Mugabe na siasa za kindumilakuwili!

Mzee wa Gumzo

Senior Member
Apr 21, 2008
197
5
Robert Mugabe kiongozi aliyetawala Zimbabwe kwa miaka 28 sasa amesisitiza kuwa hayupo tayari ‘kushindwa’ katika ngwe ya marudio ya uchaguzi wa rais nchini humo utakaofanyika mwezi ujao.

Kauli ya Mugabe kuwa ‘kalamu haiwezi kushindana na bunduki’ siyo kauli ya kubeza.
Kimsingi Mugabe hazungumzii bunduki za maveterani waliomtoa mkoloni mwaka themanini bali anazungumzia bunduki zinazoandaliwa na maveterani na vijana waadilifu wa ZANU-PF tayari kuzuia kwa hali yoyote ile uwezekano wa MDC kuingia madarakani kwa njia ya sanduku la kura.

Binafsi nilikuwa namheshimu sana Mugabe kama kiongozi wa kuigwa na mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika.Matamshi yake na matendo yake kwa sasa yameongoa kabisa ile sifa aliyokuwa amejijengea ndani ya bara letu.

Anachokifanya Mugabe kinatoa picha mbili tofauti.Kwa baadhi ya waafrika anaonekana kuwa kiongozi asiyekuwa tayari kuona Zimbabwe inaabudu wazungu kwa kukihusisha chama cha MDC na mataifa ya magharibi.
Pili Mugabe anatoa picha ya kuwa king’ang’anizi na mlafi wa maadaraka.Pamoja na ukweli wa kutokuwa tayari kuwaabudu wazungu, haiyumkiniki kuwa ni yeye tu ndani ya ZANU-PF anayeweza kuiongoza Zimbabwe.Hatua ya kutokuwaamini hata wenzake ndani ya chama ilimfanya ajitengenezee mazingira ya kugombea na kuendelea kuitawala Zimbambwe pamoja na kuwepo kwa miongo miwili madarakani.

Ile hoja ya kuwa MDC ni vibaraka au pandikizi la nchi za magharibi inakosa mashiko kutokana na ubinafsi wa Mugabe anaouonesha waziwazi ndani ya chama chake kwa kutokuwa tayari kuwaamini wenzake.

Kauli hii ya jana kuwa kalamu haiwezi kuishinda bunduki ni sababu nyingine kwa wale wanaoendelea kumsifu Mugabe na kumwona kama kiongozi pekee wa Afrika aliyeko mwenye mapenzi ya dhati na nchi yake kutafakari kwa upya juu ya imani yao hiyo.
Huwezi ukatoa kauli nzito na ya shari kiasi hicho inayoonesha wazi kwa serikali imejiandaa kwa vita.Vita aliyoitangaza Mugabe siyo dhidi ya wazungu bali ni dhidi ya MDC, wanachama wake na wanazimbabwe wote watakaompigia kura Tsvangirai.

Kwa ufupi Mugabe ametangaza matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi mapema hata kabla ya uchaguzi kwa kuonesha kuwa mamilioni ya wazimbabwe watatumia kalamu zao kumwingiza Tsvangirai madarakani lakini ZANU-PF kitatumia bunduki kumzuia Tsvangirai asitekeleze matakwa ya wananchi wa Zimbabwe.

Hizi ni salamu za upendo na somo la kisiasa la Mugabe kwa CCM na vyama vingine vilivyoko madarakani tangu kupatikana kwa uhuru Afrika.Nao wanaonekana kulielewa somo ndio maana hawasemi lolote.
Binafsi nitaendelea kumthamini Mugabe wa miaka ya nyuma kama mwanaafrika halisi lakini sitachoka kuendelea kumpinga Mugabe wa sasa kwa kauli matendo ya kibinafsi na shari
 
Back
Top Bottom