Mvua kubwa iliyonyesha wilayani Kilosa imesababisha kukatika kwa barabara kuu ya Dumila Kilosa katika eneo la Ilonga na kupelekea kukosekana kwa mawasiliano kati ya wakazi wa kijiji cha Mvumi na Kilosa mjini huku magari yanayotumia njia hiyo ya kilazimika kupita njia ya Kimamba Kilosa na kuasababisha usumbufu kwa wasafiri watumiao barabara hiyo.
ITV imeshuhudia vijana wa eneo hilo wakitumia msemo wa kufa kufaana kwa kuvusha watu na pikipiki kwa fedha kwa kutumia daraja dogo walilojenga kwa mikono yao.
Wakizungumzia adha hiyo baadhi ya wasafiri wameiomba serikali kujenga miundombinu imara ambayo itasaidia kuoondoa tatizo hilo ambalo limekuwa hujitokeza kipindi cha masika.
Akielezea hatua zilizochukuliwa na wakala wa barabara nchini TANROADS mkoa wa Morogoro mhandisi Godwin Andalwisye amesema tayari wameongeza karavati katika eneo hilo huku akitaja changamoto ya uharibifu wa mazingira kuwa chanzo cha tatizo hilo.