figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,620
- 55,262
Mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu mkoani Singida zilizoanza jana Juni, 27 na zinatarajiwa kufungua, kuzindua, kuweka mawe ya msingi katika miradi 45 mbalimbali ya maendeleo ya wananchi, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20.1.
Mwenge huo ulioanza mbio zake katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida ukitokea mkoani Dodoma, utafungua miradi 14, utazindua nane, mawe ya msingi 13 na utatembela kumi.
Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mwenge huo yaliyofanyika jana kijiji cha Sanza, mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alisema kati za fedha hizo, zaidi ya shilingi 6.2 bilioni ni nguvu kazi ya wananchi, halmashauri shilingi bilioni moja, serikali kuu bilioni 13.2 na wahisani shilingi bilioni moja.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo ni ya kutoka sekta ya ufugaji, mazingira, maji, afya, elimu, barabara, utawala bora, kilimo, ushirika, biashara, ardhi na programu za mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.
Aidha, makabidhianao hayo, yalitumika pia kuzindua dawati la sekta binafsi ambalo litakuwa chini ya uratibu wa maafisa maendeleo ya jamii.
“Dawati litatambua kwa takwimu, mahali, aina ya shughuli na hali ya uzalishaji ili kuhakikisha ushiriki mtambuka unaowajibika ipasavyo ikiwemo kutoa taarifa ya soko la mazao mbalimbali. Lengo ni kurahisisha uwekezaji mkoani kwetu,” alisema Dk. Nchimbi.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za mwenge mwaka huu, Amour Hamad Amour, amesema kuwa amefurahishwa na wilaya ya Manyoni, kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha dhana ya Tanzania ya viwanda imeanza kutekelezwa kwa vitendo.
Alisema mradi wa ushonaji nguo na wa ufugaji nyuki kibiashara una viashiria vya wazi kuwa halmashauri ya Manyoni, itakuwa ya viwanda vidogo, ya kati na hata vikubwa kwa siku za mbeleni.
“Nitumie fursa hii kuwaomba maafisa wa maendeleo ya jamii, wahakikishe vikundi vya wanawake na vijana, wanapatiwa mikopo kutoka asilimia tano ya mapato ya ndani ya halmashauiri ili viweze kupata nguvu ya kuanzisha viwanda vidongo. Msiishie hapo, wapeni na mafunzo mbalimbali ya ufugaji nyuki, kuku na mifugo kibiashara,” alisema Amour na kuongeza.
“Na hawa akina mama waliojiunga kwenye kikundi cha ushonaji, wapewe mafunzo ya kuboresha shughuli zao ziweze kwenda na wakati”.
Mbio za mwenge wa uhuru asubuhi hii leo Juni, 28 zinatarajiwa kuendelea katika halmashauri ya Itigi na kesho Juni 29 utakimbizwa wilaya ya Singida.
Na Nathaniel Limu, Manyoni