Mwenyekiti wa CHADEMA Usa River auwawa kinyama

Mwenyekiti wa CHADEMA auawa


na Grace Macha, Arusha


amka2.gif
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kata ya Usa River, wilayani Arumeru, Msafiri Mbwambo (38) ameuawa kwa kukatwa shingoni na kitu chenye ncha kali.
Kifo hicho kilitokea juzi majira ya saa mbili usiku eneo karibu na uwanja wa polisi Mji Mwema, ambapo wauaji hao walimkata shingo kwa kuanzia nyuma na kubakiza kidogo eneo la mbele ya shingo na kumwacha akiwa amelala chini kama aliyeanguka na pikipiki.
“Atakuwa amekatwa na kitu kama shoka kwani wamekata shingo kwa nyuma, tulipotoka ndani baada ya kuitwa tulimkuta amelala pale unapoona kuna damu, kichwa chake walikiweka juu ya jiwe, kiwiliwili chake kilikuwa kwenye pikipiki, mguu mmoja ukiwa chini mwingine juu kama vile alikatwa akiwa kwenye pikipiki akaanguka nayo.
“Unajua mimi nakaa nyumba ile lakini sikusikia tukio hili likitokea mpaka nilipokuja kugongewa na majirani na tulikuwa hatuna umeme ulikatika kama saa mbili zilizokuwa zimepita, ila ilikuwa majira ya saa tatu kasoro hivi,” alisema mwananchi anayeishi karibu na eneo lililipotokea tukio hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea takriban wiki moja baada ya watu wanne kuuawa kwa kunyongwa na miili yao kutupwa kwenye maeneo tofauti wilayani Arumeru, ambapo alisema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa vifo hivyo.
Naye mke wa marehemu, Eunice Mbwambo (30) alisema kuwa siku ya tukio marehemu alimchukua kwa pikipiki kutoka eneo la Kisambaro anakofanyia shughuli zake za kushona nguo majira ya saa mbili usiku akiwa na mtoto wao wa mwisho, Magreth (6) kati ya watatu walio nao na kuwapeleka nyumbani.
Alisema kuwa kabla hawajashuka kwenye pikipiki marehemu alipokea simu akamweleza kuwa anakwenda kwenye kioski kinachofahamika kwa jina la mmiliki, Hashimu, kwa ajili ya kumuona rafiki yake anayeitwa Gurisha Msuya, maarufu kama ‘Kipara’, ambapo baada ya muda ndipo akapata taarifa kuwa amekutwa amekufa.
Mmiliki wa kioski hicho, Hashimu Bakari na rafiki wa marehemu Mwambo, ‘Kipara’ walikiri marehemu kufika kwenye kioski hicho ambapo walisema kuwa aliondoka muda mfupi baada ya kupigiwa simu na kuondoka kwa ahadi ya kurudi baada ya muda mfupi kwa ajili ya kumpitia Kipara kwani wanaishi nyumba jirani lakini hakutokea mpaka majira ya saa nne usiku walipopata taarifa ya kifo chake.
“Marehemu alikuwa na kawaida ya kuja hapa kuangalia mpira, hakuwa mtu mgomvi na jana (Ijumaa) alikuja kuangalia uamuzi wa kikao cha CCM juu ya sakata la kuwataka mawaziri wajiuzulu ndipo akiwa hapa akapigiwa simu akaondoka, hakuwa mgomvi wala hakuwa anakunywa pombe, alikuwa Msabato,” alisema Hashimu.
Wakizungumza kwa wakati tofauti wakazi wa eneo hilo walihusisha kifo hicho na tabia yake ya kupigania haki na kupambana na ufisadi kwenye miradi ya wananchi, ambapo walidai kuwa alikuwa amefuatilia mpaka kwa ofisa mtendaji wa kata kuhakikisha kikao cha mapato na matumizi cha kitongoji cha Magadini ambacho akijafanyika kwa zaidi ya miaka minne sasa kinafanyika Jumatatu.
Wananchi hao, Jubileti Muro, Ruth Munisi, Eline Kisanga, Ibahimu Salum na wengine kadhaa ambao hawakuwa tayari majina yao kuandikwa gazetini walisema kuwa marehemu Mbwambo alipigania mkutano huo kwa kupeleka barua kwa Ofisa Mtendaji wa kata, Laizer John, ambaye aliagiza kikao hicho kifanyike Jumatatu.
Walisema kuwa ufuatiliaji wake wa mambo ulimfanya marehemu kutofautiana na viongozi wa kitongoji akiwamo Mwenyekiti wake, Matia Nathan, ambaye ilifikia hatua ya kumtolea vitisho ambavyo aliwahi kuwaeleza wananchi kwenye moja ya mikutano yake ya hadhara.
Walisema kuwa kwenye kikao hicho marehemu Mbwambo alikuwa amejiandaa kikamilifu kwa kukusanya nyaraka mbalimbali kuthibitisha tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma zinazofanywa na viongozi kwenye miradi ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Kata ya Laki Tatu, mradi wa kusambaza maji safi na salama na mradi wa machimbo ya kokoto kitongojini hapo.
Wananchi hao walisema kuwa marehemu alikuwa akisimamia jambo lake anakuwa na ushahidi wa kutosha, ambapo walitolea mfano kuwa aliweza kuwabana viongozi wakatoa fedha zilizokuwa zimekwisha kuliwa kwenye mradi wa maji, zilizotumika kutengeneza barabara kwa kiwango cha changarawe ambapo kwa sasa wanafikiria barabara hiyo waipe jina lake kwa ajili ya kumuenzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Nathan, alikanusha kutofautina na marehemu katika utendaji wake na kuwa hakuwahi kumtisha ambapo alisema kuwa yeye binafsi alikuwa akimpenda hasa kutokana na tabia yake ya kufuatilia mambo huku akiwa mkweli, kwani alikuwa akikosoa na kusifia panapostahili.
“Binafsi sijawahi kumtishia marehemu kwa kufuatilia mapato na matumizi ya kitongoji, nilikuwa nachukulia ufuatiliaji wake kama changamoto ya kufanya kazi vizuri zaidi,” alisema Nathan akiongea na Tanzania Daima kwa njia ya simu.
Alisema kuwa ni kweli alipanga kuitisha kikao cha uongozi kati ya Jumatatu na Jumanne ili waweze kupanga tarehe ya kufanya mkutano mkuu wa kitongoji kwa ajili ya kusoma taarifa ya mapato na matumizi huku akisema kuwa hana taarifa kama marehemu aliwahi kuwasiliana na mtendaji wa kata kuhusiana na suala hilo.
Naye Mbunge wa jimbo hilo, Joshua Nassari, aliwataka wananchi kuwa watulivu kwa kipindi hiki kigumu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wake ili kuhakikisha waliohusika na tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria

chanzo tanzania daima

 
Alazwe mahali Mungu atakapotaka! Ametangulia tu - tuliobaki tuko njiani kumfata kwani maandiko matakatifu yanasema "kila nafsi itaonja mauti"
 
Back
Top Bottom