwanyamazisha wananchi na kuyazima madai yao.

Nakubali kwamba uamuzi wa kupambana na nguvu za dola kwa kufanya maandamano, au hata kwa kutumia maneno, ni uamuzi mgumu. Panaweza pakazuka madhara kwa kusema kweli.

Madhara hayo yanaweza yakamfika mtu au watu binafsi na hata jamii, kwa jumla. Katika hali kama hiyo ambapo pana uwezekano mkubwa wa dola kuteremsha vifaru vya kijeshi mitaani na panapodhihirika kuwa haitojali endapo damu itamwagika, je, wananchi waendelee tu kusema kweli na kudai haki zao au wayamezee yanayotendeka na wakae kimya? Si rahisi kulijibu swali hili.

Si rahisi kulijibu kwa sababu si ushujaa peke yake unaohitajika katika nyakati kama hizo. Panahitajika pia hekima. Viongozi wa upinzani Zanzibar wamekabiliwa mara kadhaa na hali hiyo ya kutatanisha.

Watawala wamekuwa wakitumia vitisho kuwatia hofu wananchi. Wakati huohuo wamekuwa wakitumia ujanja wa kujaribu kuwalaghai watu wasiolaghaika tena. Viongozi wa upinzani, kwa upande wao, wamejiepusha kuingia kwenye mtego wa kuweza kuwafanya walaumiwe endapo wafuasi wao watamiminika mitaani kupambana na nguvu za dola na kusababisha umwagaji damu.

Labda wamejifunza funzo la kifalsafa kutoka kwa wenye kutega ndege kwa urimbo na masusu mabovu. Pengine funzo lenyewe limewafanya waweze kufikiri wenyewe badala ya kuwaachia wengine wafikiri kwa niaba yao. Katika mazingira ya sasa ya Zanzibar kufikiri namna hivyo kunahitaji ushujaa.

Mwenye ushujaa anakuwa na uwezo wa kupata maarifa mepya. Daima maarifa yanakomboa. Ni nyenzo moja ya kuleta ukombozi. Labda maarifa waliyoyapata viongozi wa upinzani ni maarifa ya watega ndege, ya kutambua kwamba ndege mjanja hunaswa na tundu bovu.

Makala hii ilichapwa kwa mara ya kwenye gazeti la Raia Mwema toleo la Februari 2, 2017.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Screenshot_20230516-113915_Chrome.jpg
 
Back
Top Bottom