UPDATE:
6. Utafiti - Kupitia utafiti wa Mungu, dunia tunayoijua leo ikaumbwa.
Ukisoma Biblia katika kitabu cha Mwanzo mstari wa kwanza kabisa, kinaonyesha Mungu tayari alishaziumba mbingu na nchi. Unaweza kusema alipoona ukiwa, utupu na giza vimetanda akaona kuna maboresho yanaweza kufanyika na ndiyo kazi aliyoifanya kwa siku sita.
Ukiangalia kila baada ya siku moja, neno linaishia na 'Mungu akaona ya kuwa ni vyema'. Mimi kwa maoni yangu naona kama kwa lugha ya kibiashara, Mungu alikuwa anaenda akiboresha kupitia tafiti. Ndiyo maana hata alipomfanya Adam baadae akaona siyo vyema awe peke yake, ndiyo akampatia Hawa (Biblia kusema haikuwa vema inaonyesha Mungu alikuwa kila akimaliza siku anafanya 'upembuzi yakinifu' au 'assessment'). Baada ya siku sita kuisha akaangalia alipofikia akaona 'bidhaa iko vizuri na iko tayari kuingia sokoni'.
Katika biashara, makampuni mengi duniani, hasa makubwa yanawekeza sana kwenye tafiti. Haya makampuni yana vitengo vya R&D (Research and Development) na wanavipa hela nyingi sana. Hata nchi mbalimbali, mfano Israel ambao ni moja ya nchi zinazoongoza kwa uvumbuzi wa teknologia mpya inajua sana umuhimu wa tafiti. Kupitia tafiti ndiyo bidhaa mpya zinagunduliwa au zile za zamani zinaboreshwa.
Lakini hili halihitaji kubaki tu kwa makampuni makubwa kama Apple au Google. Hata wewe katika biashara yako ndogo usiache kufanya utafiti. Je kuna jambo moja zaidi unaweza kulifanya kuleta wateja wapya? Halafu jaribu hilo jambo uangalie. Ukiona wameongezeka au wale wa zamani wanalipa zaidi, sema ni vyema, iweke kwenye biashara halafu nenda kwenye utafiti unayofuata. Ni hadi hapo utakapoona una 'perfect product' ndiyo upumzike.
7. Fungu la kumi na kubakisha faida iliyobaki kwenye biashara.
Kuna tatizo linatusumbua wengi wafanyabiashara ndogondogo au wale wanaoanza. Nalo ni kujua kiasi gani ule na kiasi gani kibaki kwenye biashara. Wengi hatujiwekei mshahara maalumu, muda wowote unatoa unachotaka, wewe si ndiyo bosi bwana!
Mungu anajua hilo ni kosa kubwa. Aliwaambia Waisrael fungu la kumi ni lake. Yeye wala hataki zaidi wala hataki kuwa anakuja na kujichukulia kama vile chuma ulete! Anajua akitaka zaidi au akichukua bila mpangilio ingawa vyote ni vyake utaumia na biashara itakufa na kesho utashindwa kupeleka hilo fungu la kumi.
Niliwahi kumsikia mfanyabiashara mmoja mkubwa anaitwa Steve Masiyiwa, anayemiliki Kwese TV akisema, hata kama biashara yako ni ndogo, jiwekee mshahara na uwe na nidhamu ya fedha ya biashara. Hata kisheria, biashara ni 'nafsi' inayojitegemea.