Mdogo wa Waziri Nchimbi ajitosa Ubungo
na Andrew Chale
MDOGO wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi, aitwaye Alfred John Nchimbi (39), jana ameongeza idadi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wenye nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Ubungo mwakani.
Alfred Nchimbi, ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati ya Siasa Wilaya ya Kinondoni na Muhadhiri wa Chuo cha Utumishi wa Umma (Magogoni), alitangaza azima yake ya kugombea ubunge katika jimbo hilo, alipozungumza na waandishi wa habari jana, muda mfupi baada ya kufungua semina ya mafunzo ya siku moja ya anwai za jamii.
Kada huyo alisema kuwa, ameamua kujitokeza kuitaka nafasi hiyo ili kupata fursa ya kuwaongoza wananchi waliokosa fursa ya kufanya maamuzi sahihi, huku wengi wao wakipitia kwenye maisha magumu na ya mateso.
"Wakati ukifika nitagombea. Naomba ridhaa ya chama changu ambao ndio walio na maamuzi ya mwisho na wakinikubali nitagombea," alisema Nchimbi.
Alibainisha kuwa ana uhakika wa kupata nafasi hiyo adhimu ambapo ataitumia kwa kupeleka maendeleo katika jimbo hilo pamoja na kuwakomboa wananchi ambao kwa miaka mingi hawajapata maendeleo yanayotakiwa.
Aliongeza kuwa, ametumikia chama kwa muda mrefu na kuiva katika siasa jambo ambalo anaamini litamsaidia kufanikisha maendeleo ya huduma muhimu zikiwemo za miundombinu, afya na ulinzi.
Nia hiyo ya Nchimbi, inakifanya kinyang'anyiro cha kumtafuta mgombea ubunge wa CCM katika jimbo hilo kuwa kigumu baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga kutangaza mapema kuwania kiti hicho. Mbali na Mwangunga, kuna taarifa za kuaminika kuwa kada kijana wa chama hicho, Nape Nnauye, naye ni miongoni wa watakaowania kiti hicho kinachoshikiliwa na mbunge wa sasa, Charles Keenja, ambaye naye huenda akakitetea tena kiti hicho. Katika uchaguzi mkuu uliopita, Keenja alichuana vikali na kada machachari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, na kupata ushindi uliogubikwa na mizengwe mingi.