Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Joseph Waryoba Butiku, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameishachaguliwa kihalali, hivyo hakuna msingi wa kudai aondoke madarakani, akisisitiza kuwa Rais huyo si wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee bali ni Rais wa Watanzania wote.
Akizungumza katika maelezo yake, Butiku alisema jamii haina sababu ya kuogopa kumzungumzia Rais pale panapokuwa na hoja au changamoto, mradi mjadala huo uwe wa nia njema na kwa heshima kubwa.
"Sasa tatizo ni nini? Hatutaki kusema ni Rais? Rais ni mmoja wetu tu. Anaweza kuwa na tatizo lake, tulizungumze na aruhusu tuzungumze. Huwezi kuwa na baba ndani halafu hazungumzi, halafu panapokuwa na watu 20 anazungumza. Kwa hiyo Rais ni Rais wetu," amesema Butiku.
"Tunamzungumzia kama tunazungumza kwa nia njema na kwa heshima kubwa kabisa. Hatuzungumzi kumuondoa kwa sababu utaratibu wa kumuondoa upo. Ndiyo maana hatukubaliani na wanaosema aondoke kesho; hatukubali," ameongeza.
Akirejea falsafa ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Butiku amesema hata pale taifa linapofanya kosa katika uchaguzi wa kiongozi, suluhu si kuvunja misingi ya utawala, bali kurekebisha kwa utaratibu uliowekwa.
"Alishachaguliwa, na Baba wa Taifa alisema mkifanya kosa mkamchagua. Huyu hatujafanya kosa; yeye hana kosa, alichaguliwa kupitia chama. Kwa hiyo ni Rais wetu, siyo wa CCM, ni Rais wa Tanzania," amesema Butiku.
Kauli ya Butiku inakuja wakati kukiwa na mijadala mbalimbali ya kisiasa nchini, kutokana na matukio ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao umeacha maumivu kwa raia kufuatia vifo vya watu wengi kabla, wakati na baada ya uchaguzi.