na Asha Bani na Francis Dande
SIKU moja baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR–Mageuzi), kuvuliwa uanachama, hivyo kupoteza ubunge wake, ameibuka na kudai kuwa alitokwa machozi wakati uamuzi huo ukitangazwa baada ya kuwakumbuka wananchi wa jimbo lake.
"Nimefanya na nina mipango mingi ya kusadia wananchi wa Kigoma katika nyanja mbalimbali. Ufumbuzi wa hili utapatikana kwa njia ya mazungumzo ya sheria za nchi," alisema Kafulila kwa kupitia ujumbe mfupi baada ya gazeti hili kutaka kujua amepokeaje uamuzi huo.
Wakati akisema hivyo, jana Katibu Mkuu wa chama hicho, Samuel Ruhuza, alikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutoa taarifa ya maamuzi yaliyofikiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa, akisema mbunge huyo alionekana kuwa na makosa ya kujenga mtafaruku, hivyo wajumbe wakaamua kumvua uanachama.
Kafulila alikuwa amekaa katika moja ya ofisi za chama kwa takriban saa nne wakati Ruhuza akizungumza na waandishi wa habari na baada ya kumalizika kwa mkutano huo, mbunge huyo hakutaka kuzungunza chochote.
Akisoma maazimio ya NEC iliyokutana juzi, Ruhuza alisema kuwa baada ya kupitia tuhuma nzito zilizotolewa juu ya Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, waliona kuwa hakuwa na makosa na chama kimechukua jukumu la kumpa pole.
Ruhuza alisema wajumbe walipokea na kujadili utetezi wa Mbatia na maelezo ya waleta tuhuma akiwamo, Mbwana Hassani na wengine 26, waliosaini hati ya kutokuwa na imani na mwenyekiti huyo.
Alisema kikao pia kilijadili tuhuma dhidi ya Kafulila na wanachama wengine ambao walijenga mtafaruku ndani ya chama kwa kupiga vita chama nje ya vikao vya chama.
Mbali na Kafulila, Ruhuza aliwatangaza wanachama wengine waliovuliwa uanachama kuwa ni pamoja na Hashim Rungwe, aliyewahi kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Wengine waliovuliwa ni Hassani, ambaye alikuwa Kamishna wa chama katika Mkoa wa Tanga na Yothamu Lubungira, Lucy Kapia, Ali Omar Juma na James Bazitsa.
Katika mkutano huo, Ruhuza aliwataja wanachama wengine 16 ambao walipewa karipio kali kuwa ni Joseph Nyoni, Ussa Hussein, Ameir Ali, Kayumbo Kabutali, Bashiry Bayona, Daimon Mwasampeta, Kassim Libenanga, Patrick Salhanga, Greyson Mwasenga, Amina Suleiman na Juma Vuai.
Wengine ni Maryam Juma, Suwed Othman, Salma Juma, Henry Mapunda na Felix Mkosamali (Mbunge wa Mhambwe). Hatua hiyo ya NCCR-Mageuzi imeungwa mkono na wabunge wawili wa chama hicho, Moses Mkosamali (Kasulu Mjini) na Agripina Bulyogela (Kasulu Vijijini) pamoja na Godbless Lema wa Arusha Mjini (CHADEMA).
Katika maoni yake, Lema alisema Kafulila ni rafiki yake mkubwa ambaye amekuwa akimsifu kwa uwezo wake lakini akadaii uamuzi wa chama chake ni wa msingi sana kutokana na mwanasiasa huyo kushindwa kuelewa kwamba hakuna mtu aliye maarufu zaidi ya chama.
"Kafulila lazima akubali amekosea na hapaswi kukata tamaa kwa adhabu hii bali ajifunze kutokana na kosa hilo, iko siku atasimama tena na kurejesha umaarufu wake kisiasa," alisema Lema na kuongeza kuwa huo ni msimamo wake binafsi, ambao anautoa kwa kukumbukia kile kilichowapata madiwani wa chama hicho jijini Arusha, waliokiuka maamuzi ya chama, hivyo kuvuliwa uanachama.
"Ni bora chama kikabaki na watu wachache kuliko kuogopa kuondoa baadhi ya wanachama wanaochochea vurugu," alisema Lema.
Naye, Machali alisema alichokifanya Kafulila hakistahili msamaha hata kidogo. Kwamba kushindwa kuheshimu sheria zilizowekwa ndani ya chama ni tatizo ambalo linaweza kuwafikisha pabaya.
"Nilimkanya rafiki yangu Kafulila lakini akashindwa kunielewa, mimi sipendi unafiki juu ya hilo, ila hakufanya kitu kizuri," alisema Machali.
Machali alisema Kafulila alifanya kosa kubwa kulinganisha chama chao na Chama cha Mapinduzi (CCM) ilhali akijua wao si CCM.
Kwa upande wake, Buyogela, alisema Kafulila alikuwa akifanya maamuzi yake bila kushirikisha wabunge wenzake na kwamba waliumia kumpoteza ila wamefanya hivyo kwa lengo la kudumisha nidhamu ndani ya chama.
"Hata mtoto unaweza kumbeba miezi tisa tumboni ila baadaye akabadilika na akawa hakusikilizi, basi utaamua kumuacha na kuiachia jamii, katika chama hakuna aliye juu ya sheria," alisema.