Mwakyembe apeleka 'tsunami kuu' Bandari

armanisankara

JF-Expert Member
Jul 15, 2011
283
49
mwakyembe(11).jpg

Waziri wa Uchukuzi Dk. Harison Mwakyembe akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua yake ya kuwasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Manaibu wake wawili na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zinazowakabili.


Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameifumua Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu, Ephraem Mgawe, na mabosi wengine sita kufuatia ufisadi wa kutisha unaodaiwa unaofanyika kwenye mamlaka hiyo.

Wengine waliosimamishwa ni manaibu wakurugenzi wawili wa TPA ambao ni Julius Mfuko (Maendeleo ya Miundombinu), Hamad Kashuma (Huduma), Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng’amilo na mameneja wawili wa Bohari ya Mafuta Kurasini Oil Jetty (KOJ) pamoja na mhandisi wa bohari hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe alisema mabosi hao wa TPA wamesimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazoukabili uongozi wa bandari ikiwemo wizi wa makontena, wizi mkubwa wa mafuta, udokozi wa mizigo na rushwa katika utoaji wa huduma.

Waziri Mwakyembe alisema kumekuwa na wizi usioisha bandarini kiasi cha kutishia uhai wake kwa kuwa unafukuza wateja ambao wamehamia bandari za Mombasa nchini Kenya na Durban nchini Afrika Kusini ambako hakuna kero hizo.
Alisema kero nyingine ni uzembe wa utoaji huduma pamoja na foleni ndefu ya meli zinazosubiri kushusha mizigo, jambo ambalo pia ni kero kubwa kwa wafanyabiashara.

“Utendaji huu umepunguza imani ya wananchi na imekuwa kero sana kwa wafanyabiashara, itakuwa ni makosa makubwa tukiacha hali hii iendelee kwa mategemeo kwamba itaisha yenyewe,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema: “Hata ukiweka ulinzi wa askari 20 kwenye kontena moja pale bandarini bado litaibwa...hali hii ni mbaya na imefukuza wafanyabiashara wa Rwanda, DRC na Malawi ambao wametukimbia na kwenda Mombasa na Durban Afrika Kusini.”

Dk. Mwakyembe pia amepiga marufuku malipo ya fedha taslimu kwa huduma za bandari kwa kuwa mfumo huo unachochea rushwa na hivyo ameagiza malipo yafanyike benki kulipia huduma zozote za bandari.

Alisema ameagiza matumizi ya mfumo wa benki au mwingine wa teknohama kama kadi uanze mara moja ili kuvunja mtandao wa kisanii wa kudai rushwa na kuiibia TPA.

Alisema atakayekiuka utaratibu huo mpya atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu.

Kadhalika, Dk. Mwakyembe alisema TPA ina matatizo ya mfumo wa kiutendaji inayosababisha ‘vurugu’ katika uwajibikaji na utendaji hasa kwa kuwa na mamlaka mbili za manunuzi na kumpa madaraka makubwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema meneja huyo amekuwa na nguvu kuliko hata wakurugenzi wa TPA, jambo linaloleta shida katika uwajibikaji. Alisema: “Hivyo nimeiagiza bodi iondoe hiyo vurugu kwa kuangalia upya utendaji huo.”

Akizungumzia KOJ, alisema kwa kipindi kirefu katika Bandari ya Dar es Salaam kumekuwa na wizi mkubwa wa mafuta unaofanyika kila siku kwa kisingizio cha kutoa mafuta machafu bandarini.

Alisema upotevu wa mafuta kutoka kwenye meli hadi kwenye bomba linaloyapokea kwa ajili ya kuyapeleka kwenye matangi ni asilimia mbili, kiasi alichosema ni kikubwa na ni biashara ya wajanja wachache.

“Tumefuatilia hayo yanayoitwa mafuta machafu tukakuta kwamba yanaishia vituo vya mafuta, nimechukua sampuli ya mafuta hayo na nimezipeleka Mombasa na Ewura ili wapime tujue kama kweli ni machafu,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema katika ziara yake ya kushtukiza bandarini hapo alibaini kwamba kampuni hiyo inaeleza kutoa mafuta machafu lita 9,000, lakini ikiwa na mafuta masafi lita 26,000 ambayo yanawekwa rangi kidogo ili yaonekane ni machafu.

Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela (CCM), mkoani Mbeya alisema tatizo la kutokuwepo kwa mita za mafuta kunachangia serikali kutojua kiasi cha mafuta kinachoingia nchini hiyo ameiagiza TPA kuzinunua haraka iwezekanavyo na zipatikane ndani ya mwezi mmoja.

“Nimeiambia TPA ishirikiane na wakala wa serikali wa vipimo na mita hizo zirejeshwe ndani ya mwezi mmoja kwa gharama yoyote, lakini sijawaambia wasizingatie sheria ya manunuzi...bandari haiwezi kuiweka nchi rehani,” alisema.

KAMPUNI YA SINGARIMO

Kuhusu kampuni ya Singarimo inayotoa mafuta machafu bandarini, Dk. Mwakyembe alisema zabuni yake imekwisha muda wake na TPA ilikwisha kutangaza nyingine, lakini katika hali ya kushangaza walioshinda hawajapewa taarifa.

“Kwa sasa kampuni hii inachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na Ewura kwa maelekezo ya waziri (yeye Mwakyembe) kwa hiyo nimeiagiza bodi ya wakurugenzi wa TPA kuisimamisha kazi mara moja na aitwe mzabuni aliyeshinda,” alisema.

Alisema tangu mwaka 2008, Ikulu ilielekeza kwa maandishi kwamba Singarimo haifai na kisha Wizara iliiagiza TPA kuachana na kampuni hiyo kwa kuwa haikuwa inafaa kufanyakazi hiyo, lakini katika hali ya kushangaza Mamlaka ya Bandari ilikaidi maagizo hayo.

“Ni kampuni ya viongozi na watendaji ndani ya TPA, ndiyo maana kila mwaka yenyewe inashinda tenda (zabuni), huu ni mgongano wa kimaslahi ambao ni kinyume kabisa cha sheria ya bandari,” alisema.

MKATABA WA TICTS UPITIWE

Akizungumzia kampuni ya kupakua na kupakia makontena bandarini (Ticts), Dk. Mwakyembe alisema ameiagiza idara ya sheria ya TPA kupitia na kuchambua kifungu kwa kifungu mkataba wa kampuni hiyo ili kubaini kama unatekelezwa kama ulivyokubaliwa.

“Kuna wizi wa kutisha wa makontena bandarini, hivyo nimeagiZa ripoti ya uchambuzi wa mkataba huo niipate mezani kwangu Jumatano ijayo,” alisema.

HATUA KWA WALIOSIMAMISHWA

“Kutokana na kasoro za kiutendaji nimeunda kamati ya watu saba kuchunguza wakurugenzi wa TPA, nimewapa hadidu za rejea zenye maswali 50, kazi hii nimeagiza ifanyike kwa siku 14, hawa wamesimamishwa kupisha uchunguzi,” alisema.

Alisema ameiagiza bodi ya TPA kuteua watu wazalendo na waadilifu kukaimu nafasi zilizoachwa wazi.

Hata hivyo, Dk. Mwakyembe amemteua Madeni Juma Kipande kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA kuanzia jana. Kabla ya uteuzi huo, Kipande alikuwa Wizara ya Ujenzi.

Dk. Mwakyembe alisema maelekezo aliyoyatoa kwa TPA yanaanza mara moja na kwamba ambao hawatatekeleza atajua ni hujuma ambazo hawezi kuzivumilia.

Juni 5, mwaka huu, Dk. Mwakyembe alimsimamisha kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi, baada ya kubaini kwamba utaratibu wa uteuzi wake haukufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Viongozi wengine aliowasimamisha ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Uhandisi, John Ringo, Mwanasheria Amini Mzaray, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Justus Bashara na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Josephat Kagirwa.

Baada ya kusimamishwa kwa vigogo hao wa ATCL, Dk. Mwakyembe aliunda kamati ya wajumbe watatu wenye uelewa wa mambo ya fedha na sheria ili kuchunguza matumizi ya fedha iliyokuwa imepokelewa kuanzia mwanzoni mwa Mei, mwaka huu.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom