Nahitaji msaada, ninayopitia katika maisha yananivunja moyo

Naona mtu kapigwa klebu moja matata kabisa, aisee watu wanafukua makaburi
Mkuu kama unapitia changamoto pole sana
 
Moja kwa moja nianze na historia yangu.

Nimezaliwa miaka 27 iliyopita huko mkoani Mara wilaya ya Musoma Vijijini. Nikiwa mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto 6 wa kiume tukiwa watatu na wa kike watatu. Wazazi wangu walikua wakulima. Kwa vile Kijiji chetu kipo kandokando ya Ziwa Victoria, baba yangu pia alikuwa akifanya shughuli ya uvuvi wa dagaa.

Mwaka2001 nilianza Darasa la Kwanza. Ilipofika mwaka 2007 nikiwa Darasa la Saba, baba yangu alianza kulalamika kusikia maumivu ya kichwa; alienda hospitali kuanzia pale kijijini hadi hospitali ya mkoa lakini hakupata kupona. Ndugu walishauriana apelekwe kwa waganga ndipo alianza kwenda kwa mganga mmoja baada ya mwingine bila mafanikio.

Aliuza baiskeli na baadhi ya mashamba ili agharamie matibabu yake lakini hakupata nafuu. Baadaye tatizo lilikuwa kubwa na kupelekea kupoteza uwezo wa kuona. Kiukweli hili lilikua pigo kubwa kwa familia maana yeye ndiye tulikua tukimtegemea Kama injini ya kuendesha familia. Jukumu la kulea familia lilibaki kwa mama yangu pamoja na mimi.

Nilianza kujikita katika uvuvi kwa muda wote nilipokua nasubiria matokeo ya darasa la saba, nilihakikisha familia yangu inapata mboga na mahitaji madogo Kama mafuta ya taa na sabuni. Mwaka 2008 nilibahatika kuchaguliwa kidato cha kwanza katika shule iliyokua Kijiji cha pili kutoka kijijini kwetu ni mwendo wa kilometa tano. Kwa vile baba hakuwa na uwezo wowote zaidi ya kututegemea, nilianza kwenda kuvua samaki maarufu Kama "kukokora" ili nipate pesa ya mahitaji ya shule na ada.

Nilifanikiwa kupata nusu ya mahitaji na pesa nyingine mama aliuza mihogo nikafanikiwa kujiunga kidato cha kwanza japo nilichelewa nilianza mwezi wa pili. Mama yangu aliendelea kupambana kwa kulima vibarua na wadogo zangu wawili ambao nao walikua wameanza kuwa wakubwa. Siku za Jumamosi na kipindi cha likizo nilikuwa nikimsaidia mama kazi za shamba na nikiendelea kuvua samaki ili kutafuta pesa ya ada na uniform.

Mnamo mwaka 2010 mwezi wa7 nikiwa Kidato cha Tatu, baba yetu alifariki; nilisoma kwa bidii japo changamoto zilikua nyingi na mwaka 2011 nikafanikiwa kumaliza kidato cha nne. Nikiwa nasubiria matokeo nilianza biashara ndogondogo ya kuchuuza samaki nilimuomba baiskeli mjomba wangu nikawa napeleka samaki Musoma mjini kwenye soko linaloitwa Kwasaanane lililopo Mitaa ya Nyakato.

Matokeo yalipotoka nilipata division four ya point 27. Kutokana na uwezo mdogo kiuchumi nilikua sina msaada wowote wa kuendelea na masomo, niliendelea na kazi ya kuchuuza samaki huku nikihifadhi pesa kwa ajili ya kuendelea na masomo ilipofika mwezi wa nne mwaka 2012.

Kuna kijana mmoja wa pale kijijini tulisoma nae shule moja Ila yeye alinitangulia madarasa mawili; yeye alipohitimu kidato cha nne alielekea Dar-es-Salaam kutafuta maisha. Kuna ndugu yake alinipa namba yake ya simu tukawa tunawasiliana na mimi nilivutiwa kwenda Dar kutafuta maisha. Mwaka 2012 mwezi wa 5 nilichukua akiba niliyokua nimeitunza nikafunga safari kuelekea Dar kutafuta maisha. Nilifikia kwa rafiki yangu aliyekuwa amepanga maeneo ya Tegeta Kwa Ndevu alikua akifanya kazi ya ulinzi. Alinipokea na kuanza kunitambulisha kwa rafiki zake, mmoja wa wale rafiki zake alinitafutia kazi ya house boy kwa boss mmoja mitaa ya Kigamboni.

Nilikua nikijituma na kutekeleza majukumu yote niliyopewa, nilionyesha nidhamu ya hali ya juu. Hakika boss alinikubali; watoto wake walipokua wakitoka shule nilikuwa nikiwasaidia kufanya homework na kuwafundisha; yule boss alinipenda sana na kunichukulia kama ndugu yake. Kuna siku aliniambia nitafute kituo cha resiters ili nirudie mtihani. Nilifurahi na kuanza mara moja kutafuta kituo na kujiandikisha na kila mida ya jioni baada ya kumaliza kazi nilikuwa nikienda kusoma. Hatimaye, mwaka2013 nilirudia mtihani matokeo yalitoka nikawa nimefaulu. Aliamua kunilipia ada nikajiunga na Advance.

Nilipokuwa nakaribia kumaliza Form 6, boss wangu aliugua ghafla akalazwa kama wiki moja bahati mbaya akafariki. Kwangu ulikuwa msiba mzito. Nilifanya mitihani nikiwa na mawazo sana baada ya kumaliza mtihani nilitakiwa kwenda JKT huko Tabora (Msange). Nilimaliza kozi ya JKT nakurudi Dar. Pale kwa boss wangu nilikuta nyumba imepangishwa familia imehamia Dodoma.

Nilirudi kwa rafiki yangu tayari na yeye alikuwa ana familia. Nilianza kujichanganya mtaani na kufanikiwa kupanga chumba, selection za vyuo zilitoka nilichaguliwa chuo cha DUCE kozi ya BAED (Bachelor of Arts with Education) ila sikubahatika kupata mkopo. Ilibidi niahirishe masomo nikaendelea kufanya vibarua mtaani. Niliona kurudi mkoani nikama kuanza upya nilijitahidi kutunza akiba lakini kutokana na majukumu ya familia huko nyumbani sikufanikiwa kupata chochote kwani wadogo zangu wawili wa mwisho bado nao wanasoma.

Mwaka uliofuata 2018 nilijaribu tena kuomba mkopo Loan Board kwa mara nyingine, sikufanikiwa. Nikaamua kuachana na mambo ya chuo na kujikita kutafuta maisha, kwani wadogo zangu bado ni wanafunzi wa mwisho yuko Form 2 na mwingine anaingia Form 6 na mimi ndiyo tegemeo lao, na mama yangu hana msaada wowote zaidi yangu.

Nilianza kufanya biashara ya dagaa nilikua naagiza dagaa Mwanza na kuuza kwenye minada ya wiki maeneo mbalimbali hapa Dar, lakini nimeishia kutapeliwa na mtu ambaye nilimwamini na tunatoka kijiji kimoja na tulifanya biashara kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu. Alikuwa akinitumia mzigo.

Kiukweli, kwa sasa nimeyumba. Sina mtaji wa kutosha kuendesha biashara na majukumu nayo yameniandama. Nilikuwa naomba kama kuna mtu atakae guswa basi anikopeshe japo laki5 au anitafutie kazi popote najua humu kuna watu wa kada tofauti tofauti. Nitatoa ushirikiano kwa taarifa zaidi atakazohitaji kutoka kwangu.
Katafute shule private ufundishe
 
Back
Top Bottom