Nani akitumiwa — Mondlane au Leo Milas?

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
Na Ahmed Rajab

ALIZALIWA Marekani katika mji wa Pittsburgh, Texas. Mama yake akiitwa Catherine Bell Miles na baba yake akiitwa Leo Clington Aldridge Sr. Wazazi hao, Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, walimpa mtoto wao jina lile lile la baba yake: Leo Clington Aldridge.

Ukubwani alijitambulisha kwa jina la Leo Milas na akisema kwamba alizaliwa Msumbiji katika ukoo wa chifu fulani. Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 29 na alisema alikwenda Marekani alipokuwa na umri wa miaka 19. Hata hivyo, alikuwa hajui lugha yoyote ya Msumbiji. Si Kimakonde, si Kimakua, si Kichopi, si Kimwani, si lugha yoyote ya kienyeji. Na ingawa akizungumza Kihispania alikuwa hawezi kuzungumza Kireno, lugha ya wakoloni wa Msumbiji.

Licha ya yote hayo, Milas alifanikiwa kuwazuga wengi waamini aliyokuwa akiyasema. Miongoni mwa aliowateka akili alikuwa Dk. Eduardo Mondlane, Rais wa mwanzo wa chama cha ukombozi wa Msumbiji, Frente de Libertação de Moçambique (Frelimo).

Frelimo hakikuwa chama cha kawaida tangu kiasisiwe 1962. Kiliundwa kwa kuunganishwa vyama vitatu vya wananchi wa Msumbiji. Vyama hivyo, MANU, UDENAMO na UNAMI, vilikuwa haveshi kuparurana na kusuguana roho.

Julius Nyerere, waziri mkuu na Rais wa mwanzo wa Tanganyika na baadaye wa Tanzania, ndiye aliyevishinikiza vyama hivyo viache kuzozana vyenyewe kwa vyenyewe na viungane viwe kitu kimoja. Nyerere pia ndiye aliyefanya juu chini hata Mondlane akaibuka kiongozi wa chama kipya cha Frelimo.

Nyerere na Mondlane walikutana kwa mara ya kwanza Machi 1955 Nyerere alipokwenda New York kudai uhuru wa Tanganyika mbele ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa (UN Trusteeship Council).

Wakati huo Mondlane alikuwa akifanya kazi katika Baraza hilo. Mondlane alikuwa na usuhuba mkubwa na Nyerere aliyekuwa akiwasiliana naye mara kwa mara katika shughuli zake za kuutetea uhuru wa Tanganyika.

Nyerere alivutiwa na Mondlane. Nadhani alivutiwa zaidi na usomi wake kushinda uanaharakati wake wa kisiasa. Kwa hakika, Mondlane hakuwa na sifa ya kusimama kwenye majukwaa na kuulaani ukoloni wa Ureno katika muda wote aliokuwa Marekani. Wareno, kwa upande wao, wakimtaka arudi Msumbiji kwenda kufanya kazi katika utawala wa kikoloni nchini humo. Alikuwa ni mzaliwa pekee wa Msumbiji aliyekuwa na shahada ya PhD.

Sifa kubwa ya Mondlane kwa wakati huo ilikuwa ya usomi. Alikuwa amesoma katika vyuo vikuu mbali mbali Afrika Kusini, Ureno na Marekani ambako Chuo cha Oberlin cha Ohio kilimtunukia shahada yake ya mwanzo ya B.A. katika somo la anthropolojia. Aliipata shahada yake ya uzamili (MA) katika masomo ya anthropolojia na elimujamii (sociology) kwenye chuo kikuu cha Northwestern na shahada ya uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu hicho hicho. Baadaye alipata fursa ya kuwa mhadhiri wa muda kwenye Chuo Kikuu cha Harvard. Alikuwa Harvard kwa muda wa mwaka.

Mwaka 1957 Mondlane aliajiriwa kufanya kazi ya utafiti katika Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa. Aliifanya kazi hiyo, iliyompa fursa ya kutembelea Afrika, kwa muda wa miaka mine.

Mwanzoni mwa 1961 Mondlane alifunga safari kutoka Marekani akenda Msumbiji ambako Gavana Mkuu alimpokea na kumpa heshima ya kuwa “shujaa wa Kireno”. Hapo ndipo Wareno walipojaribu kumpa kazi katika utawala wa Msumbiji lakini aliwakatalia.

Aliyoyashuhudia Msumbiji yalizidi kumfungua macho kuhusu madhila ya ukoloni wa Ureno, hususan kwa upande wa elimu ya watoto wa Kiafrika. Mondlane alikaa Msumbiji kwa muda wa miezi miwili akizuru sehemu mbali mbali za nchi.

Aliporudi New York Mondlane alijiuzulu kazi yake ya Umoja wa Mataifa ili aweze kushiriki katika harakati za kisiasa kwa vile masharti ya kuajiriwa kwake na Umoja wa Mataifa hayakumruhusu awe mwanaharakati.

Aliandika ripoti kuhusu aliyoyaona Msumbiji wakati wa ziara yake na akaonya kwamba huenda pakazuka mapigano kama ilivyokuwa Angola. Aliikabidhi ripoti hiyo kwa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Baada ya kuacha kazi Umoja wa Mataifa akawa profesa wa historia na elimujamii (sociology) kwenye chuo kikuu cha Syracuse.

Mondlane alikuwa amejawa na hisia za kutaka kuikomboa nchi yake kutoka kwa Wareno waliokuwa wakiitawala Msumbiji tangu mwanzoni mwa karne ya 16.

Nyerere alizitambua sifa za Mondlane za usomi pamoja na uzoefu wake wa kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa. Alimuona kuwa ni mtu atayeweza kuwaongoza wananchi wenzake katika kupigania uhuru wa nchi yao. Kwa sababu hizo Nyerere alimuahidi Mondlane kwamba Tanganyika itapopata uhuru itamsaidia aikomboe Msumbiji.

Tanganyika ilipopata uhuru Desemba 1961, Nyerere aliitimiza ahadi yake. Ndipo ulipofanywa mkutano wa kuviunganisha vyama vya siasa vya Msumbiji. Mkutano huo uliofanywa kwenye ukumbi wa Arnatouglo, Dar es Salaam Juni 25, 1962 ulimchagua Mondlane awe rais wa chama na Mchungaji Uria Simango awe makamu wake wa kwanza.

Waziri Mkuu wa Tanganyika Rashidi Kawawa na waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Oscar Kambona, nao pia walihudhuria mkutano huo na wakatoa hotuba zilizoupongeza umoja wa Frelimo.

Leo Milas alikuwa Marekani na hakuhudhuria mkutano huo wa kihistoria. Wala hakuna aliyekuwa akimjua miongoni mwa waasisi wa Frelimo isipokuwa Mondlane. Waliwahi kukutana New York na ajabu ya mambo ni kwamba Mondlane sio tu alimuamini kwamba kweli alizaliwa Msumbiji lakini pia alivutiwa na umahiri wake.

Ulipofika wakati wa kuwachagua viongozi wengine wa Frelimo Mondlane aliwapendekeza watu waliokuwa karibu naye wapewe nyadhifa za uongozi ndani ya chama. Waliohudhuria mkutano huo wanasema kwamba kwa kweli hapakuwa na uchaguzi. Alisimama Mondlane na karatasi yenye orodha ya majina ambayo aliyataja. Miongoni mwayo yalikuwa majina ya Marcelino dos Santos na Leo Milas.

Dos Santos, mshairi ambaye hadi leo akiwa na umri wa miaka 90 bado ni mfuasi wa itikadi ya Umarx na Ulenin, alifanywa katibu wa mambo ya nje na Milas alitangazwa kuwa katibu wa habari na utamaduni.

Lilipotajwa jina la Dos Santos baadhi ya waliohudhuria, waliokuwa na siasa za kibaguzi za “ugozi”, walipiga kelele wakipinga wakidai kwamba Dos Santos si mwana wa Msumbiji bali ati alitokea Cape Verde. Sababu hasa waliyompingia ni kwamba Marcelino dos Santos amechanganya damu ya Kireno. Pia alipingwa kwa kuwa na mke wakizungu kutoka Afrika Kusini.

Serikali ya Tanganyika iliahidi kukipa chama cha Frelimo msaada wa fedha zisizopungua dola za Marekani 30,000. Fedha hizo zilikusudiwa kupanga ofisi, kuwalipa wafanyakazi na kwa safari za kuhudhuria mikutano muhimu ya kimataifa.

Baada ya mkutano kumalizika, Mondlane alifanya haraka akatoka ukimbini akaingia kwenye teksi kuelekea uwanja wa ndege kwa safari ya kurudi New York.

Huku nyuma Mondlane alikiacha chama kichanga cha Frelimo kikiwa kimezongwa na mizozo ya aina kwa aina miongoni mwa viongozi wake. Walikuwa hawana msimamo mmoja kuhusu mbinu za kutumika kuwaondoa wakoloni nchini mwao.

Mondlane aliporudi New York alirejea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Syracuse. Wakati huo huo akitafuta misaada ya fedha ya kukisaidia chama chake na akiendesha siasa za kuupinga ukoloni wa Kireno nchini Msumbiji. Alipoanza kupelekewa ripoti za mizozano ndani ya chama chake huko Dar es Salaam, Mondlane mwishoni mwa 1962 aliamua kumpeleka Milas ende kuyatanzua mambo akiwa ni mwakilishi wake binafsi. Alimwandikia barua Kambona akimuomba amsaidie Milas.

Alipowasili Dar Novemba 14, 1962, Milas alizidi kuyakoroga mambo na kuwafitinisha viongozi wa Frelimo . Mwanzoni mwa Januari 1963 Mondlane alipata ripoti kutoka Dar es Salaam kwa Milas akimuarifu kwamba amewafukuza viongozi wawili wa Frelimo, David Mabunda na Paulo Gumane. Milas alimwambia Mondlane kwamba alichukua hatua hiyo baada ya kuarifiwa na polisi wa Tanganyika ya kuwa viongozi hao wakishirikiana na Wareno.

Muda si muda kibao kikamgeukia Milas kwani wenzake ndani ya Frelimo waligundua akidanganya na hakuwa mwananchi wa Msumbiji. Wengine wakasema akitumiwa na idara mojawapo ya kijasusi ya Marekani.

Kuna wasemao kwamba Milas hakuwa jasusi wa CIA kwani wanadai kuwa kuna ushahidi kwamba CIA ikifanya njama za kumkashifu Milas ili kumkinga Mondlane aliyekuwa kipenzi cha Wamarekani. Mondlane alikuwa na mke wa kizungu wa Kimarekani na kwa sababu hiyo kuna waliokuwa wakisema kwamba yeye ndiye aliyekuwa akitumiwa na CIA.

Lawi Sijaona aliyekuwa waziri wa nchi katika ofisi ya makamu wa pili wa Rais wa Tanzania, Rashidi Kawawa, anasemekana kuwa miongoni mwa waliokuwa wakimchimba Mondlane na kumpaka matope ya kisiasa.

Mondlane aliuliwa Dar es Salaam kwa kitabu kilichotegwa bomu Februari 3, 1969. Haijulikani nani hasa aliyemuua. Alikuwa na maadui ndani ya Frelimo lakini pia watawala wa Kireno walikuwa adui zake. Polisi wa Tanzania waliwahi kusema kwamba wanamjua nani aliyemuua lakini hadi sasa hawakumtaja.

Milas hakudumu muda mrefu ndani ya Frelimo. Alifukuzwa kutoka Frelimo na Tanzania akenda Sudan ambako aliwahi kukamatwa na kufungwa Khartoum. Mwaka 1963 alisilimu na alibadili jina na kujiita Seifulaziz Leo Milas. Baadaye alihamia Ethiopia ambako akifundisha chuo kikuu na akiandika vitabu. Alifariki huko Ethiopia.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom