Mwenziyo unanikosha!

Choveki

JF-Expert Member
Apr 16, 2006
457
164
Mpendwa,

Salamu natuma kwako, naomba uzipokee
Nauliza hali yako, nataka nikujulie
Barua hii ni yako, ujumbe uusikie
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Binti Msemaovyo, mwenziyo unanikosha
Siropoki hovyohovyo, na hilo nakujulisha
Nasema ujue hivyo, sikwamba nimechemsha
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Kwa maumbile na pozi, kiroho chaniripuka
Nashindwa kufanya kazi, kichwani wanizunguka
Nauomba ukimbizi, kwa weye uloumbika
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Ningali bado kijana, m-bichi nisiyeoa
Tuli nimetulizana, ni mwenza natafutia
Usiku pia mchana, nikweli nakuwazia
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Pia tena mcha mungu, huyo huyo wako wewe
Naomba tena kwa mungu, niweze kupata wewe
Dini yako ndiyo yangu, nasema bila kiwewe!
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Msomi ki kweli kweli, kijana miye nasema
Shahada ya uzamili, nimemaliza si zama
Ki pesa nipo kamili, nimejaliwa karama
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Nitawacha ukapera, na hilo nasisitiza
Kijana sina papara, nashinda nikikuwaza
Nitakufanya kinara, uweze kuniongoza
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Nane nasema tamati, kwako uliye umbika
Hakuna ambayo nyeti, kwangu yaliyofichika
Ni mimi mtanashati, nakuagia waraka
Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha!

Wakatabahu waraka,

Kijana Bin Mbichi .
 
Mpendwa;

Yapata mwezi wa pili, ningali nikisubiri
Nahisi kama ni zali, kwanini hunifikiri
Sichezi miye kidali, mwenziyo hapo nakiri
Ningali nikisubiri, mwenziyo kwangu ni zali!

Nauliza yako hali, pia jibu nasubiri
Itume japo mahali, barua ulo hariri
Nakesha nikiwa chali, usiku nikifikiri
Ningali nikisubiri, mwenziyo kwangu ni zali!

Barua hii ya pili, na wala sifanyi siri
Nambie huo ukweli, pitia wako msiri
Nijibu hata makali, majibu yalo mahiri
Ningali nikisubiri, mwenziyo kwangu ni zali!

Niandikayo ni kweli, bila yake kachumbari
Namtafuta dalali, aweze kukuhubiri
Uweze kunikubali, halafu tujivinjari
Ningali nikisubiri, mwenziyo kwangu ni zali!

Ninayapata makali, kichwani nikifiri
Nahisi kama kabali, ya mtu mwenye jeuri!
Dhoofu nisiye hali, nashindwa kuwa ngangari!
Ningali nikisubiri, mwenziyo kwangu ni zali!

Barua siyo batili, na wala siyo stori
Najua siyo katili, ni yepi yalo kujiri?
Yamenijaa maswali, nasaka yako nambari!
Ningali nikisubiri, mwenziyo kwangu ni zali!

Saba zilizo kamili, ni mwisho wangu jasiri
Zaidi ya pilipili, moyoni mwangu nakiri
Uchungu huo mkali, naomba uufikiri
Ningali nikisubiri, mwenziyo kwangu ni zali!

Wasalam.

Daima akupendaye,

Kijana Bin Mbichi
 
duh swahiba mashairi makali kinoma kama ningekuwa mie ningeingia kichwa kichwa bila hata ya kuangalia mlango wa kutokea

ila ikifika mwezi wa tatu na ukahakikisha hajakujibu ujue hakutaki sasa ni juu yako kusuka au kunyowa
 
....kama ningekuwa mie ningeingia kichwa kichwa bila hata ya kuangalia mlango wa kutokea"ila ikifika mwezi wa tatu na ukahakikisha hajakujibu ujue hakutaki....."
......ka'asemavyo mkuu hapo juu ukifika mwezi watatu hujajibiwa basi kipepeo hicho si chako!! itabidi utafuta ghuba nyingine ilo tulii.goodluck.

Wapendwa
ndugu, jamaa na marafiki;

Hiyo tamaa sikati, ninawajuza wengine
Nimpendaye kwa dhati, ni huyu siyo mwengine
Nitasubiri wakati, miezi hata minane
Mitatu ama minane, nitasubiri kwa dhati!

Nitasubiri kwa dhati, mitatu hata minane
Na bado tampa chati, hata akiwa mjane
Ni huyu huyu binti, sitaki hao wengine
Mitatu ama minane, sitojalia wakati

Nasema kweli sikati, kwa huyu siyo wengine
Ingawa jibu sipati, upite mwezi wa nane
Mwengine simtafuti, na wala sendi pengine
Mitatu ama minane, tamaa miye sikati

Dhamira yangu ya dhati, kutozengea wengine
Sitotumia visheti, wala vitamu vingine!
Mitego ama manoti, kuwinda hao wengine!
Mitatu ama minane, hiyo tamaa sikati

Maneno mengi siteti, bali barua nyengine
Najua ni vizingiti, muvisemavyo wengine
Ni miye mtanashati, ambaye sina mwingine
Mitatu ama minane, kamwe tamaa sikati

Undeni hata kamati, nakadhalika nyingine
Kuwacha kweli siwati, wala silongi mengine
Majibu kwenu ya dhati, ni huyu siyo mwingine
Mitatu ama minane, nitasubiri wakati

Nasema hapa tamati, sitoongeza mengine
Nawajulisha umati, pamoja nanyi wengine
Ingawa kuwa sipati, sitompenda mwengine
Mitatu ama minane, tamaa hiyo sikati!!

Wakatabahu waraka,

Kijana Bin M'bichi
 
Tamati iso na jibu,sitokubali asilani
Utampata tabibu,ukitazama kwa ndani
Kuna akina mwajabu,dadae na hamdani
Aweza kuwa tabibu,akutoe mashakani.

Usijikune sharubu,Kwa mawazo ya moyoni
Mtume hata habibu,akuletee mwandani
Uliza wa kina babu,walifanyaje zamani
Moyoni sipate tabu,Kumtafuta mwandani

Mbona wajipa sulubu,na kuumia moyoni
Nenda hata bububu,takwambia kwa shani
Utoe hata dhahabu,Maneno ndio sumuni
Upole pia adabu,Vitakushindia mwandani
 
Mpendwa

Mwenziyo ninarejea, kukujulisha kiumbe
Barua nasubiria, ya kwako yenye ujumbe
Kimwana weye sikia, sikwiti wala mzembe
Uloumbika kiumbe, ni miye nakumbushia

Ni miye nakumbushia, ambaye nitaabani
Mshenga nilitumia, na humu mtandaoni
Naomba yako barua, ibwage hata njiani
Uloumbika kiumbe, ni miye nakumbushia

Imeshapita kadhaa, niisemayo miezi
Nisijepata kichaa, ama uchizi uchizi
Kuhepa hilo balaa, kwako miye mkimbizi
Uloumbika kiumbe, ni miye nakumbushia

Sikiya kweli sikia, na wala si longolongo
Mapenzi yanitesea, pia yavunja mgongo
Ukweli nakuambia, tena sisemi uongo
Uloumbika kiumbe, ni miye nakumbushia

Mwenziyo yanizidia, mashaka nikifikiri
Kichwani ninahisia, ni mengi natafakari
Kitanda nikilalia, nahisi ni misumari
Uloumbika kiumbe, ni miye nakumbushia

Tamati ninaishia, ewe unayenikosha
Ningali nasuburia, na huku wanikondesha
Charanga hiyo barua, uweze kuniponyesha!
Uloumbika kiumbe, ni miye naku agia!

Wasalaam,
"Umkondeshaye"
 
Mpendwa,

Ni mingi imetimia, niisemayo miaka

Na bado nasubiria, kwa dhati ninatamka

Moyoni naugulia, kwa kweli hilo kumbuka

Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha

Sikia mwenza sikia, ningali nataabika

Naliya miye nalia, kichwani nikisumbuka

Moyoni nakulilia, ni lini utakumbuka?

Kwa pozi na maumbile, mwenziyo unanikosha

Waraka wangu pokea, usome nimeandika

Zamani hizo tangia, kichwani hujanitoka

Kwa kweli ninaumia, machozi yanidondoka

Ningali nikisubiri, wajua kwangu ni zali?

Mshenga natafutia, ambaye hatajachoka

Wa kwanza, wa pili pia, wasema walishachoka

Wahisi nitajifia, wasema kwa uhakika

Ningali nikisubiri, wajua kwangu ni zali?

Wazee wanizengua, wasema ninazeeka

Kwa hamu wanangojea, harusi ije sikika

Wameikata tamaa, harusi yetu kufika

Mitatu ama mine, tamaa hiyo sikati!

Sitaikata tamaa, kichwani mwako kumbuka

Kwa ndugu pia jamaa, ukweli unajulika

Wasisitiza komaa!, wajua utanasika

Mitatu ama minane, tamaa hiyo sikati

Mwenziyo nakuitia, itika kwanza itika

Nahisi umesinzia, ni lini utaamka?

Najua hujasikia, sauti yanikauka

Uloumbika kiumbe, ndo miye nakumbushia

Kapera na sijaoa, ni wewe wasubirika

Tulia kwangu tulia, najuwa umetukuka

Ni wangu wewe najua, mwengine sijamtaka

Uloumbika kiumbe, ndo miye nakumbushia

Kikomo nakomelea, wakatabahu waraka

Nahisi umejulia, ni wewe uloumbika

Mwengine sijapatia, na wala sitomtaka

Ningali nasubiria, majibu yako mwanana

Wakatababu,

Kijana Bin Mbichi
 
Nakusalimu kaka yangu, nakutakia Amani
Nahisi wako uchungu, umeanza ni zamani
Leo ni mwaka wa tatu, mpenziwe wamtaman
iElewa huyo mwenzangu,hakutaki asilani

Mara ya kwanza tunaona, kwa shahiri ulinena
Sifa zako twakumbuka, hapa ndani ulimwaga
Akajibu kwa dharau, msichana ulie mlenga
Elewa huyo mwenzangu, hakutaki asilani

Barua yako ya pili, ukakusudia kukiri
Kilokua chasumbua, humo mwako kifuani
Msichana akazidi kukuona mpuuzi
Elewa huyo mwenzangu, hakutaki asilani

Mara ya tatu ukaja, kwa dhiki na hasama
Jibu lako kulitaka, na bado hukupata
Mwanadada kama kawa, akapiga kimya kimya
Elewa huyo mwenzangu, hakutaki asilani

Hatimae ukasema kua shaka laingia
Ukakosa uhakika, maana kimya cha sumbua
Ila tamaa hukukata, ingawa hukujibiwa
Elewa huyo mwenzangu, hakutaki asilani

Ndoto yako hujatimiza, huku muda unasonga
Wazee wanauliza: Bin Mbichi kaoa?
Walazimisha kumngoja, yako ndoa hujafunga
Elewa huyo mwenzangu, hakutaki asilani.

Unaumwa, wateseka…Na moyo wasononeka
Nakuonea huruma, ndugu yangu wahathirika
Tafuta pakufarijika, ingawaje kwa dakika
Elewa huyo mwenzangu, hakutaki asilani
 
Nakusalimu kaka yangu, nakutakia Amani
Nahisi wako uchungu, umeanza ni zamani
Leo ni mwaka wa tatu, mpenziwe wamtaman
iElewa huyo mwenzangu,hakutaki asilani
............................
Unaumwa, wateseka…Na moyo wasononeka
Nakuonea huruma, ndugu yangu wahathirika
Tafuta pakufarijika, ingawaje kwa dakika
Elewa huyo mwenzangu, hakutaki asilani

Nilishajibu zamani, kwa ndugu pia jamaa
Marafiki na watani, ukweli wakajulia
Walijikuna vichwani, wakati wakishangaa
Kwa ndugu pia jamaa, nilishajibu zamani

Nasema kweli zamani, mwenzenu nilijulia
Mwengine sitotamani, ingawa anizengua
Walisema utotoni, kichwani wanisumbua
Kwa ndugu pia jamaa, nilishajibu zamani

Hamsa wa ishirini, miezi ikapitia
Sikuwacha asilani, kichwani kufikiria

Ni huyu wangu mwandani, ingawa asua sua
Kwa ndugu pia jamaa, nilishajibu zamani

Kijana Bin Mbichi
 
Wapendwa
ndugu, jamaa na marafiki;

Hiyo tamaa sikati, ninawajuza wengine
Nimpendaye kwa dhati, ni huyu siyo mwengine
Nitasubiri wakati, miezi hata minane
Mitatu ama minane, nitasubiri kwa dhati!

Nitasubiri kwa dhati, mitatu hata minane
Na bado tampa chati, hata akiwa mjane
Ni huyu huyu binti, sitaki hao wengine
Mitatu ama minane, sitojalia wakati

Nasema kweli sikati, kwa huyu siyo wengine
Ingawa jibu sipati, upite mwezi wa nane
Mwengine simtafuti, na wala sendi pengine
Mitatu ama minane, tamaa miye sikati

Dhamira yangu ya dhati, kutozengea wengine
Sitotumia visheti, wala vitamu vingine!
Mitego ama manoti, kuwinda hao wengine!
Mitatu ama minane, hiyo tamaa sikati

Maneno mengi siteti, bali barua nyengine
Najua ni vizingiti, muvisemavyo wengine
Ni miye mtanashati, ambaye sina mwingine
Mitatu ama minane, kamwe tamaa sikati

Undeni hata kamati, nakadhalika nyingine
Kuwacha kweli siwati, wala silongi mengine
Majibu kwenu ya dhati, ni huyu siyo mwingine
Mitatu ama minane, nitasubiri wakati

Nasema hapa tamati, sitoongeza mengine
Nawajulisha umati, pamoja nanyi wengine
Ingawa kuwa sipati, sitompenda mwengine
Mitatu ama minane, tamaa hiyo sikati!!

Wakatabahu waraka,

Kijana Bin M'bichi
mmh mshair mzur weye had raha na majib ya hapo kwa hapo jaman mmh
 
UNGALI WASUBIRIA?

Heri ya mwaka mpya, pokea zangu salamu
vipi ya kwako afya, maisha na majukumu
Ni muda upo kimya, sina ninachofahamu
Je vipi yule mwandani, ungali wasubiria?

Ni muda tena kitambo, walia na penzi lake
Nadhani kunalo jambo, hauna haiba kwake
Au akuona shombo, wewe si mapigo yake
Je vipi yule mwandani, ungali wasubiria?

Wasubiri hadi lini, bora upya ujipange
Tafute alo makini, yule nadhani mtenge
Madhila hutobaini, mtani wacha unyonge
Je vipi yule mwandani, ungali wasubiria?

Subira ina kikomo, siku nazo hazigandi
wavutwa na chake kimo, kifua nao mtindi
Hiki kipimo dhaifu, kama hanao ufundi
Je vipi yule mwandani, ungali wasubiria?

Na penda unapopendwa, usipopendwa achia
Ni wengi tumeshatendwa, ndo maana nakwambia
Si wote waliofundwa, wachache wathaminia
Je vipi yule mwandani, ungali wasubiria?

SINDANO MWANA WA GANZI (SMG)
 
UNGALI WASUBIRIA?
..................................................
Na penda unapopendwa, usipopendwa achia
Ni wengi tumeshatendwa, ndo maana nakwambia
Si wote waliofundwa, wachache wathaminia
Je vipi yule mwandani, ungali wasubiria?

SINDANO MWANA WA GANZI (SMG)

Wapendwa
Ndugu ,Jamaa na Marafiki,

Nakukumbusha mtani, tamaa kweli sikati
Nilishasema zamani, kuwacha kweli siwati
Na wala siyo utani, nina mpenda kwa dhati
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!

Mwengine sitotamani, ingawa nakula buti
Ni huyu kwangu mwandani, juweni wana kamati
Asiye na mshindani, kwa kweli nampa chati
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!

Majungu pia pigeni, moyoni mwangu hatoki
Semeni mengi semeni, mseme ana nishiti
Ni huyu kwangu moyoni, siwezi kum saliti
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!

Nafikiria kichwani, kupenda kama mauti
Yaingiapo mwilini, huwezi pata zingiti
Utabaki mtu duni, wakati u mahututi
Tamaa kweli sikati, juweni ndugu juweni!

Nakomelea mwishoni, na tena hapa tamati
Mwenzenu nipo penzini, nasubiria wakati
Nasema wangu mwandani, tamaa kwake sikati

Kijana Bin M’bichi

SHAURI SASA UKATE

Mapenzi si kama ufu, Mfu hajui kupenda
Ni jambo lilo tukufu, si vyema kuwa na inda
Amelisifu Latifu, na nyoyo yanazilinda
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate

Miaka inakatika, ni nini wasubiria
Mvi zitaja kufika, bila lengo kutimia
Au waweza zimika, huna ulicho twachia
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate

Wajipa nyingi adhabu, kweli wajiadhibia
Moyo waupa na tabu, mapenzi waunyimia
Tafuta mwenye adabu, huwezi kuja jutia
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate

Kibuti alikupatia, ni wewe umetwambia
Binti kaonyesha nia, njema hajakusudia
Mbona wapapatikia, wadai kuvumilia
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate

Hakuna alo majungu, huruma twakuonea
Ondoa huo ukungu, kaumu yakuzomea
Jipatie mcha mungu, mpole aso gomea
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate

Sipendi uwe wa duni, sababu eti mapenzi
Hofu na shida mwilini, kwa asiyejua kuenzi
Tabu wajipia nini, kupenda huyo hawezi
Tasubiri hadi lini, shauri sasa ukate

Sindano Mwana wa Ganzi (SMG)
Safarini Tongoleani
LA KWAKO LA PANDE MOJA

Yailahi yarabana, Mola mtangu na tangu
waja twakimbizana, Mapenzi nayo machungu
Kila leo danadana, Tusaidie e Mungu
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

Choveki u mahututi, Kwa penzi usilopata
Nimefanya utafiti, na pia ninazo 'data'
Ulisha pigwa kibuti, yanini sasa kufata
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

Mapenzi jambo swadifu, wawili mkipeana
Na wala hayana kifu, mwaruka mwatekenyana
Yataka na utwiifu, hakuna cha kunyimana
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

Mapenzi ni ya wawili, la mmoja sijaona
Haitakiwi bahili, vyote vyote mwapeana
Utanawiri na mwili, kwa penzi lisilo bana
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

Na hili la pande moja, si pendo ni ukatili
Huwezi kuwa na hoja, limefungwa ka pingili
Hata useme wangoja, haliwezi kuwa 'dili'
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

Kwa kweli pendo sioni, yako ni mataabiko
Iweje wewe huoni, pasipo na furahiko
Au tupulize honi, waweza pata zinduko
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

Na pendo ni kuwa nalo, si kama wafikiria
Ukiona hilo silo, ni bora kujiachia
Utafute lile ndilo, moyoni utatulia
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

Yatosha kubembeleza, fanya tafuta mwingine
kuna miji ya Arusha, Tanga Pwani na kwingine
Waweza kubahatisha, ujitoe kivingine
Mapenzi hapo sioni, la kwako la pande moja

SINDANO MWANA WA GANZI (SMG)
KIJIJINI TONGOLEANI
 
Kumbe huu uzi bado uko? nitarudi

Amani fanya urudi, muase ndugu choveki
Afanye jambo la budi, amuache yule feki
Na raha atafaidi, asijue nini dhiki
CHOVEKI ANISHANGAZA, KWA PENZI KUNG'ANG'ANIA

Beti nilimtumia, kumpa yeye nasaha
Hekima nikajazia, aepuke ya karaha
Awache kung'ang'ania, ajenge yake staha
CHOVEKI ANISHANGAZA, KWA PENZI KUNG'ANG'ANIA

Beti zangu hakujibu, sijui hata kwa nini
Labda ni zake ghadhabu, kwa vile bado kuwini
Au kashikwa aibu, binti kutomthamini
CHOVEKI ANISHANGAZA, KWA PENZI KUNG'ANG'ANIA

Na hataki shaurika, eti mrembo ni wake
siku nazo zakatika, aishi kivyake vyake
uzee utamfika, bila hata ya mwenzake
CHOVEKI ANISHANGAZA, KWA PENZI KUNG'ANG'ANIA

Amani mpe shauri, atafute yeye mwenzi
Kuna wadada wazuri, mahodari wa mapenzi
Tena hawana viburi, kwa mema yao malezi
CHOVEKI ANISHANGAZA, KWA PENZI KUNG'ANG'ANIA

SINDANO MWANA WA GANZI (SMG)
KIJIJINI TONGOLEANI
 
8 Reactions
Reply
Back
Top Bottom