Mtumwa aliyechimbia fedha ardhini ili isipotee

Mtumwa aliyechimbia fedha ardhini ili isipotee

John Achila Mukumwa

Senior Member
Joined
Jan 4, 2024
Posts
111
Reaction score
214
Mtumwa aliyechimbia fedha ardhini ili isipotee

Katika maandiko, kuna mfano uliotolewa ya Yesu kwa mitume wake. Mfano huo uko kwenye kitabu cha Mathayo 25:26-30.


Mfano huo unahusu tajiri mmoja kumuachia mtumwa wake, fedha, talanta moja, kisha yeye akaenda safari. Aliporudi kutoka safari, tajiri alitegemea kuwa ile fedha aliyomuachia mtumwa wake, ingekuwa imeongezeka. Lakini, badala yake haikuongezeka hata kidogo, kwani aliichimbia ardhini, ili isije ikapotea. Alikuta kiasi kile kile alichomuachia mtumwa wake.

Huyo tajiri alichukizwa na ile hali, na kuona kuwa yule mtumwa ni mpuuzi na mzembe. Akamtimulia mbali.

Hapa kuna mambo ya kujiuliza
Mosi
: kulikuwa na ubaya gani kwa mtumwa yule kurudisha talanta ile moja, kwani hakupoteza kitu wala hakuleta hasara yo yote? Pili: je kulikuwa na sababu gani ya yeye kuhukumiwa vile?

Ili tuweze kuelewa vizuri sababu ya mtumwa yule kuhukumiwa vile, tuisome habari yenyewe kwa uchache.

Mathayo 25:14 “Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. 15 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri”.
Ni muhimu tuzingatie hayo maneno mawili watumwa wake na mali zake.

Tukiisoma habari hii tunaweza kutafakari kuwa huyu mtu aliwekeza mali zake kwa “rafiki zake” au “ndugu zake”.
Ingekuwa heri kama ingekuwa ni rafiki zake au ndugu zake, kwani hata wasingeleta faida yoyote angeweza kuwaelewa. Lakini, aliwekeza mali zake kwa watumwa wake ambao ni watu anaowalipa mshahara kila baada ya muda fulani.

Hebu piga picha, una biashara yako, halafu umeajiri mfanya kazi na kukubaliana naye mshahara, na ukaondoka. Kurudi jioni unakuta hajafanya kazi yoyote. Mbaya zaidi, anakuambia fedha zako za mtaji zipo pale pale hajazigusa.

Bila shaka utachukizwa naye. Kwa nini?
Kwanza: ulitegemea kupata faida, ndiyo maana wewe ukamweka pale kufanya kazi. Pili: mshahara wake unatokana na faida katika hiyo kazi, kwa utendaji wake. Kwa hiyo, kama hatafanya kazi yo yote na mwisho wa siku au mwisho wa mwezi, atataka mshahara, je utamlipa nini? Maana utakapofika mwisho wa mwezi atakudai mshahara, kwani wewe umeshaingia naye mkataba wa kumlipa.

Kwa hiyo, ni wazi kuwa ni lazima utakasirika, kwa sababu kutofanya kwake kazi ni hasara kwako, kwani mwisho wa siku ni lazima utamlipa.

Hivyo, anakurudisha nyuma. Hata kama hajagusa mtaji wako, lakini mwisho wa siku utaathirika wewe katika kumlipa mshahara. Hivyo ni hasara.

Ndicho kilichomtokea yule mtumwa aliyeficha talanta aliyopewa na bwana wake. Ni kweli kairudisha ile talanta kama ilivyo, lakini mwisho wa mwezi atataka mshahara, kwa sababu yeye ni mwajiriwa na si ndugu au rafiki. Bosi wake atatoa wapi fedha ya kumlipa, ikiwa hajazalisha chochote?

Ndiyo maana bwana wake akamwambia ni heri hata angeipeleka kwa watoa riba, kama vile benki, kuliko kuificha ardhini.

Tuangalie kitabu cha Mathayo 25:26-30
Mathayo 25:26 "Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;
27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.
28 Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.
29 Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.
30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Hili ni fundisho kamili kwa wakristo, kwamba vipawa, karama na uwezo tuliojaliwa na Bwana, tutumie katika kumtumikia Mungu pasipo udhuru. Hii ni kwa sababu sisi ni watumwa wake, ametuweka kwa faida yake.

Bwana atusaidie tusifiche karama na talanta zetu ardhini, bali tuzitendee kazi au tuzipeleke kwa watoa riba, ili ziongezeke.

Maeneo ya kutendea kazi au watoa riba ni pamoja na makanisani, kwenye jumuiya za wakristo na uenezaji wa injili. Usifiche fedha zako, bali zitumie hata katika kuipeleka injili, kupanua wigo wa kueneza Neno la Mungu, ili mwisho wako usiwe kama yule aliyeficha talanta yake ardhini.

Kumbuka kuwa mwisho wa siku, utaulizwa: je, ulifanya nini katika kueneza Neno la Mungu, ili liongezeke na kusambaa?
 
Watu wamegoma kutoa sadaka nini? Nakumbuka mchungaji wetu mapato yakiwa machache huwa anatoa hilo fundisho🤔
 
Watu wamegoma kutoa sadaka nini? Nakumbuka mchungaji wetu mapato yakiwa machache huwa anatoa hilo fundisho🤔
Haha! kule wewe ni shekhe huku ni mutu ya mchungaji!..😅
 
Back
Top Bottom