Chilojnr
JF-Expert Member
- Jul 5, 2012
- 302
- 1,306
“I want him dead,” (ninataka afe mara moja)
“Okey! Sir! Do you want us to kill his family too?” (Sawa! Mkuu! Unataka tuimalize na familia yake pia?)
“Yes! Just kill them all,” (ndiyo! Waue wote)
“Okey! No problem. Give us the time we are going to make you smile,” (sawa! Hakuna tatizo. Tutakupa tabasamu) alisema kijana mmoja.
Yalikuwa ni mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika kwa njia ya simu kati ya rais wa nchi ya Matapatapa, Bwana Salim Labad na vijana wake aliokuwa amewatuma kwa ajili ya kummaliza mtu mmoja na familia yake.
Hayakuwa mazungumzo marefu sana, ndani ya sekunde chake, wakamaliza na hatimaye kilichokuwa kikisubiriwa kilikuwa ni mauaji hayo kufanyika na rais huyo kupewa taarifa kwa kila kitu kilichokuwa kimefanyika.
Huo ulikuwa mwaka wa kwanza wa Rais Labad kukalia nchi ya Matapatapa. Alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipendwa ambao watu waliaminika kwamba kama wangekuwa viongozi wa nchi hiyo basi ilikuwa ni lazima nchi hiyo ipae kiuchumi kutokana na biashara kubwa aliyokuwa akiifanya mtu huyo.
Hakuwa mwanasiasa, alikuwa mfanyabiashara mkubwa, alifanya biashara sehemu mbalimbali duniani. Alijijengea heshima, alipata kila kitu alichokihitaji katika maisha yake, na kitu pekee alichokihitaji ambacho hakuwa akikipata kilikuwa ni saluti tu kutoka kwa polisi na wanajeshi.
Hakutaka kuwa mbunge, hakutaka kuwa mwenyekiti wa chama bali kitu alichokihitaji kilikuwa ni urais tu. Alitumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye chama chake mpaka kumpitisha. Alihonga kadiri alivyoweza na hatimaye kufanikiwa kuwa rais wa nchi hiyo.
Kutokana na sura yake ya kipole aliyokuwa nayo, wananchi wengi wakampenda na wengine kumfananisha na malaika huku mabango mitaani yakisema kwamba malaika alipewa nchi hiyo hivyo watu walitakiwa kusubiri neema.
Kabla ya kuwa rais wa nchi hiyo, Labad alikuwa mfanyabiashara mkubwa, aliyekuwa na migodi mingi ya dhahabu, alipendwa kwa sababu tu alikuwa mtu wa watu, kila alipokanyaga kulionekana kuwa na neema kubwa.
Aliwapenda wananchi wenzake, alikuwa tayari kufanya kitu chochote katika maisha yake lakini mwisho wa siku apate alichokuwa akikihitaji. Alitumia sehemu kubwa ya utajiri wake kwa watu wengine, masikini na watoto wa mitaani kitu kilichomfanya kupendwa kila siku.
Machoni alionekana mtu, alionekana kuwa mwema lakini maisha yake ya upande wa pili alikuwa mtu mbaya, katili, aliyewanyanyasa wanawake kingono kwa kufanya nao kilazima hasa baada ya kuwatuma vijana wake kwenda kuwanunua.
Alikuwa msambazaji mkubwa wa madawa ya kulevya, aliwatumia vijana wengi kusafirisha madawa hayo kwenda nchi mbalimbali duniani kama China, Pakistan na nchi nyingine nyingi.
Hakukuwa na mtu aliyeyaona maovu yake, kila alipoangaliwa, watu walimuona kuwa malaika ambaye alishushwa duniani kwa ajili ya kuwafurahisha na kuwaletea neema watu wote.
Japokuwa alikuwa na utajiri mkubwa lakini maisha yake hayakuwa na raha. Kila siku alikuwa mkimya, hakuwa mzungumzaji sana, moyo wake ulijaza kisasi kikubwa ambacho kila siku kilikuwa kikimfurukuta moyoni mwake.
Alikuwa kwenye ugomvi mzito na bilionea kutoka nchini Tanzania, Bwana Fredrick Massawe. Bifu hilo lililodumu kwa miaka mitano, lilisababishwa na upinzani wa biashara uliokuwa kati yao.
Japokuwa alikuwa raia wa Matapatapata lakini Labad hakutaka biashara zake ziishie nchini Matapatapa, alichokifanya ni kuzitawanya kwenda mpaka nchini Tanzania ambapo huko alitaka kuanzisha biashara ya kusambaza saruji, mabati na chokaa lakini kabla ya kufanya hivyo alitakiwa afuatilie taratibu zote, apate kibali kihalali kitu ambacho hakutaka kabisa kukifanya kwani aliamini kwamba kwa pesa alizokuwa nazo, zingemrahisishia kila kitu.
Serikali ya Tanzania ikamuwekea kizuizi kwa kumlazimisha kufanya kile alichotakiwa kukifanya. Hakutaka kufanya hivyo kwani aliamini angetozwa kodi kubwa, akakataa na hivyo kurudi nchini kwake na ndani ya wiki hiyohiyo, zile biashara zote alizotaka kuzifanya, zikaanza kufanywa na bilionea Massawe.
Hilo likawa kosa kubwa, Labad akaumia moyoni kwa kuhisi kwamba serikali ya Tanzania ilimuwekea vizuizi kwa sababu ya Massawe na ndiyo maana alipoamua kuondoka mwanaume huyo akachukua tenda hiyo. Moyo wake ukawaka kwa hasira. Hakutaka kukubali, hakutaka kumuacha Massawe akaishi, alichoamua ni kumuua, hivyo akaanza kupanga vijana wake.
Kumpata haikuwa kazi nyepesi, alihangaika kwa miaka yote hiyo, alipambana lakini hakufanikiwa. Massawe alikuwa na ulinzi mkubwa, kila alipokuwa, alikuwa na wanaume kama watano waliokuwa na bastola, mbali na vijana hao, pia kulikuwa na wengine ambao hawakuwa wakigundulika, wote hao walikuwa wakimlinda yeye.
“Nitamuua tu siku moja, haiwezekani nishindwe na wakati nishawahi kuua watu wenye ulinzi mkubwa zaidi yake,” alisema Labad huku akionekana kuwa na hasira kubwa.
Mpaka anapata urais wa nchi hiyo bado alikuwa akihangaika kumuua mwanaume huyo, alishindwa, moyo wake ulimuuma na siku ambayo aliambiwa kwamba Massawe na familia yake walitembelea katika Mbuga ya Wanyama ya Kizwalinda iliyokuwa hapo Matapatapa, akapanga kumuua katika kipindi hichohicho.
“Una uhakika ni yeye?” aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Siwezi kumchanganya mkuu! Ni yeye!”
“Nashukuru!”
Alipewa taarifa na askari wa mbugani ambao alikuwa amewaweka kuhakikisha kote anakuwa na ulinzi, kutokusemwa kwa mabaya aliyokuwa akiyafanya. Alipopewa taarifa kwamba mwanaume huyo alikuwa kwenye mbuga hizo akawasiliana na vijana wake na kuwaambia wafanye kila linalowezekana mpaka kuhakikisha mwanaume huyo na familia yake wanauawa kinyama kama kulipa kisasi.
****
“Sina amani mke wangu…” ilisikika sauti ya bilionea Massawe.
“Kwa nini mume wangu? Mbona unanitisha hivyo?”
“Sijajua! Ila sina amani kabisa.”
“Hapana ! Inawezekana kuna kitu! Hebu tusali kwanza,” alisema mke wake, Lydia aliyekuwa kitandani pamoja naye na hivyo kushikana mikono kuanza kusali.
Moyo wa bilionea Massawe ulikuwa mzito, hakuwa na furaha, moyo wake ulisononeka mno kana kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikienda kutokea. Alimwangalia mke wake, hakufurahia, walikuwa na safari ya kuelekea Matapatapa kwa ajili ya kutembelea mbuga ya wanyama lakini kila alipokumbuka safari hiyo, alikosa amani.,
Hakujua ni kitu gani kilikuwa kinakwenda kutokea. Aliamua kumshirikisha mkewe na kumwambia alichokuwa akijihisi moyoni mwake na hivyo kumwambia kwamba walitakiwa kusali.
Walifanya hivyo, mpaka sala inakwisha bado moyo wake ulikuwa vilevile. Alishindwa kuelewa sababu gani alikuwa katika hali hiyo.
“Mpigie simu daktari aje mara moja,” alisema Massawe.
Daktari wa familia akapigiwa simu na kufika nyumbani hapo. Alimpima Massawe kwa kuhisi labda alikuwa akiumwa lakini kitu cha ajabu kabisa, hakuwa na tatizo lolote lile.
“Huna tatizo lolote!”
“Kweli?”
“Ndiyo! Nimeangalia Malaria, typhord na magonjwa mengine, huna tatizo, hata presha yako ipo vizuri kabisa,” alisema daktari huyo wa familia.
“Sawa. Nashukuru!”
Usiku mzima hakuwa na amani moyoni mwake, alishindwa kulala, alikuwa na mawazo mno na kitu alichokuwa akikifikiria kilikuwa ni safari ya kuelekea nchini Matapatapa tu.
Alihisi kwamba angepata tatizo kwenye safari hiyo, alijaribu kumwambia mkewe waahirishe safari, ili kama itawezekana waende siku nyingine lakini mkewe hakukubaliana naye kwani alijua fika kwamba mumewe alikuwa bize mno na kama angekubaliana naye, kupata muda kama huo kufurahia na familia yake ingekuwa ngumu kupatikana.
“Haiwezekani! Ikishindikana kipindi hiki, utaniambia unakwenda Marekani, mara Uingereza au Kongo! Hebu tumalizane na jambo hili mume wangu,” alisema mkewe kwa sauti ya upole iliyoonyesha kwamba alikuwa na hamu kubwa ya kuwa na mumewe katika safari hiyo.
“Basi sawa. Waandae watoto kabisa.”
Hilo halikuwa tatizo, Lydia akawaanda watoto wao mapacha waliokuwa na miaka kumi na tano, Christopher na Christina kwa ajili ya safari ambayo ilitarajiwa kufanyika siku inayofuata.
Siku ya safari ilipofika, wakajiandaa na saa 4:12 asubuhi safari ya kwenda huko kwa kutumia ndege yao binafsi ikaanza. Kila mmoja akaonekana kuwa na furaha, ndani ya ndege walizungumza mambo mengi, walitaniana sana.
Ilipofika saa 5:25 ndege ikaanza kutua kwenye kiwanja kidogo cha ndege kilichokuwa katika Mbuga ya Wanyama ya Kizwalinda ambapo wakapokelewa na kupelekwa katika hoteli ya kifahari iliyokuwa hapohapo mbugani.
“Mungu ni mwema. Tutaitumia siku nzima kuzunguka mbugani, na kesho tutarudi nchini Tanzania,” alisema MAssawe huku akionekana kuwa na furaha tele.
“Ninashukuru kwa kuniheshimu mume wangu! Nina furaha sana kuwa pamoja nawe katika mbuga hii,” alisema mke wake huku uso wake ukionyesha kuwa na furaha tele.
Hawakujua kama siku hiyo ndiyo walitakiwa kuuawa na tayari wauaji walikuwa njiani kutekeleza azma yao.
***
Vijana watatu walikuwa njiani wakielekea katika Mbuga ya Wanyama ya Kizwalinda kwa ajili ya kutekeleza mauaji waliyokuwa wameambiwa. Walikuwa na mabegi yao na ndani ya mabegi hayo walikuwa na bastola ambazo wangezitumia kuimaliza familia hiyo.
Walionekana kuwa na hamu ya kufanya mauaji hayo kwani ni kazi ambayo walipewa na rais wa nchi hiyo ambaye alitaka kuona lile alilokuwa ameliagiza likifanyika kwa haraka sana pasipo watu wengine kugundua kitu chochote kile.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika mbugani hapo ambapo moja kwa moja wakachukua vyumba katika hoteli ileile na kujifanya kwamba ni Wamarekani waliofika mahali hapo kwa ajili ya kutembelea mbuga hiyo.
Kuwagundua ilikuwa ngumu kwani hata kwa jinsi walivyokuwa wakiongea, waliongea kama Wamarekani. Hawakuishia hapo bali hata fedha zao walitumia dola, yote hiyo ilikuwa ni kuwazuga wahudumu wa hoteli hiyo kwamba walikuwa Wamarekani waliofika hapo kwa ajili ya utalii.
Chumbani, wakaanza kupanga ni kwa namna gani wangeweza kufanikisha mpango wao. Kabla ya yote ilibidi wachunguze kwa makini ili wajue mahali ilipokuwa familia hiyo, hilo wala halikuwa tatizo kwani walimuita mhudumu mmoja na kumwambia kwamba walifika hotelini hapo kwa ajili ya kuonana na bilionea Massawe kutoka Tanzania.
“He is here,” (yupo hapa) alisema mhudumu kwa uchangamfu huku akiachia tabasamu pana, hakuishia hapo bali alimwambia mpaka vyumba walivyochukua yeye na familia yake.
“Thank you! Have the great day,” (nashukuru sana! Uwe na siku njema)
Wakarudi katika chumba kimoja walichokuwa wakipanga mipango yao na kutulia huko. Ilikuwa ni lazima kuhakikisha siku hiyo bilionea huyo na familia yake wanauawa kwani hawakuwa na siku zaidi ya mbili kukaa ndani ya hoteli hiyo.
Walipanga kufanya mauaji hayo usiku, muda ambao kila mtu atakuwa amelala. Mchana, walipokuwa wakienda katika matembezi yao ya kuona wanyama, walikuwa ndani ya gari moja na familia ya mzee huyo, hawakutaka kuua kwani idadi kubwa ya watu iliwaogopesha na mbaya zaidi kulikuwa na askari wa wanyamapori waliokuwa na bunduki.
“Tuwaue hapahapa ndani?” aliuliza jamaa mmoja kwa sauti ya kunong’oneza.
“Hapana! Tusubiri kwanza.”
“Ila hii ni nafasi yetu kubwa.”
“Najua! Ila hatutakiwi kugundulika. Usiwe na presha,” alisema jamaa mmoja.
Wakatulia, hawakutaka kuonyesha presha yoyote mpaka aliporudi hotelini ambapo saa mbili usiku, walikuwa wakiwafuatilia watu hao, jinsi walivyokuwa wakinywa juisi kwenye mgahawa hotelini hapo kama familia na mpaka walipokwenda chumbani.
Walifika huko na kutulia, haikuwa usiku sana hivyo kabla ya Chis na Tina hawajakwenda chumbani kwao walikaa chumbani humo na kuzungumza kama familia. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha tele, mkewe, ndiye aliyeonekana kufurahi zaidi kwani alimuondoa hofu mume wake kwamba safari hiyo isingekuwa na hatari yoyote ile, na kweli walikwenda, walitalii mpaka walipokuwa wakijiandaa kurudi, hakukuwa na jambo baya lolote lile.
“Nilikwambia! Hakuna baya lolote,” alisema mke wa Bilionea Massawe.
Wakati wakiwa wanazungumza humo ndani, Chris akasimama na kwenda chooni kujisaidia huku wengine wakiendelea kukaa chumbani hapo wakizungumza mawili matatu huku mazungumzo hayo yakishushiwa kwa kahawa tamu iliyokuwa moja ya huduma zilizokuwa zikipatikana humo.
Wakati wakiendelea kuzungumza, ghafla walisikia kama kitu kikiwa kimeanguka kwa nje, si kimoja, kama viwili. Hawakujua ni vitu gani, walihisi kulikuwa na kitu kumbe walinzi wao wawili waliokuwa wamesimama nje ya chumba hicho walipigwa risasi na wanaume wale ambao waliamua kuifanya kazi hiyo usiku huohuo.
Bilionea Massawe akashtukia kitu, harakaharaka akasimama na kwenda kuufungua mlango kwa ufunguo, hata kabla hajarudi kukaa kwenye kitanda, akashtuka kuona kitasa kikitekenywa kwa lengo la kufunguliwa.
“Who are you?” (wewe ni nani?) aliuliza Bilionea Massawe.
“Open the door,” (fungua mlango!)
“I ask you, who the hell are you?” (nimeuliza, wewe ni nani?) aliuliza Bilionea Massawe
Kila mtu ndani ya chumba hicho alikuwa akitetemeka, waliviona vifo vyao mbele yao, walitamani kukimbia lakini hakukuwa na sehemu nyingine ya kukimbilia zaidi ya kubaki ndani ya chumba hicho.
Wanaume waliokuwa nje ya chumba kile waliendelea kusisitiza kwamba wafunguliwe mlango lakini Bilionea Massawe na familia yake hawakutaka kabisa kuufungua hivyo watu hao kuanza kuuvunja.
Hawakutumia nguvu kubwa, mlango ukavunjika na kuingia ndani. Tina na mama yake walikuwa wakipiga kelele za kuomba msaada lakini hakukuwa na watu waliowasikia.
“Naombeni msituue,” alisema Bilionea Massawe huku akipiga magoti.
“Hilo utakwenda kumwambia Mungu! Sisi tumetumwa ni lazima tuzichukue roho zenu,” alisema mwanaume mmoja huku akikiweka vizuri kiwambo cha kuzuia mlio wa risasi kusikika.
“Tunaomba mtusamehe…” alisema Bilionea Massawe.
“Hilo ungemwambia Rais Salim Labad hata kabla hatujaingia ndani ya chumba hiki.
Hawakutaka maelezo zaidi, hawakutaka maswali walichokifanya kilikuwa ni kuwamiminia risasi watu hao, damu zikatapakaa chumbani, hawakuwaonea huruma hata kidogo, walikwenda ndani ya chumba hicho kwa kazi moja tu ya kufanya mauaji hivyo ilikuwa ni lazima kuhakikisha watu hao wanakufa kama walivyotakiwa kufa.
Walipomaliza, wakatoka nje ya chumba kile. Hakukuwa na mpangaji yeyote aliyetoka, walisikia mlango ukivunjwa, na walipotoka kwenye korido waliiona miili ya walinzi wakiwa chini huku damu zikiwatoka na hivyo kujua kwamba kulikuwa na hatari, wakajifungia vilivyo vyumbani mwao.
Wakatoka nje, hata kabla ya kuondoka, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Rais Labad na kumwambia kwamba kazi aliyokuwa amewatuma waliikamilisha kwa asilimia mia moja.
“Safi sana. Mmekumbuka kuimaliza na familia yake?” aliuliza rais kwenye simu.
“Ndiyo bosi!”
“Safi! Rudini mjini! Nilitaka nimalize kizazi chake chote, yaani watoto wake wasizae kuendeleza kizazi na ndiyo maana hata wao nilitaka muwamalize,” alisema Rais Labad huku sauti yake tu ikisikika kama mtu aliyekuwa na furaha tele.
“Watoto wake?”
“Ndiyo!”
“Kwani si ana mtoto mmoja wa kike?”
“Hapana! Anao wawili!”
“Mbona sisi tumemkuta mmoja?”
“Hapana! Wanatakiwa wawe wawili. Rudini ndani ya chumba mkamtafute na yeye mmuue,” aliagiza Rais Labad, harakaharaka vijana hao wakaanza kurudi ndani ya chumba hicho kwa ajili ya kumuua mtoto mmoja aliyebaki ambaye walikuwa na uhakika kwamba alikuwa chooni au chini ya uvungu wa kitanda amejificha.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa.