Mwache atumikie nyumba yake, okoa ndoa yake

Hassan Mambosasa

JF-Expert Member
Aug 2, 2014
3,350
4,485
Sikia,

Umeozesha mwanao, au mdogo wako kaolewa. Elewa huyo hayupo chini ya mamlala yako tena kama ni mzazi. Pia elewa si yule mdogo wako ambaye ulikuwa ukimtuma na kumwambia hivi akawa anatiii. Au uliyemkaripia zamani na hata kuchukua fimbo kama akienda kinyume na maamrisho yako.

Yupo chini ya mamlaka ya mwanaume mwingine, ambaye alimtoa nyumbani kwako au kwenu kwa baraka zenu wote. Hivyo mwache aishi na kuendelea kuwa chini ya mume wake, wasikilizane na kuamuliana mambo yao. Usiwe kipaza sauti chake, kumwamuru aende hivi au vile.

Kama unataka kudumisha ndoa kupitia usbauri, anza na ya kwako. Maana unaishi na mwanaume ambaye unamwelewa vyema, na wake humjui yupo namna gani na ana vipaumbele gani. Namna ya kukaa na mumeo usitumie kumshawishi binti yako au mdogo wako ndiyo aifanye. Wanaume hawajawa wanyama useme wote wana mwelekeo mmoja. Na kama umeachika basi tulizana, ungekuwa na ushauri mzuri zaidi basi ndoa yako ingekuwa imara.

Habari ya kumwita aje kwako na kukaa nawe ukijisikia, hata kama mumewe alikuwa na shida naye sana. Ziishe kama alishatoka nyumbani hayupo chini ya mamlaka yenu, bali ni mamlaka ya mwingine hata dini inamuusia amtii Mumewe.

Siyo mumewe katoka kaenda kazini, basi ushampigia simu aje kwako. Ukae naye, ukijua hawezi kukataa kwasababu wewe ni mkubwa wake. Hadi mumewe akirudi amkose nyumbani aanze kukupigia wewe simu akikwambia umwambie arudi. Unaidhoofisha ndoa yake na heshima kwa mume wake ije kupungua, akijua akiwa kwako basi jamaa hawezi leta lolote.

Hivi ushawahi kujiuliza ndoa yako unafanyiwa hayo? Mzazi wako au dada yako alikuwa akikuendesha kama gari bovu. Alikuita utoke nyumbani kwako atakavyo, hata kama mume hajatoa idhini hiyo? Hebu achia ndoa ya watu isimame, mikono yako isiwe sababu ya kuiharibu.

Huu ndiyo mwanzo wa kukuwadia au kuwaunganisha mabinti na wapenzi wao wa zamani, kisa tu umeshawishiwa na kupewa hela. Kwakuwa amekuwa akikusikiliza sana nafasi hii inatumika kabisa kumshawishi hata aombe talaka kwa mume wake, kusudi aungane na mwanaume ambaye unamtaka wewe na kumwona anafaa zaidi kuolewa na mdogo wako au binti yako.

Unakuta binti alishatulizana na kwenye ndoa yake basi mzazi au dada anaanza kumshawishi aonane na mtu ambaye alikuwa mpenzi wake. Anamwita kwake kusudi awakutanishe, mume akijua ni kwenda kuonna naye kumbe nyuma ya pazia ndiyo anaharibu mambo kabisa.

Pia huu ndiyo mwanzo wa kuwa na sauti mbili ndani ya nyumba, mume anasema hichi mke anakubaliana na uamuzi huo. Ila akitoka na kwenda kujazwa maneno na mzazi au dada, basi anakuja na uamuzi mwingine mpya kichwani. Huo anauleta kwa mumewe, anashikilia na kukazania zaidi juu ya hilo. Kwamba iwe hivi na hataki kuachia msimamo huo. Matokeo ni mume aone anadharauliwa kauli zake, ije kuwa ugomvi mkubwa kwao wote.

Nyumba inabaki mizozo isiyo na maana kisa anachukua maneno nyumbani kwao au kwa dada yake. Jamani kama alishatoka nyumbani kwao siku ya harusi na kuwaaga wote pale nyumbani, inamaanisha hadi kimaamuzi na mambo mengine hawezi kuwa chini yenu. Kila kitu kitafanywa kwa ushirikiano wake na mumewe, maana ndiyo wanaishi pamoja si nyinyi tena. Mlishatoa ruhusa ya kuchukuliwa kwake kihalali, basi endeleeni kuwa kimya hivyohivyo msijipe umuhimu mahali msipohitajika.

Mtumwa ambaye umempa uhuru huna mamlaka naye tena, huwezi kumwita tena na kumfunga minyororo uanze kumtumikisha upya. Mwache aendelee kuutumikia uhuru wake mliyompatia, kama mkiona mlikosea kumpa uhuru bado hamna mamlaka naye vilevile. (Sijalenga kudhalilisha hapa, ni msemo wenye kuhusishanisha tu hali ilivyo)

Atabaki kuwa mwanao vilevile au mdogo wako. Endelea kuamini hilo na pia kuheshimu uwepo wa mume wake. Kufanya kinyume na hapo ni dharau tosha kwa mkwe au shemeji yako. Waheshimu waume wa wadogo au watoto wenu kwa kuacha kuingilia mambo yao. Kuachika si jambo zuri ni mateso kwa watoto wake, kuja kulelewa na mtu ambaye si mzazi wao. Wakosw upendo wa baba na mama

Epusha ndoa ya mdogo wako au binti yako kuvunjika kiholela kwa kujifanya unataka kumwongoza yeye. Waachie mambo hayo na mume wako, ili tupunguze viwango vya talaka zisizo na maana mjini kisa kuingiliwa mambo yao na ndugu. Huyo ni mali ya mume wake na hata kama akiandikwa jina, la mwisho atatumia la mume wake.

Okoa talaka zisizo na msingi, acha kuingilia ndoa za watu. Hakuna mwanaume anayejitambua anayetaka kukaa na mwanamke anayeendeshwa na kwao. Fanya yako mwachie yake.


Hassan Mambosasa
Tanga, Tanzania
 
Back
Top Bottom