Ole Sendeka alieleza kitu kizuri kwamba tatizo bunge letu halina kamati ya kudumu ya kufuatilia maazimio yake, lakini alikuwa amechelewa na hakuna aliyemsikiliza. Hali itaendelea kuwa kama ilivyo ya kusema "Rais hashinikizwi" au "tatizo ni mfumo". Maana halisi ya bunge kuisimamia serikali ni ipi?
Mtakumbuka tangu mwanzo wanaCCM wengi hawakutaka kabisa suala la kuwawajibisha hao jamaa, kwa hiyo kwa namna yoyote wataendelea kutetea msimamo wao wa tangu mwanzo.
Nawasifu wabunge wa upinzani kipindi hiki hata walipoona adhabu inapangwa na mmoja wa watuhumiwa hawakutoka nje ya bunge kama ambavyo wamekuwa wakifanya kipindi cha nyuma walipokuwa wakichakachuliwa, walisimama wakaanza kuimba nyimbo za kutiana hamasa bila kutoka hadi mama makinda alipoahirisha bunge na likaendelea kesho yake. Wangetoka ingekuwa nafasi nzuri kwa upande wa pili kujipangia mambo yao kwa masilahi yao wenyewe. Naona hii mbinu ya kukatalia mle ndani na kupoteza utulivu ni nzuri zaidi ya kushinikiza mambo yenye masilahi kwa taifa.
Nashauri, kama maazimio ya bunge hayatatekelezwa, katika vikao vijavyo vya Bunge waingie bungeni kama kawaida lakini wasikubali kumsikiliza waziri yeyote (wapoteze utulivu) hadi siku maazimio ya bunge yatakapotekelezwa. Hiyo ndiyo njia pekee ya kuishinikiza serikali kutekeleza maazimio ya bunge.
Ikumbukwe kwamba wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hivyo maamuzi ya Bunge ni maamuzi ya wananchi milioni 45.