Wapendwa
Ndugu ,Jamaa na Marafiki,
Nakukumbusha mtani, tamaa kweli sikati
Nilishasema zamani, kuwacha kweli siwati
Na wala siyo utani, nina mpenda kwa dhati
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!
Mwengine sitotamani, ingawa nakula buti
Ni huyu kwangu mwandani, juweni wana kamati
Asiye na mshindani, kwa kweli nampa chati
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!
Majungu pia pigeni, moyoni mwangu hatoki
Semeni mengi semeni, mseme ana nishiti
Ni huyu kwangu moyoni, siwezi kum saliti
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!
Nafikiria kichwani, kupenda kama mauti
Yaingiapo mwilini, huwezi pata zingiti
Utabaki mtu duni, wakati u mahututi
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!
Nakomelea mwishoni, na tena hapa tamati
Mwenzenu nipo penzini, nasubiria wakati
Nasema wangu mwandani, tamaa kwake sikati
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!
Kijana Bin Mbichi
SHAURI SASA UKATE
Mapenzi si kama ufu, Mfu hajui kupenda
Ni jambo lilo tukufu, si vyema kuwa na inda
Amelisifu Latifu, na nyoyo yanazilinda
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate
Miaka inakatika, ni nini wasubiria
Mvi zitaja kufika, bila lengo kutimia
Au waweza zimika, huna ulicho twachia
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate
Wajipa nyingi adhabu, kweli wajiadhibia
Moyo waupa na tabu, mapenzi waunyimia
Tafuta mwenye adabu, huwezi kuja jutia
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate
Kibuti alikupatia, ni wewe umetwambia
Binti kaonyesha nia, njema hajakusudia
Mbona wapapatikia, wadai kuvumilia
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate
Hakuna alo majungu, huruma twakuonea
Ondoa huo ukungu, kaumu yakuzomea
Jipatie mcha mungu, mpole aso gomea
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate
Sipendi uwe wa duni, sababu eti mapenzi
Hofu na shida mwilini, kwa asiyejua kuenzi
Tabu wajipia nini, kupenda huyo hawezi
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate
Sindano Mwana wa Ganzi (SMG)
Safarini Tongoleani
LA KWAKO LA PANDE MOJA
Yailahi yarabana, Mola mtangu na tangu
waja twakimbizana, Mapenzi nayo machungu
Kila leo danadana, Tusaidie e Mungu
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
Choveki u mahututi, Kwa penzi usilopata
Nimefanya utafiti, na pia ninazo 'data'
Ulisha pigwa kibuti, yanini sasa kufata
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
Mapenzi jambo swadifu, wawili mkipeana
Na wala hayana kifu, mwaruka mwatekenyana
Yataka na utwiifu, hakuna cha kunyimana
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
Mapenzi ni ya wawili, la mmoja sijaona
Haitakiwi bahili, vyote vyote mwapeana
Utanawiri na mwili, kwa penzi lisilo bana
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
Na hili la pande moja, si pendo ni ukatili
Huwezi kuwa na hoja, limefungwa ka pingili
Hata useme wangoja, haliwezi kuwa 'dili'
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
Kwa kweli pendo sioni, yako ni mataabiko
Iweje wewe huoni, pasipo na furahiko
Au tupulize honi, waweza pata zinduko
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
Na pendo ni kuwa nalo, si kama wafikiria
Ukiona hilo silo, ni bora kujiachia
Utafute lile ndilo, moyoni utatulia
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
Yatosha kubembeleza, fanya tafuta mwingine
kuna miji ya Arusha, Tanga Pwani na kwingine
Waweza kubahatisha, ujitoe kivingine
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja
SINDANO MWANA WA GANZI (SMG)
KIJIJINI TONGOLEANI