AMA kwa hakika usilolijuwa litakusumbua, usemi ambao hutumiwa na watu wengi katika nyakati tofauti wakiashiria matukio anuai wanayokutananayo wakati wakitekeleza majukumu yao.
Na maranyingi mtumiaji anapoamua kutumia msemo huu huwa na lengo la kufikisha hujumbe fulani kwa jamii na hasa pale anapobaini kuna jambo moja ama jingine limetokea.
Haijalishi kwamba jambo lenyewe ni chanya au hasi itategemea mtazamo wa mzungumzaji utakavyokuwa kwa wakati.
Nimesema hivyo kwa sababu baadhi ya watu siku hizi ili waweze kufanikiwa katika mambo yao ni lazima wajaribu kusema au kutengeneza uongo ili kuweza kuhalalisha uharamia wanaoutaka dhidi ya mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu au taasisi kwa maslahi binafsi au taasisi zao.
Mtakumbuka wakati wa kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 pale vyama vya siasa vilipoanza michakato ya kumpata nani atakayewakilisha Chama chake kwenye kinyanganyiro cha kupeperusha bendera ya chama chake.
Baadhi ya wagombea kwenye vyama vyao walitumia mikakati ya kuchafuana ili kila mmoja aweze kupata nafasi ya kukiwakilisha chama chake hata kama mkakati huo kwa upande mwingine ulikuwa ukihatarisha mshikamamo na umoja wa chama chake.
Hali ya kuchafuana ilitumika kwa kiasi kikubwa mpaka ikafikia hatua kiongozi mkubwa mmoja akatoa kauli kwa umma kwamba ukimuona mtu anatumia kalamu ya waandishi kuwachafua wenzake kwa lengo la kuhakikisha malengo yake yanatimia, mtu huyo atahakikisha anaendelea kubaki kwenye nafasi hiyo hata ikibidi kutumia risasi ili aendelee kubakia.
Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa taasisi au jamii ya watu katika harakati zozote zili za kufikia malengo ya taasisi na umma kwa ujumla wake.
Mtaona mustakabali wa watu waliotumia kalamu kuchafuana, leo hii taasisi yao imekuwa haina umoja tena wala mshikamano miongoni mwao.
Bali ina makundi ambayo kila mojawapo linasimama na kutetea maslahi ya kundi lake, hali inayopelekea hivi sasa nchi kuingia kwenye matatizo makubwa yakiwemo balaa la giza!.
Mfano mwingine kuna Chama kinakituhumu Chama cha Wananchi (CUF) eti ni CCM B hali yakuwa wanajua CUF ndio kiongozi wa Demokrasia hapa nchini na kipindi chote kimekuwa kikiongoza umoja wa vyama vya upinzani ili kuhakikisha lengo la kuiondoa CCM madarakani linatimia.
Historia inaonesha kwamba, kwenye Bunge la tisa CUF ndicho chama ambacho kilikuwa na Wabunge wengi Bungeni na hivyo kuwa na uhalali wa kuunda kambi rasmi Bungeni.
Hata hivyo hakikufanya uchoyo, bali kilivishirikisha vyama vyote vya upinzani vilivyokuwa na wabunge Bungeni ili kuunda kambi ya upinzani ya pamoja katika kuwatetea Watanzania walio wengi.
Sote tuliwaona kina Hamad Rashid, Padri Willbroad Slaa, Habib Mnyaa, Zitto Kabwe na wengine walivyoungana kutetea maslahi ya watanzania bila kujali vyama vyao.
Lakini leo hii baadhi ya hao walioshirikiana na kina Hamad Rashid ndio wamekuwa mstari wa mbele katika kusema CUF ni CCM B ili kuwahadaa Watanzania na kuwaaminisha kwamba wanayoyasema ni ya kweli kwa kutengeneza uongo kwa ajili ya kutimiza malengo yao.
Wakati wa Bunge la tisa mtakumbuka Bunge lilibadilisha kanuni chini ya Spika wa kasi na viwango Samuel John Sitta kwa kuruhusu kamati tatu za Bunge kuwa lazima ziongozwe na Wenyeviti kutoka kambi ya Upinazani Kamati ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma, Kamati ya Serikali za Mitaa na Kamati ya fedha za Serikali Kuu.
Kwa mujibu wa kanuni hizo ni kwamba Wenyeviti wa Kamati hizo huchaguliwa na wajumbe wanaounda kamati hizo ambapo wengi wao walikuwa wanatokana na CCM.
Na hivyo waliochaguliwa kuongoza kamati hizo kwenye bunge la tisa hakuna hata mmoja alitoka chama cha CUF.
Waliochaguliwa kuongoza kamati hizo walikuwa Dk Slaa (LAAC) na Zitto Kabwe (POAC) wote kutoka Chadema huku John Cheyo wa (UDP) akiongoza kamati ya (PAC).
Pamoja na kuwa CUF waliomba lakini wajumbe wa CCM waliwachaguwa waliowaamini pengine ndio walioona kwamba wanamaslahi nao, lakini hakuna aliyewaona Chadema ni CCM B.
Hivyo basi ni dhahiri mtaona nani kati ya CUF na hivyo vyama vingine anastahili kuitwa CCM B, Chama cha CUF hata siku moja hakijawahi kuwaambia watanzania kama vyama hivyo ni CCM B kwa kuwa kinaamini ni utaratibu uliowekwa na kanuni za Bunge ili kuendesha shughuli zake.
Aidha wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010 kada maarufu wa CCM Mustafa Sabodo alijitokeza hadharani na kukisaidia Chadema fedha za kuendesha kampeni.
Katika hilo pia hakuna aliyehoji kwamba inakuwaje Chadema inayodai CCM ni chama kinachoongozwa na genge la mafisadi, lakini bado viongozi wake wanapiga magoti mchana kweupee na kupokea msaada wa fedha kutoka kwa kada wa CCM!
Mbali na hilo, viongozi wa chama hicho walizunguka nchi nzima na kuwaambia Watanzania kuwa wakipewa ridhaa ya kuongoza nchi mfuko wa saruji utauzwa 5,000/= bati, mbao na vifaa vingine vya ujenzi vitashuka bei,
Pia wangeleta treni ya kwenda kasi kutoka Dar es Salaam hadi mwanza kwa masaa machache pamoja na kuunda Katiba mpya kwa siku 100 tu!
Walijaribu kutumia aina yoyote ya hadaa kwa watanzania ili malengo yao yatimie, upepo wa kisiasa ukabadilika na watanzania wakakubaliana na hadaa hizo.
Baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 watanzania waliwachagua wabunge wa vyama vya upinzani kutoka kwenye majimbo, CUF wabunge 24, Chadema wabunge 23, NCCR Mageuzi wabunge wanne, TLP na UDP mbunge mmoja mmoja kila chama.
Chama cha CUF na Chadema kilifanikiwa kupata wabunge wa viti maalum, Chadema wabunge 25 na CUF wabunge10.
Chama cha CUF kilifanikuwa kushiriki kuunda Serikali ya Ummoja ya Kitaifa Zanzibar baada ya kufanikiwa kuwa na Wawakilishi ndani ya Baraza la Wawakilishi na kufikisha zaidi ya asilimia tano ya kura zote zilizopigwa na Wanzazibar kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar.
Hata vyama vingine vya Siasa vingefanikiwa kuwa na wawakilishi na kufanikiwa kupata kura kuanzia asilimia tano vingeshirikisha kuunda Serikali ya Ummoja wa Kitaifa Zanzibar.
Mafanikio ya kisiasa yaliyopata Chama cha CUF kwa upande wa Zanzibar ndio yamezusha chuki na hasada kwa badhi ya vyama vya upinzani hususani Chadema na kuanzisha propaganda za kusema CUF ni CCM B na kuanza ghilba na hadaa kwa watanzania kukinasibisha CUF na CCM ili watimize malengo yao ya kuaminika na Watanzainia.
Chuki, choyo na hasada zikahamishiwa katika Bunge la kumi la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Chadema kufanikiwa kuwa na Wabunge wengi kwa mujibu wa kanuni za Bunge za kuunda Kambi rasmi Bungeni bila kuvishirikisha vyama vingine vya Upinzani.
Hali hiyo ilepelekea Chadema kufikia hadi kusema hawako tayari kushirikiana na vyama vya upinzani hovyo hovyo vya siasa vyenye wabunge Bungeni.
Walifanikiwa kuunda Kambi rasmi Bungeni bila kuvishirikisha vyama vingine vya Upinzani Bungeni kwa mujibu wa Kanuni za Bunge na sarakasi ikaanza pale walipotaka hata zile Kamati tatu kimsingi zinazotakuwa kuongozwa na Wabunge wa Upinzani nazo walitaka kuziongoza wao peke yao, angalieni choyo na roho baya ya madaraka waliokuwa nao hawa jamaa.
Lakini chakushangaza na kustahajabisha Chama cha CUF wajumbe waliokuwa wengi wa CCM hawakuwapa ridhaa ya kuongoza hata kamati moja japokuwa waligombea.
Wajumbe wa CCM walimchagua Zitto Kabwe POAC, Mrema LAAC na John Cheyo PAC, sasa wasomaji wenyewe mtabaini kulikoni.
Mimi binafsi siamini na wala sitaki kuamini ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama kuna Wabunge waliochaguliwa na wananchi wa Taifa hili la Tanzania kupitia vyama vyao eti vyama hivyo ni hovyo hovyo.
Isipokuwa kutokana na hadaa waliyokuwa wakiifanya viongozi wa Chadema wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwakajana kama nilivyokumbusha hapo juu, watanzania wakawachagua wakidhani ni watu wema!
Kumbe mara baada ya kuingia bungeni na mara kwa mara wakionekana kususia vikao hivyo kwa kutoka nje kama watoto wadogo, ndipo ilipobainika kwamba vingaavyo vyote sio dhahabu.
Na hapa ndipo nami ninapowataka wananchi wanaoishi kwenye majimbo ambayo wabunge wa Chadema wameshinda kukumbuka msemo huu wa wahenga kwamba, Usilolijua litakusumbua.