Nape na Tendwa wanena kuhusu Kafulila

tendwa1(39).jpg

Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa


Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amesikitishwa na uamuzi wa Chama cha NCCR-Mageuzi kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini,

David Kafulila, na kuvitaka vyama vya siasa kutokutumia ubabe na kukomoana wakati wa kutoa maamuzi.


Alisema NCCR-Mageuzi ingechukua uamuzi mwingine na sio kumvua mbunge huyo uanachama kwani kufanya hivyo kunakidhalilisha chama na kukifanya kishuke.


Tendwa alisema katika mahojiano na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufungua mafunzo ya viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa kuhusu uongozi/uwajibikaji na utawala bora, jijini Dar es Salaam jana.


Alisema vyama vya siasa nchini vinapaswa kutumia vikao vyake kusuluhisha migogoro na malumbano yanayowakabili ndani ya chama badala ya kutumia fursa hizo kufukuzana.


Alisema uamuzi uliochukuliwa na chama hizo dhidi ya Kafulila utaigharimu kiasi kikubwa serikali katika kuitisha uchaguzi mdogo kuziba nafasi itakayoachwa wazi na mwanasiasa huyo kijana.

Alisema gharama za kuendesha uchaguzi mdogo ni zaidi ya Sh. bilioni 10.


Pia alisema uamuzi huo wa NCCR-Mageuzi umepoteza uaminifu kwa wananchi na kukidhalilisha chama hicho, kwani uamuzi huo utamfanya Kafulila kupoteza ubunge wake.

Aliwataka viongozi na wanachama wa vyama vya siasa nchini kuwa na maadili mema na kusema kiongozi bora ni yule

anayefahamu mahitaji ya watu anaowaongoza na hivyo kutambua malengo ya chama anachokiongoza.

Pia alivitaka vyama vya siasa nchini kujenga uhusiano mzuri na Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), kwani navyo pia vinawajibika katika ulinzi wa taifa.


Wakati huo huo, Katibu Halmashauri Kuu (NEC) Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, pia alisikitishwa na uamuzi huo wa NCCR-Mageuzi dhidi ya Kafulila na kusema si kitendo cha kiungwana

Alisema kitendo cha kumfukuza mwanasiasa kijana katika chama ni kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.


Nape alisema kilichopaswa kufanywa na NCCR-Mageuzi, ni kumuonya na kumfundisha Kafulila na si kumvua uanachama.


Alitolea mfano wa enzi za utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, kuwa mtu alipokuwa akikosea ndani ya chama, alionywa na kufundishwa.

“Tupo tayari kumpokea mtu yoyote ndani ya chama atakayekuwa tayari kujiunga nasi. Milango iko wazi,” alisema Nape na kuwashukuru NCCR-Mageuzi kwa kile alichokisema kuwarudishia jimbo lao la Kigoma Kusini.



CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom