Mwalimu Macheyeki: Sheria Kandamizi Zinatishia Uhuru wa Habari nchini

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
HOTUBA YA WAZIRI KIVULI WA MAWASILIANO, TEKNOLOJIA YA HABARI NA UCHUKUZI ACT WAZALENDO MWL. PHILBERT MACHEYEKI KUHUSU MPANGO WA BAJETI YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024.

Utangulizi
Tukiwa katika mwendelezo wa kufuatilia Bunge la bajeti, juzi Ijumaa Mei 19, 2022, Ndg. Nape Moses Nnauye aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/23 na Mpango wa Makadrio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa Mwaka wa fedha 2023/24.

Wananchi na wadau wengine wa Sekta ya Habari na mawasiliano wanametoa maoni yao juu ya hotuba na vipaumbele vya wizara hii kutokana na ukweli kwamba katika zama tulizopo sekta ya Habari na mawasiliano ina mchango mkubwa sana katika Maisha ya mwananchi wa kawaida.

Aidha, wizara hii ndio yenye dhamana ya Usimamizi wa taasisi zinazoshughulikia masuala ya udhibiti, upatikanaji, biashara, uwezeshaji na usalama wa habari na mawasiliano. Majukumu haya yote kwa sehemu kubwa, yanategemea mpango wa bajeti ili kufanikishwa kwake.

Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya habari wa ACT Wazalendo Mwl. Philbert Macheyeki amefanya uchambuzi wa hotuba hii muhimu. Kutona na uchambuzi huo, tumeonyesha hoja saba (7) kuhusu vipaumbe, utekelezaji wa bajeti na mpango wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Hoja saba (7) za ACT Wazalendo kuhusu Hotuba ya Bajeti ya wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

1. Sheria kandamizi zinatishia Uhuru wa Habari nchini
Tangu Uhuru nchini Tanzania tasnia ya habari imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi zinatokana mfumo wa utamaduni kandamizi. Utamaduni kandamizi umepelekea Serikali kutunga sheria za habari zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa habari. Sheria hizo ni kama vile; Sheria ya Magazeti ya 1976, Sheria ya Usalama wa Taifa 1977, Sheria ya Mawasiliano ya kieletroniki na Posta 2010, Sheria za makosa ya kimtandao 2015 (Cybercrimes act 2015), Sheria ya takwimu 2015.

Katika miaka saba iliyopita, Tanzania imetunga sheria kadhaa zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, na zinazokazia ukali wa sheria zilizopo ambazo ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi.

Sheria ya kupata habari 2016, Kanuni za maudhui ya mtandaoni 2018, Sheria za makosa ya kimtandao 2015 (Cybercrimes act 2015) Kanuni za jumla za 2016, na Sheria ya Takwimu 2015 (pamoja na marekebisho yaliyofanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali) (Na. 3), 2018. Kwa pamoja, sheria hizi zinajinaisha uandishi wa habari za kina na za uchunguzi na zilikazia ukali wa sheria zilizopo ambazo ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi.

Katika taarifa ya utekelezaji wa bajeti mwaka 2022/23 Serikali imeeleza kuwa imeanza kufanya mapitio ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambapo muswada wa marekebisho ya Sheria hiyo umesomwa Bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Februari, 2023. Ingawa, Serikali imeonyesha nia ya kufanya mapitio kuna ushirikishwaji mdogo sana juu ya sheria hiyo. Aidha, bado zipo sheria nyingine kama tulivyozieleza hapo juu ni kandamizi kwa ustawi wa tasnia ya habari nchini.

Katika Ilani ya Uchaguzi ACT Wazalendo 2020 2(1) tulieleza namna ya kuhakikisha uhuru wa habari na haki ya kupata habari unavyopaswa kuzingatiwa kwa kufanya marekebisho ya sheria. “Serikali ya ACT Wazalendo, ndani ya MIEZI SITA ya kwanza itafuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya habari, na kutengeneza sheria, kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru na weledi na ukuaji wa sekta ya habari.”

Hivyo basi, tunaitaka Serikali kufuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya Habari na kutengeneza sheria mpya kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru na weledi na ukuaji wa sekta ya Habari.
Pili, tunaendelea kutoa wito kwa Serikali kusimamia uanzishwaji wa Baraza huru la habari nchini ili kulinda na kutetea haki na masilahi ya wanahabari.

Tatu, tunaitaka Serikali iongezwe ushirikishwaji katika mchakato wa mapitio ya Sheria ya huduma ya habari na muswada uliowasilishwa Bungeni mwezi Feb 2023 upelekwe kwa wadau na kujadiliwa kwa kina.

2. Usimamizi mbovu wa huduma ya mawasiliano na kupanda kwa bei za Vifurushi nchini.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ina wajibu wa kuratibu na kusimamia huduma za mawasiliano ya simu na intaneti zikiwemo; viwango vya uwekezaji, ubora na viwango wa huduma; gharama za huduma na uzalishaji na usambazaji (upatikanaji).

Kwa muda mrefu pamekuwepo malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu gharama za vifurushi na data. Mambo ambayo wananchi wamekuwa wakilalamikia ni pamoja na;

i. Kubadilika mara kwa mara kwa vifurushi vya data na muda wa maongezi,

ii. Vifurushi vya data kuisha bila mtumiaji kufanya matumizi yoyote,

iii.Kuisha kwa data tofauti na matumizi

iv. Kupanda kwa kasi kwa gharama za vifurushi vya data (kupunjwa kwa vifurushi hususani data na muda wa maongezi).

Serikali mara zote imekuwa ikitoa hoja za utetezi kwa watoa huduma kuhusu malalamiko ya wananchi badala ya kushughulikia na kutatua changamopto zao. Sekta ndogo ya habari na mawasiliano ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi kubwa zaidi hapa nchini inakua kwa asilimia 9.1%. Hii ni kwasababu Sekta hii inatumiwa na watu wengi katika masuala ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa. Aidha takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya huduma ya intaneti yanakua siku hadi siku hadi kufikia Mwezi Aprili 2023 watumiaji wa huduma za intaneti nchini ni Milioni 33.1 ongezeko la asilimia 10.7% kutoka mwaka 2022.

Katika mazingira ambayo sekta hii inakua kwa kasi hii bila kuratibu na kusimamia vizuri viwango vya huduma na gharama zake ni kuruhusu wananchi wako kunyonywa na kupitia mateso makubwa bila ungalizi. Ni kuwaacha wananchi bila ulinzi na inapoteza wajibu wa Serikali kwa watu wake.

Mathalani, gharama za za vifurushi kwa sasa hivi 1GB inanunuliwa kati ya Shilingi 2,500 hadi 3,000 na kasi ya kuishi kwake ni kubwa zaidi. Takwimu zinaonesha mtandao wa Facebook umetumia GB Milioni 48.99 kwa kipindi cha robo muhula tu, mpaka kufikia Machi 2023. Hoja za Serikali hazijibu wala kutatua changamoto hii kubwa kwa wananchi.

Mosi, tunaitaka Serikali kufanya marekebisho ya kanuni zinazosimamia vifurushi vya dakika za kupiga miongoni mwa mitandao ya nchini, bando ya intaneti na meseji. Kwa kuwashirikisha vya kutosha wananchi ili kuwezesha kudhibiti, uholela wa makampuni kuamua na kuwa na gharama nafuu.

Pili, Serikali ianzishe mchakato wa kutengeneza Upya sera Taifa ya mawasiliano kwa kuwashirikisha kikamilifu watoa huduma, watumia huduma, wataalamu wa masuala ya kimtandao na wadau wengine ili kama Taifa tuwe na sera inayoendana kasi ya ukuwaji wa teknolojia Duniani kwani sera sera ya taifa ya mawasiliano ya simu ya mwaka 1997 haiendani mahitaji ya wakati huu na sera ya taifa ya teknolojia ya habari na mawasiliano ya mwaka 2016 ambayo malalamiko haya ni kutokana na kugubikwa na changamotoSmbalimbali, ni lazima serikali iwe na meno.

Tatu, tunaitaka Serikali kuhakikisha inatoa huduma ya data bure maeneo yote ya umma kama vile hospitali, shuleni, vyuoni maofisinini na maeneo ya masoko.

Nne, Serikali ipunguze gharama za kikodi katika miundombinu ili mtumiaji apate nafuu katika kupata huduma. Mathalani kwa sasa gharama za kampuni kuunganisha mkongo kupitia pembezoni mwa barabara ni dola za kimarekani alfu moja ($ 1,000) sawa na Tsh Milioni 2.3 kwa kilometa moja wakati TANESCO wanalipa dola Tano ($ 5) sawa na Tsh 11,695 tu, kushusha kwa gharama hizi kutasaidia kupunguza gharama za miundombinu kwa watoa huduma hivyo kupunguza gaharama za huduma na kupunguza mzigo kwa wananchi. Kumudu gharama za mawasiliano.

3. Asilimi 31 ya Watanzania hawana mawasiliano na mtandao wa simu za mkononi.
Wakati serikali ikipiga mbiu ya kuhakikisha inaleta mageuzi ya kidigitali, tunaona kuwa kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano hususani kwa maeneo ya pembezoni ni ndogo sana. Kwa mujibu wa taarifa za uchambuzi wa wizara ya mwaka 2022 ambao umetumika katika Bajeti hii ya 2023/2024 ni kuwa asilimia 69 ya ardhi ya Tanzania (Geographical Coverage) imefikiwa na huduma ya mwasiliano ya simu za kiganjani ilinganishwa na asilimia 66 mwaka 2021.

Kwa maana nyingine kuwa sehemu ya wananchi kwa wastani wa asilimia 31 hawapati huduma ya mtandao wa simu. Aidha, takwimu zinaonyesha kuna Zaidi ya vijiji 2,212 vina changamoto ya mawasiliano nchini mpaka kufukia April 2023 ni vijiji 616 tu ndio vilifikiwa na huduma ya mawasiliano kwa kujegewa minara kwa mwaka wa fedha uliokwisha, kasi hii ya kupeleka mawasiliano vijijini ni ndogo mno.

Aidha, yapo maeneo mengi ya mipakani na baadhi ya Halmashauri hazipati kabisa huduma za matangazo ya Redio ya TBC au Televisheni mpaka sasa kuna wilaya 12 hazina usikivu wa uhakika wa redio (Mafinga, Pangani, Ikungi, Mkalama, Bukombe, Tabora (v), Simanjiro, Malinyi, Mafia, Sumbawanga (V) Kishapu na Biharamulo) Hali huwa ni tofautu kwa maeneo ya mipakani mara nyingi wanasikiliza Redio za nchi jirani. Inasikitisha katika miaka sitini ya uhuru wa nchi yetu, wapo wananchi ambao wameachwa nyuma kiasi cha kutokuwa na uwezo wa kupata Habari aidha kwa simu au redio ama televisheni.

Changamoto hizi, humalizwa kwa serikali kuamua kuwekeza kwa kutenga fungu la fedha za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano vijijini ni wa uhakika.
ACT Wazalendo, tunatoa rai kwa Serikali katika mwaka huu na miaka ijayo ihakikishe Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unatengewa fedha za kutosha ili kuimarisha mtandao wa mawasiliano nchini.

4. Wizi wa simu, utapeli wa kimtandao na simu za kilaghai ndani nchi.
Sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania hasa wa mijini wamekua wakiitumia katika kufanya, kufanya biashara mtandaoni, kuagiza na mizigo kutoka nje ya nchi, kufanya miamala, kupata huduma mbalimbali zikiwemo za Serikali kupitia mfumo wa huduma za Serikali kidigitali.

Kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuhusu uwajibikaji mdogo wa serikali katika kushughulikia matukio yanayoripotiwa kuhusu wizi wa simu, utapeli wa kimtandao, na jumbe la kilaghai. Pamoja na Serikali katika bajeti za kila mwaka ikiomba kutengewa fedha kwa ajili ya kuimarisha Mfumo utakaowezesha kuzuia matumizi ya simu zilizoripotiwa kuibiwa, kupotea, kufanya ulaghai au kuharibika pamoja na kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango.

Serikali inataja takwimu kuwa katika kipindi kinachoishia tarehe 30 Aprili, 2023, jumla ya namba tambulishi 92,643 za vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki vilifungiwa baada ya kubainika kuhusika kwenye vitendo vya udanganyifu, wizi au kupotea. Lakini uhalisia ni kuwa wananchi wengi wanakutwa na matatizo ya kimtandao lakini jeshi la polisi linashindwa kutumia mifumo kwa haraka kunusuru dhulma na upotevu badala yake inataka kuongeza maumivu kwa wananchi kwa kuwataka walipia gharama za kufuatilia.

ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuhakikisha inashughulikia kwa wakati taarifa za wananchi kutapeliwa, kuibiwa na kulaghaiwa. Na, ifute tozo zinazowekwa kama gharama za kufanya uchunguzi.

5. Kasi ndogo ya Mradi wa vifaa vya TEHAMA na kuunganisha shule na mtandao wa intaneti
Serikali kupitia USCAF ilipanga kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za Umma 150 ambapo kila shule ilipangwa kupelekewa Kompyuta 5, Printa Moja na Projekta moja mpaka kufikia Aprili 2023 hakuna shule hata moja imepewa vifaa hivyo bado vifaa vipo kwenye hatua ya manunuzi. Tanzania kwa mujibu wa Sensa ya watuna Makazi yam waka 2022 ina jumla ya Shule za msingi 19,769 ambapo shule 19,266 zipo Tanzania Bara, Shule za Sekondari zipo 5,857 kati ya hizo sekondari 5,592 zipo Tanzania Bara na Sekondari 265 zipo Zanzibar.

Katika bajeti ya mwaka 2021/22 Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilisema itaenda kutekeleza mradi wa kuunganisha mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule za umma 151. Kwa kila shule ni kompyuta 5 na printa 1. Na wamefanikiwa kuziunganisha na intaneti shule 100.

Katika mwaka 2022/23 serikali imesema itatekeleza Mradi kwenye shule 150 na mpaka leo hakuna hata shule moja iliyopewa vifaa hivyona Wizara katika mwaka wa Fedha 2023/2024 inapanga kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 160 na Shule 6 za watoto wenye mahitaji maalum kwa kutumia Takwimu hizi na Mwenendo huu wa miaka takribani tatu. Nidhahiri kuwa itachukua miaka 150 ili kuweza kuziunganisha shule 25,626 sekondari na msingi zilizopo nchini.

Ni rai yetu ACT Wazalendo, kuwa Serikali isifanye jambo hii kama ni hisani kwa wanafunzi badala yake ichukuliwe kuwa ni tehama katika shule zetu ni nyenzo muhimu katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishajihivyo tunataka hatua za kibajeti ili kuhakikisha angalau kila mwaka shule miatano zinafikiwa na huduma ya kuunganishwa na intaneti na kupatiwa vifaa muhimu vya TEHAMA ili kuendana na maendeleo ya Dunia ya sasa.

6. Usalama na ulinzi wa taarifa za kimtandao kwa watumiaji.
Katika kuendea dhana ya Tanzania ya kidijitali ni muhimu kuweka mikaka dhabiti juu ya usalama wa kimtandao kwa wananchi wanaotumika mitandao. Pamoja na kujenga miundombinu ya Teknolojia ya habari kulinda taarifa (privacy) za watumiaji.

Tunatambua zilikuwepo jitihada za kuwa na sheria ya kulinda taarifa za watumiaji ili zisiweze kuibwa kwa ajili ya makampuni mbalimbali dunia. Tunaamini kuwepo kwa sheria ya Ulinzi wa taarifa (Data Protection) ni kuhakikisha usalama na usiri wa taarifa zinazotembea katika mtandao na kuzuia udukuzi wa aina yoyote na kwa hivyo kulinda na kuimarisha utayari wa biashara kupitia kwenye mtandao kwa mfano biashara ya fedha na kuifungua nchi kilimwengu zaidi.

ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Sheria hii itizame kwa makini namna ya kubeba Teknolojia ya kisasa za kubeba, kutunza na kusafisirisha data kama vile sayansi ya Blockchain ambayo ndio ufunguo mkuu wa biashara ya kutunza taarifa na kusafirisha fedha kwa usalama na kwa uhakika na hivyo kuvutia kustawi kwa eneo hilo hata Tanzania ikikusudia kuingia biashara za eneo hilo.

Aidha, tunapendekeza kuwa serikali ifanye tathmini na uchambuzi mara kwa mara wa vihatarishi vya usalama katika mtandao na mifumo ya kompyuta kwa lengo la kubaini mapungufu yaliyopo dhidi ya mashambulio ya mtandao (cyber-attacks).

7. Usimamizi mbovu wa Mashirika yaliyo chini ya Wizara
Katika ukaguzi wa Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) umedhihirisha kuwa kuna mapungufu makubwa ya kiusimamizi wa Wizara kwa taasisi zilizochini yake, hii inapelekea hasara kubwa kwa taifa, ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi na kuchochea ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma na ufisadi tumechukua mashirika mfano wa mashirika ni kama

(a) Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL)
i. Shirika kushindwa kufikia malengo Shirika la Mawasiliano Tanzania limekumbana na changamoto kadhaa katika kufikia malengo yake ya kimkakati. Shirika la Mawasiliano (kanda ya kati ya Dar es salaam) limeshindwa kufikia malengo ya kupata wateja 112,324 sawa na asilimia 73 ya lengo lililowekwa na shirika la kutakiwa kufikia wateja 152,950 kutokana na ukwasi.

ii. Uongozi wa TTCL kutowatambua wadaiwa wao, ambapo CAG amesema alibaini kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania lilikuwa na madeni makubwa yenye thamani ya shilingi bilioni 21 ambayo uongozi haukuweza kutambua wadaiwa husika, katika kiasi hiki Shirika la Mawasiliano Tanzania lilitoa mapendekezo kwa Bodi ya Shirika kufuta deni la shilingi bilioni 7.51. bila kuomba kibali kwa msajili wa hazina.

iii. Mapungufu katika miradi Katika Shirika la Mwasiliano Tanzania, kulikuwa na miradi 464 iliyokamilika yenye thamani ya shilingi bilioni 10.33 ambayo haikufungwa kutokana na ufatiliaji usioridhisha na kuchelewa kuwasilishwa kwa nyaraka muhimu toka kwa mameneja wa miradi. Hii inaleta hatari ya matumizi mabaya ya fedha kutokana na uwezekano wa kutokuwepo kwa miradi hiyo.

(b) Kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN)
CAG amebaini kampuni hii imeendesha zabuni kinyume na sharia ya Zabuni kifungu cha 4A (1) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410. Yenye thamani ya shilingi shilingi bilioni 7.49 na dola za Marekani 48,480 hali inayosababisha hofu juu ya uadilifu, ushindani, uwajibikaji, uchumi, ufanisi, uwazi na kufikia thamani ya fedha. Na inaacha mwanya wa Ubadhilifu na Ufisadi.

(c) Barazala Ushauri la Watumiaji wa Huduma za mawasiliano Tanzaniani (TCRA CCC)
Mpaka kufikia wakati wa ukaguzi baraza hili halikua na Bodi ya wakurugenzi ambapo mara ya mwisho kuwa na Bodi ni novemba 2021. Usimamizi mbovu unapelekea kuonekana mashirika ya Umma hayafanyi vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake, baadhi ya watu wakiwepo viongozi wakubwa kwasababu hiyo wamekua na mawazo ya kubinafsisha mashirika hayo, mawazo ya namna hiyo yanatoa hofu kwa Umma kuwa watendaji hawatekelezi majukumu yao ipasavyo ili kuyahujumu na kutaka kubinafsishwa.

ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali kujidhatiti katika kusimamia mashirikia yote ipasavyo na kuwachukulia hatua watumishi wote wanaokwamisha ufanisi na kuleta hasara kwa mashkirika hayo. Kwa kuunda kikosi kazi maalumu (taskforce) ya ufuatiliaji wa kina juu ya masuala yote yaliyoibuliwa na CAG na kujua chanzo chake ili yarekebishwe maramoja.

Hitimisho.
Tunaendelea kufuatilia mienendo ya Wizara hii muhimu nchini na kuyafanyia kazi masuala mbalimbali ya kisera na kisheria ikiwa ni mwendelezo wetu wa kutoa mapendekezo kwa ajili ya maendeleo ya Kisekta. Hata hivyo Kutokana na Sintofahamu ya Uendeshaji wa zoezi la Anuani ya watu na makazi ambao unaendelea kwa makazi Milioni 12 kupewa Anuani, Sisi Tunataka ufanyike Ukaguzi Maalum katika Utekelezaji wa Mradi (Operesheni) huu Ili kuona matumizi na malipo ya utekelezaji wa Mradi huu Muhimu.

Hata hivyo, Katika kuelekea kwenye mabadiliko makubwa ya kidijitali mchango wa sekta ya habari ni mkubwa sana. Kwahiyo, ipo haja kwa serikali kuwekeza vya kutosha ili kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inakuwa vizuri ili kuboresha na kuimarisha uchumi wetu. Pia, sekta ya habari katika mukta wa kitanzania inakabiliwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti wa kidola.

Sheria, kanuni na taratibu nyingi zilizopo tumerithi maudhui ya kikoloni katika kuitazama sekta ya habari na uhusiano wake na dola. Kwahiyo, sura na sifa za dola na silka za mtawala wa wakati huo ndio zinaakisi sheria na Mwenendo wa vyombo vya habari na tasniaya habari kwa ujumla. Uelekeo wa namna hii, hauleti afya katika jamii ya watu huru na sekta yenyewe. Hivyo basi, sasa ni wakati sahihi wa kufanya mabadiliko ya mifumo ya sheria na kanuni zote zenye sura na sifa ya ukandamizaji (kikaburu na kikoloni).


Mwl. Philbert Macheyeki
Twiiter: @PMacheyeki
Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi
ACT Wazalendo
21 Mei, 2023
 
Back
Top Bottom