Mzee Kaunda na mchango wake kwenye ukombozi wa Afrika, na uhusiano kati ya China na Afrika

ldleo

Senior Member
Jan 9, 2010
164
250
VCG11447097585.jpg

VCG31N992107558.jpg

Aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zambia mzee Kenneth Kaunda amefariki dunia katika hospitali ya jeshi mjini Lusaka, alikokuwa amelazwa kutokana na kuumwa. Kuumwa na kuaga dunia kwa Mzee Kaunda, sio tu kumewafanya watu wengi wakumbuke mchango wake katika ukombozi wa eneo la kusini mwa Afrika, na mchango wake katika kuhimiza uhusiano kati ya China na Zambia, na kati ya China na nchi za Afrika.Tukianza na kuangalia juhudi zake kwenye ukombozi wa nchi za Afrika kusini mwa Sahara, itakumbukwa kuwa yeye alikuwa ni mmoja wa viongozi muhimu kwenye nchi zilizoitwa Nchi za Mstari wa Mbele katika ukombozi wa eneo la kusini mwa Afrika FLS na kupambana na utawala wa wazungu wachache. Mwaka 1985 alichukua nafasi ya mwenyekiti wa nchi hizo kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere, na kuifanya Zambia kuwa kituo cha wana ukombozi. Ni katika kipindi chake kulikuwa na mafanikio ya kuondoa ukoloni nchini Namibia, na utawala wa wachache nchini Afrika Kusini.Tunakumbuka kuwa ni katika kipindi hichohicho cha ukombozi kwenye eneo la kusini mwa Afrika, yeye na Mwalimu Nyerere walianzisha uhusiano wa karibu na China. Mzee Kaunda na Nyerere walionana na mwenyekiti Mao Zedong, na ni wao walimwomba mwenyekiti Mao awapatie msaada wa kujenga reli itakayosaidia kuleta ukombozi wa eneo la kusini mwa Afrika. Alikumbusha akisema walipowasilisha ombi kwa Mwenyekiti Mao na Waziri Mkuu Zhou Enlai, jibu walipolpewa ni kuwa “tutakwenda pamoja kuijenga reli hiyo”, na amesema ni kweli walikuja kama ndugu kujenga reli hiyo.

Mzee Kaunda pia alikuwa kiongozi mwanzilishi na mtu mwenye uelewa wa kina wa uhusiano kati ya China na nchi za Afrika. Alishuhudia ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika tangu wakati wa mapambano ya kupigania uhuru, alishuhudia ushirikiano kati ya China na Zambia, na China na Afrika wakati akiwa Rais wa Zambia, na pia alishuhudia ushirikiano huo hata baada ya kuondoka madarakani. Kwa hiyo alipozungumzia uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, alikuwa anazungumzia jambo alilolijua kwa undani na alilokuwa na uhakika nalo.

Katika miaka ya hivi karibuni wakati wa wimbi kubwa la tuhuma za vyombo vya magharibi kuwa China inafanya uporaji wa raslimali barani Afrika, Mzee Kaunda alisema wanaoishutumu China kufanya uporaji wa raslimali barani Afrika, ndio waliofanya uporaji wa raslimali barani Afrika kwa mamia ya miaka. Alikumbusha kuwa China ilizisaidia nchi za Afrika kwenye mapambano dhidi ya ukoloni, na imekuwa inazisadia kuendeleza uchumi, na hicho ndio China inakifanya kwa nchi za Afrika, ikiwa ni rafiki wa kweli wa nchi za Afrika.

Mzee Kaunda alikuwa mwanasiasa wa mwisho wa kizazi cha kwanza kwenye uhusiano kati ya China na Afrika. Yeye amewahi kuwa na uhusiano wa karibu kabisa na Mwenyekiti Mao, aliyekuwa waziri Mkuu wa China Bw Zhou Enlai na hata Bw. Deng Xiaoping, na pia amewahi kufanya ziara mara nyingi nchini China kwa hiyo alifahamiana na wanadiplomasia na maofisa mbalimbali waandamizi wa China. Moja kati ya kauli zake zinazokumbukwa ni ile aliyosema “kama China ilitusaidia waafrika kwenye miaka ya 70, wakati hakuna aliyetaka kutusaidia, kwanini sasa awatilie mashaka wachina”.

Wakati Afrika inaagana na Mzee Kaunda, ni wazi kuwa mchango wake kwenye mahusiano kati ya Zambia, Afrika na China, hauwezi kusahaulika.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom