Nani atafanya nchi isitawalike?

Nani atafanya nchi isitawalike?

sulphadoxine

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
2,257
Reaction score
649
KUMEKUWEPO shutuma nyingi zinazotolewa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) eti baadhi ya kauli na vitendo vya wanasiasa vina lengo la kuifanya nchi isitawalike.


Bila kuweka bayana ni nani hao wanaolalamikiwa, lakini ni dhahiri kidole hicho kitakuwa kinalenga vyama vya upinzani, ambapo kwa sasa tafsiri ya neno ‘upinzani' kwa CCM, ni kama kumaanisha uhaini, jambo linalowafanya viongozi na wafuasi wa vyama hivyo kujihisi kama wakimbizi wa kisiasa!


Bahati nzuri siku hizi mwenye macho haambiwi tazama, kwa sababu yote yanayofanyika hapa Tanzania hayahitaji elimu ya kiwango cha shahada, kupambanua kipi ni kipi, kwani mara nyingi tumekuwa tukiwasikia baadhi ya viongozi wa chama tawala na serikali wakipaza sauti kwenye majukwaa ya kisiasa kuwashutumu viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani eti wana agenda ya siri ya kutaka kuifanya nchi isitawalike, kwa nia ya kukidhi malengo yao kisiasa.

Kwa kawaida kila mwenye tochi humulika kwanza miguuni pake kujihakikishia usalama wake, kabla ya kumulika kwingineko, isijekuwa nyoka yupo miguuni mwake wakati yeye aking'ang'ana kuwamulikia wengine kwani Waswahili husema ukimnyooshea kidole kimoja mwenzako, ujue kwamba vidole vyako vinne vyote vilivyobaki vinakuelekea wewe mwenyewe.


Kwa kuwa tochi ya utawala imeshikiliwa na CCM, ni vyema nikaanza makala kwa kuwatahadharisha wao kabla ya kuwaelekea hao wanaonyooshewa kidole kwa kudhaniwa kuwa wana agenda ya siri ya kutaka kuhakikisha nchi hii haitawaliki. Ndiyo, CCM wanapaswa kujitafakari kwanza wenyewe, kabla ya kuwanyooshea kidole wengine!


Kauli hizi zinazodaiwa kuwa ni za kichochezi zimekuwa zikisadikiwa kutolewa na wanasiasa wa vyama mbalimbali ingawa kwa sehemu kubwa lawama zote zimekuwa zikielekezwa kwa vyama vya upinzani kupitia propaganda za CCM eti kwamba vyama hivyo vimekuja kuvuruga amani ya nchi yetu kwa kuleta uchochezi, vinalenga kuleta vita na kuwagawa wananchi kwa misingi ya udini na ukabila n.k.

Lakini CCM, wanasahau kuwa yapo mambo mengi tu yanayoweza kuifanya nchi isitawalike, baadhi ya mambo kama hayo ni pamoja na kunyimwa haki na uhuru, idadi kubwa ya wananchi kukosa huduma za msingi, ubaguzi, upendeleo, udini, ukabila, umasikini wa kupindukia n.k.

Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayoweza kuifanya nchi kukosa amani na hatimaye kujikuta katika vurugu za hapa na pale zinazoweza kuzaa mapigano au vita na kuifanya nchi isitawalike.

Kwa mfano; hata hao wanaoitwa wachochezi, wakati mwingine hutafsiriwa vibaya tu na watu wa upande wa pili, kwani neno ‘uchochezi' katika maana nyingine halina tofauti sana na neno ‘hamasa' ingawa lengo la kila upande, ndilo hasa huamua maana ‘hasi' au ‘chanya'ya neno hilo. Ndiyo maana, mfano; ‘wadai' wanapoitafsiri hali hiyo kama ‘hamasa', upande wa pili ambao ni wa ‘wadaiwa' huliona tendo hilo kama ‘uchochezi'!

Nachelea kwenda ndani sana katika kulinyumbulisha hilo neno, lakini walau kila upande unaweza kuelewa maana na matumizi ya maneno ‘uchochezi' na ‘hamasa' bila kujali maana yake ambayo hutegemea wewe umesimama upande gani. Itoshe tu kusema hata wakoloni waliwaita magaidi ama wachochezi, watu kama Nelson Mandela, Mwalimu Nyerere, Jomo Kenyatta n.k, ingawa kwa raia wa nchi zao waliwaona kama mashujaa na wanaharakati wahamasishaji!


Nikirejea kwenye mada yangu kuu ya kauli na vitendo vya wanasiasa vinavyoweza kuifanya nchi isitawalike, kama ambavyo imekuwa ikipigiwa parapanda kwenye majukwaa ya kisiasa na viongozi hasa wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ningependa kutumia mifano kwa baadhi ya viashiria vinavyoweza kuifanya nchi isitawalike.

Kama utakumbuka katika chaguzi kuu zilizopita, mwaka 2000, Mchungaji Kakobe alipita akimnadiAugostine Mrema achaguliwe kuwa Rais kwa kutumia mwavuli wa dini huku akisisitiza kwamba ndiye chaguo la Mungu.


Uchaguzi mwingine wa 2005, CCM nao wakaingiza kwenye ilani yao kipengele cha ahadi ya kuwapa Waislamu Mahakama ya Kadhi, jambo lililoleta mtikisiko mkubwa wa udini ambao hata baada ya Kikwete kuapishwa kuwa Rais, alikiri kuwepo mpasuko huo.


Ingawa Mrema na Kakobe hawakuwa na ilani ya chama yenye ahadi ya udini ama ukabila kwa jamii fulani ya Watanzania, lakini ni wazi maneno yao yaliibua hisia fulani kwa watu wasio wa imani hiyo ya dini. Tushukuru Mungu kampeni hiyo ilishindwa, lakini wasiwasi wangu ni ile ahadi ya CCM ambayo ni rasmi, kwa sababu ipo kimaandishi kwenye ilani yao ya uchaguzi uliopita.

Ikumbukwe kwamba kikundi cha Kiislamu cha Bokoharam cha nchini Nigeria, kiliundwa kupigania maslahi halali ya Waislamu ambao waliahidiwa kupitia ilani na sera za uchaguzi za baadhi ya vyama vya siasa, kwamba wakishinda wataruhusu utawala wa Kiislamu unaofuata misingi ya Sharia katika baadhi ya majimbo yanayokaliwa na Waislamu wengi.

Kwakuwa wanasiasa hao wenye uchu wa madaraka, waliyafanya hayo wakiwa na lengo la kukubalika kisiasa bila kujali maslahi ya imani za jamii ndogo nyingine zilizopo kwenye majimbo hayo, leo hii huko hakutawaliki kufuatia vita na vurugu za kidini zisizokwisha baada ya wahusika kuunda serikali na kupuuza ahadi hiyo. Je, hapo kuna tofauti gani na yaliyofanywa na CCM hapa kwetu, ikizingatiwa kuwa ahadi ni deni?


Sikumbuki kwa nini ahadi ya CCM, kuhusu Mahakama ya Kadhi ilishindwa kutekelezwa, wala sijui ni majibu gani walipewa Waislamu kuhusu kutotekelezwa kwa ahadi hiyo iliyokuwa kwenye ilani ya uchaguzi ya chama hicho, lakini kama kwa namna yoyote ile waliwahi kujitetea kwamba ilikwamishwa baada ya kupingwa na Wakristo, basi huo unaweza kuitwa uchochezi!


Kana kwamba hayo hayatoshi, chama hicho tawala pia kimekuwa mstari wa mbele kwa propaganda chafu kama walivyozitumia kukisambaratisha Chama Cha Wananchi (CUF), na kukipotezea umaarufu. Waliuhadaa umma kwamba chama hicho ni cha udini, kimejengeka katika misingi ya Uislamu, huku wakikihusianisha na ugaidi kwa kutumia baadhi ya wakuu wa vyombo vya dola kutangaza kukamata shehena ya visu vilivyodaiwa kumilikiwa na CUF!


Wimbi hilo la lugha hatarishi limeendelezwa na chama hicho pia dhidi ya chama kingine kinachopata nguvu baada ya CUF, kwa maana ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema. Hiki kimekuwa kikihusianishwa na ukabila na udini kidogo, jambo ambalo ni hatari kwa umoja na mshikamano wetu ambao ndiyo msingi mkubwa wa kuishi kwa amani na utulivu.

Nilimshangaa mbunge mmoja wa CCM katika mojawapo ya vikao vya bunge, akiwanyooshea kidole wabunge wa Chadema, tena mbele ya Kiti cha Spika, kwamba wamo humo mjengoni kwa kuchaguana kwa misingi ya ukoo, undugu, ukabila na ukanda, kana kwamba haitoshi akaibuka tena na hoja ya kuwa ana ushahidi kwamba Chadema, ni magaidi ambao yuko tayari kuwatolea ushahidi wa kulithibitisha hilo hata mbinguni!

Huyu bwana alisema bungeni wakati kesi ikiendelea kumkabili kiongozi mmoja wa Chadema ambaye amefutiwa tuhuma za ugaidi. Licha ya hatua hiyo ya kufutiwa tuhuma za ugaidi bado propaganda hizo za uchonganishi ziliendelea kuenezwa na Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, pale alipokaririwa na gazeti linalomilikiwa na chama chake, akiwaasa Wana-Igunga kushirikiana na mbunge wao aliyerejeshewa ubunge na kuachana na magaidi (akimaanisha Chadema). Huo ni ‘uchochezi' ama ‘hamasa'? Jibu litategemea uko upande gani!


Suala jingine ni matumizi mabaya ya rasilimali za nchi kunakopelekea kukosekana kwa huduma muhimu kwa jamii kubwa ya watu huku wachache wakiishi kama wako peponi, mfano ni shule zenye sura ya kibaguzi ambapo watoto wa walalahoi, wanasoma shule za kata zinazodhaniwa kutoa elimu duni, wakati watoto wa viongozi na wakubwa wakisoma shule binafsi, zenye kila kitu zinazojulikana pia kama Academy. Hata ‘huduma bora' za afya zinazopatikana nje ni kwa vigogo wa serikali na walionazo na zile za ndani za ‘bora huduma' kwa walalahoi. Mazingira haya si uchochezi?


Tuje kwenye matumizi mabaya ya vyombo vya dola yanayodhaniwa kufanywa hasa dhidi ya vyama vya upinzani na wakati mwingine kusababisha hata mauaji kwenye mikutano na maandamano ya amani ya wafuasi wa vyama hivyo kwa lengo la kuvipaka matope mbele ya umma. Vipi kukamatwa mara kwa mara kwa wabunge na viongozi wa upinzani kiasi cha kushindwa kuwatumikia wananchi, misukosuko ya Kiti cha Spika kinacholaumiwa kwa kuwa na upendeleo wa wazi n.k.



Mambo ni mengi tu yanayoweza kuigawa jamii na kupelekea nchi isitawalike, likiwamo lile la kucheza na haki za wakulima kama ilivyotokea huko Liwale, sera mbovu za ardhi na uwekezaji zinazozua mapigano kati ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na wenyeji, wimbi kubwa la vijana wasio na ajira wanaozalishwa na mfumo mbovu wa elimu ya ‘kujibia mitihani' ambayo haimuandai mwanafunzi kujitegemea n.k.


Ndiyo maana nasema, itoshe tu kusema kwamba Serikali ya CCM inapaswa kujitathmini kwanza yenyewe kuhusiana na kauli, vitendo na mambo yanayoweza kuifanya nchi isitawalike, kabla ya kuwanyooshea wengine vidole. Ikumbukwe kuwa vurugu zilizotokea kwa wenzetu wa Afrika Kaskazini na Uarabuni zilisababishwa kwa kiasi kikubwa na chuki zilizopandikizwa na serikali yenyewe
 
slaa na chama chake nadhan nimejibu,mods hamishia juu la siasa huu uzi
 
Back
Top Bottom