X-PASTER
JF-Expert Member
- Feb 12, 2007
- 11,604
- 1,848
Mwaka Mpya Na Miungu Ya Kisiasa
Watu wengi wana tabia ya kusheherekea siku ya kuingia mwaka mpya, wengi upatwa na furaha na kuingiwa na kiwewe cha kuiona siku na mwaka mpya, kwa kujiona kuwa wamefaulu kuuona mwaka mwingine. Lakini wanasahau kuwa miaka inakwenda, na umri ndio unapungua.
Binadamu anapopitisha miaka yake hana maana kuwa ana furaha bali ahesabu kuwa siku zake zinazidi kupungua na kukaribia kuingia kaburini, kwa hiyo iwe ni masikitiko na sio furaha khaswa kwa yule ambaye hakujishughulisha kufanya mambo mazuri kwa jamii yake!
Miaka itakuwa ni ya kufaulu pindi ikiwa siku zimetumika kwa mambo mazuri na yalio leta faida kwa jamii yake na yake binafsi bila ya kuwaathiri wengine kiufisadi na itakuwa ni ya huzuni ikiwa miaka hiyo itatumika kwa ufisadi au kuachia ufisadii ukitendeka bila ya yeye kuchukuwa hatua za kudhibiti ufisadi huo.
Watu wengi upendelea kuweka maazimio (resolution) yaani kuweka lengo au malengo atakayoyafanya katika mwaka huo mpya, nayo yote ni mambo mazuri, lakini Mtu makini hawezi kufanya hayo ya kuweka lengo lake au malengo yake kila mwaka tu, bali uweka malengo kila siku, na juu ya hivyo sio lengo au malengo ya kipuuzi bali ni malengo ya kujirekebisha kuwa bora kuliko siku iliyopita.
Siku zinatupita, masaa yanatupita na hali za watu wengi hazibadiliki kuwa bora kwa sababu wengi wetu tumejiweka mbali na harakati za kujikomboa.
Wengi wetu tumekalia siasa za maji taka, kuchafuana, udini, ukanda na uchama ndio tumeweka mbele, lakini tunasahau kuwa wenye maisha bora ni hao wanasiasa ambao kila kukicha tunawatetea na kuwakumbati na kuwaona ndio mitume na miungu watu!
Mfano mdogo tu, hivi ni wangapi ambao wamepinga posho za wabunge zilizo ongezwa hivi karibuni? Kwanini zisiongezwe posho za Walimu, madaktari, manesi na wafanyakazi wa kima cha chini?
Kwanini Wabunge na si raiya wa kawaida... Kwanini hizo posho zisitumike kununulia vifaa vya mahospitalini, kama hazitoshi kwanini zisinunue madawati kwenye mashule au kwanini wasipewe wale wagonjwa wasio weza kujilipia matibabu na madawa wanayo andikiwa uko mahospitalini, kwa nini wao tu?
Ni wagonjwa wangapi wanakosa dawa uko mahospitalini na hali hao viongozi wa kisiasa wakiumwa mafua wanapanda zao ndege na kuelekea Ughaibuni kutibiwa na wakirudi hapa wanasifia mahospitali ya wenzetu, na hali wanaona za kwao hazina hadhi na hata hawashtuki. Na sisi raiya wa kawaida hata hatuhoji wala kushtuka kuwa hayo wanayo yafanya viongozi wa kisiasa ni dhurma kwa raiya. Ni sawa na baba mwenye kuacha familia yake ikifa kwa njaa na yeye anakwenda kula hotelini, na akirudi familia nzima inamshangilia kuwa baba karudi na ameshiba vema. Hakika familia ya namna hii itakuwa na ugojwa wa akili si bure.
Labda niseme tabia moja, tabia ambayo Watanzania wengi kama si nchi nyingi zinazoitwa dunia ya tatu tumeikumbatia, kiasi ya kututia upofu wa akili. Tanzania ni nchi ambayo waasisi wake wameibatiza kuwa ni nchi yenye kufuata misingi ya kijamaa, wengi tunaelewa kuwa nchi nyingi zinazofuata siasa za ujamaa zilikuwa ni nchi zilizotawaliwa na mfumo wa chama kimoja. Na kwa kuwafumba wananchi macho, tuliambiwa kuwa tuna demokrasia ya chama kimoja. Ndani ya mfumo huu chama tawala kiliinuliwa juu na kuchukua nafasi ya Mungu wa taifa.
Ili kuhami nafasi hiyo, hapo ndipo zilipobuniwa semi au slogan za kudai chama na serikali havina dini. Wenye dini wako huru na dini zao, wenye taaluma wabakie na taaluma zao, wanawake wabakie jikoni, wanafunzi wabakie darasani, wafanyibiashara wabakie madukani mwao, wafanya kazi wawe huru na kazi zao na wakulima nao wabakie mashambani mwao, vijana ni taifa la kesho kwa hiyo wasijihusishe na siasa.
Siasa ikabakia kuwa eneo nyeti na haki ya kundi dogo lililojifanya kama ndio wateule katika nchi na kwa sababu ya uteule wao basi hawapaswi kuchukuliwa hatua za kisheria wanapokuwa wametenda makosa ya jinai.
Kwa kitambo watawala waliufaidi uhuru huo kwa sababu ulikuwa ni uhuru wa kufanya maovu pasipo kupingwa, huku wakiwa wamewaengua na kuwatenga kabisa wananchi wengine wasishiriki kwenye maamuzi muhimu ya kisiasa. Kwa kifupi ukawako utawala wa wachache, lakini utawala wao ukawa hauna mipaka na kwa hiyo wakawa na uhuru wa kuharibu kama wapendavyo pasipo kizuizi chochote. Na kama ilitokea mwanasiasa mmoja kwenda kinyume na wenzake, basi walimuondoa haraka sana, na kumpachika majina mabaya mabaya.
Utawala wa hao wachache ulienda sambamba na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Sheria mbaya kama za kumweka mtu kizuizini pasipo hata kumfikisha mahakamani zikatungwa kwa makusudi ya kupambana na wale watakao thubutu kuleta upinzani.
Watawala walikosa imani na mahakama kwamba zinaweza kutoa haki wanayoitaka wao ndiyo maana walikimbilia vizuizi kama kwamba hiyo ndiyo dawa pekee ya kuleta umoja wa kitaifa.
Katika maeneo mengine ya maisha zaidi ya eneo la siasa pia kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa haki za watu kwa mfano katika eneo la uchumi serikali ndiyo iliyopanga bei za mazao ya wakulima, ndiyo iliyopanga viwango vya mishahara, na pia ndiyo iliyopanga viwango vya bei za vitu pasipo kujali uzalishaji wala nguvu za soko. Sheria nyingi za ukandamizaji zilipitishwa na Bunge la chama kimoja, huku viongozi wa chama na serikali wakijigeuza miungu.
Wananchi katika ujumla wao walishirikishwa kwenye siasa kama wateja tu wa kununua hicho ambacho wanasiasa wamekitengeneza katika mipango yao kila walichokipika.
Watu walishirikishwa kwenye maandamano ya kuunga mkono maamuzi ya serikali au chama, lakini wale wachache wenye kuelewa mara walipothubutu kufanya maandamano yao kudai hiki au kile, ama maandamano ya kuelezea hisia zao, ilidaiwa ni maandamano haramu na waandamanaji walipata vipigo vya mbwa mwizi.
Hali hii inaendelea mpaka leo, hakuna hata mwanasiasa au mbunge mmoja ambaye amethubutu, kuwauliza wananchi wake walio mchagua ni nini wanataka akipeleke bungeni. Na hao wanaojaribu kuhoji vyama vyao, wamebandikwa lebo ya waasi au wenye kutaka kuleta machafuko kwenye vyama husika.
Watu wanashirikishwa kufanya neno lile ambalo chama kinataka lifanyike, lakini yanayohusu uendeshaji imekuwa ni mwiko. Siasa imebakia eneo maalum kwa ajili ya watu maalum. Kwa namna inayofanana na mchezo wa kuigiza, eneo la siasa linafanywa kama eneo takatifu na wote walioko ndani yake wanahesabiwa kama ni watakatifu, na ndio sasa hatuoni wapenzi wa vyama vya kisiasa wakiwahoji viongozi wao kwa kila jambo linalopita kwenye vyama vyao au uko bungeni. Na ndio miaka nenda rudi, ni wale wale tu, yaani hakuna kustaafu.
Tanzania kuna pengo kubwa sana kati ya wanasiasa na wananchi, yaani vyama vimetekwa na wanasiasa wachache, miaka nenda rudi. Vyama vyote vinatenda mambo yake kama vyama vya kidola au vyama vya kiserikali vya enzi ya ujamaa (Ukomunisti). Kauli zote za vyama vikiwemo vyama vyote vya siasa vikiongozwa na chama tawala, ni vyama vyenye kutoa kauli za kibabe dhidi ya wananchama wake wa kawaida, na kauli hizo wala siyo kauli za wananchi. Kwa ufupi wananchi wamefumbwa vinywa na wanalazimika kuishi kwenye kibano na kabali ya vyama vyao au dola.
Sambamba na hilo wasomi na wanataaluma nao wanakandamizwa kwa kulazimishwa kuwa chini ya uongozi na utawala wa mambumbumbu wa wanasiasa, ili tu kuhakikisha taaluma zao hazi-operate kwa uhuru.
Kutokana na hali hiyo ya viongozi kujifanya miungu na kuchukua nafasi ya Mungu wa taifa ambao ni raiya wa kawaida, basi inatakiwa ili Mungu wa kweli aweze kuchukua nafasi yake, inapaswa, na kwa hakika ilibidi mifumo ya aina hii ianguke, isambaratike, na kutokomea kabisa. Lakini wanasiasa wanajuwa kucheza mchezo wao, wamekuja na slogan ya neno mageuzi.
Yaani wametubana kweli kweli, tena kila kona, hata uko kwenye mageuzi tunakotaka kwenda tutakuwa nao tu. Wengi tunaamimini kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu, neno ili laweza kuwa na ukweli ndani yake au ikawa si kweli, inategemea na tafasiri ya mtumiaji. Lakini kwa wale wenye kuiamini hiyo kauli ukiangalia kwa undani yaani kwa jicho la rohoni utaona ya kwamba mageuzi ya kusambaratisha mifumo dhalimu hayakutoka kwa shetani bali yametoka kwa Mungu, kwani shetani hawezi kupigana na mifumo yake mwenyewe.
Uko mashariki ya kati tunashuhudia wananchi wakiingia mitaani kudai haki zao za msingi, na yote hayo ni kwa sababu za wanasiasa uchwala ndio walioshika vyama tunavyo vishabikia.
Bwana Yesu katika kuuelezea utawala wa Mungu, aliufananisha na upepo kisha akasema upepo huvuma kwenda kule utakako wala hatuwezi kuuzuia lakini sauti yake twaisikia.
Katika tafsiri halisi upepo au kimbunga kilichoiitikisa mifumo ya mataifa mbali mbali ya dunia ndani yake kuna nguvu ya Mungu, ndiyo maana watawala pamoja na ujanja wao, ubabe wao, na nguvu zao za kidola hawakuweza kuzuia wala kuzima wimbi la mageuzi.
Sehemu nyingine ya mafundisho yake, Bwana Yesu alisema yule mtu mwenye kulishika neno langu atafanana na mjenzi mwenye busara ambaye alijenga nyumba yake juu ya mwamba, hata upepo wenye nguvu ukaja ukaipiga nyumba ile lakini isitikisike, kwa sababu ilijengwa juu ya msingi imara, bali mwenye kuyapuuza maneno haya ni sawa na mjenzi mpumbavu ambaye alijenga nyumba yake juu ya mchanga, upepo wenye nguvu ulipokuja ukaipiga nyumba ile nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.
Ingawaje watawala wanajitahidi sana kuficha, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba taifa letu halikujengwa juu ya mwamba imara ambao ni katiba iliyokubaliwa na wananchi wote badala yake nchi imejengwa juu ya maneno ya wanasiasa wachache, ambao wameingiza maneno ya kipuuzi, maneno yasiyokuwa na ukweli wala umakini wowote na baya zaidi nchi imejengwa katika misingi ya ushirikina na imani isiyoeleweka kama ni imani ya Mungu au imani ya shetani. Ndiyo maana nasema wote wenye kumcha Mungu (Waislam, Wakristo, Wenye dini za jadi) tusiukubali tena upumbavu wa kusema tusichanganye dini na siasa kwani huo ni uwongo, hawa wanasiasa wamekuwa kama mashetani ambayo kila kukicha wanatutenganisha na ukweli halisi wa maisha yetu.
Mimi binafsi naami kwa kutumia imani zetu, tunaweza kuwachaguwa wanasiasa wa kweli wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na si wenye kuogopa thamani ya vyeo vyao.
Kuogopa uku thamani ya vyeo vyao, ndio kunawapelekea kuwa waongo, mafisadi na kupapia mali kwa sababu wanachuma ili kujiwekea ngome ambazo zitawalinda kesho na kesho kutwa. Na hata pale wananchi tukija kushtuka usingizini tutakuwa tumekwisha chelewa na wao wamesha jijengea himaya yenye nguvu kubwa kiasi ya kutoweza tena kutetereka.
Enzi za ujamaa tulielezwa kwamba ujamaa ni imani hauna budi kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake. Imani iliyo elezwa katika ujamaa ule haikuelezwa wazi nini tofauti yake na imani za dini, wala haikuelezwa kwamba mhusika ama huyo mwananchi auamini ujamaa kwa kutumia nini. Je kwa kutumia akili yake, au mwili wake ili asije akachanganya imani ya ujamaa, na imani ya dini yake kama ni Uislamu, Ukristo, Uhindu au dini za jadi!
Wanasiasa kwa vinywa vyao wanahubiri dini isichanganywe na siasa yao lakini katika uhalisi wa mambo na kwa matendo yao wao wanachanganya siasa yao na dini yao ya ufisadi.
Kisha kwa ujanja wanasema siasa zetu si sawa na siasa za mataifa mengine, wametutengenezea mkorogo wa kuchanganya imani ya kisiasa na imani ya kidini kidogo, kutokana na ukweli kwamba mtu asingeweza kuigawa imani yake iliyoko rohoni mwake kwenye matabaka mawili yaani awe na imani kwa ajili ya siasa, na imani nyingine kwa ajili ya dini.
Wengi tumewaona wakitumia vifungu kutoka vitabu vya dini, pale tu wanapo ona maslahi yao yapo hatarini, na kukemea udini pale viongozi wa dini wanapowakemea na kuwataka kuwa wasichanganye dini na siasa.
Watanzania tumeishi katika udanganyifu huu kwa miaka mingi huku wanasiasa waongo wakitaka tuyaamini maneno yao kama vile tunavyoliamini neno la Mungu, mbaya zaidi wakaufanya uwongo wao (ambacho ni kitu cha binafsi) uwe ni sehemu ya siasa hadi watu wengine wakafikia kusema siasa ni uwongo.
Hadi leo hii wengi wanaamini hivyo kwamba siasa ni uwongo na ndiyo maana hawataki siasa ichanganywe na dini lakini hiyo ni imani na misimamo yao potofu kwani siasa kama ulivyo uchumi, biashara, na sayansi nyingine yoyote ile inataka ukweli na uaminifu, kitu ambacho wanasiasa wetu hawana. Kwa sababu hawafuati kile kinachokatazwa na dini zao, zikiwa za kiislamu, kikristo au hata dini za jadi.
Kwa sababu dini zote hizo zinakataza wizi, ufisadi na uongo, na zinaimiza tutendeane mema na kupendana. Sasa kwa wanasiasa kwa kutumia mbinu zao wameweza kutushawishi kiasi ya kwamba tukiwabada kwa mujibu wa dini zao, wanatubana kwa kutuambia kuwa tusichanganye dini na siasa.
Basi mwaka huu wa 2012 uwe mwaka wa maazimio ya mabadiliko ya kila Mtanzania, maana tukiwaachia wanasiasa, na kuendekeza ushabiki usio na maana, hatutakuja ona mabadiriko hata baada ya miaka 100 ijayo.
Mafunzo ya dini yanasema, ukiona jambo baya liondowe kwa mkono wako, kama huwezi basi lisemee watu wasikie kama hili baya, Jambo la mwisho kama hayo yote uwezi basi angalau lichukie kwenye moyo wako na hili la kuchukia ni katika Imani dhaifu sana isiyotakiwa na Mungu.
Na kuna kauli moja inasema hivi, dalili za mtu mnafiki ni tatu, anaposema anaongopa, anapotoa ahadi hatimizi/anaivunja, anapoaminiwa na amana hufanya khiyana. Na dalili zote hizo zipo kwa wanasiasa wetu. Je tunashindwa kuondoa ufisadi na ukiritimba kwenye vyama vyetu kwa mikono yetu, na kubakia kuchukia tu!?
Haya basi tusichnganye dini na siasa... ah ah ah ah ama wametupata kweli kweli.