figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,658
- 55,485
Mvua yabomoa daraja la mto Endagaw linalounganisha barabara ya Hanang na Mbulu, Manyara.
Daraja la mto Endagaw linalounganisha mtandao wa barabara kati ya wilaya ya Hanang na Mbulu Mkoani Manyara limebomolewa na mafuriko ya maji yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Manyara na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano ya vyombo vikubwa vya usafiri, huku mamia ya abiria wanaopitia barabara hiyo kuelekea mikoa ya Singida na Simiyu wakilalamikia kutelekezwa na vyombo vya usafiri.
ITV imefika katika eneo hilo la mpakani mwa wilaya hiyo na kushughudia mamia ya abiria waliokwama wakiwa na watoto wakielekea mikoa ya Arusha, Simiyu na Singida kupitia Haydom na wengine wakivuka ili kuendelea na usafiri kutegemea kampuni za usafirishaji kubadilishana abiria, changamoto ambayo inatoa fursa kwa magari madogo kupita kwa uangalifu huku madereva wakilalamikia kukwama kwa siku tatu.
Licha ya wagonjwa wanaosafiri kwenda kupata matibabu katika hospitali ya rufaa ya KKKT-dayosisi ya Mbulu kulalamikia kuchelewa kupata matibabu, baadhi ya raia wa nje nao walioonja adha hiyo wamesema ikiwa daraja hilo limevunjwa na maji, serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka kuondoa adha hiyo ili huduma nyingine ziendelee.
Akizungumza kwa njia ya simu toka eneo la tukio meneja wa wakala wa barabara (Tanroads) mkoani Manyara Bw Yohani Kasaini amekiri kubomolewa kwa daraja hilo na amesema wamepeleka vifaa vya kuanza kutengeneza mchepuko wa barabara kabla ya ujenzi ili kutoa fursa ya vyombo vya usafiri kupita.
Chanzo: ITV