Mentor
JF-Expert Member
- Oct 14, 2008
- 20,328
- 23,909
MSALABA
Nilipata fursa ya kwenda nyumbani kwa ajili ya sikukuu ya pasaka. Haikuwa rahisi kupata ruhusa hii ukizingatia uongozi wa sasa wa hapa kazi tu. Ila, bosi wangu hakuwa na budi kuniruhusu maana nilimtoa kwenye shimo kubwa wiki moja kabla ya pasaka. Jumatatu ya tarehe 21/03 nikamuambia anipe ruhusa niende nyumbani kwa ajili ya pasaka; niondoke Jumatano na kurudi Jumanne, na isikatwe kwenye likizo yangu ya mwaka huu. Kwa sababu za kiusalama sitotaja sehemu ninayofanyia kazi…maana sisi ni masikini, masikini sana!Niliukuta msalaba nyumbani. Msalaba uliotundikwa ukutani, wenye urefu wa sentimeta 45 kwa ile mbao ya kushuka na sentimeta 30 ile mbao ya kulala. Ulichongwa vizuri ila haukuwa umepigwa nakshi yeyote. Lakini ulikuwa umetundikwa sebuleni. Kama usingekuwa ni msalaba, basi usingefaa kuwa sebuleni, maana hauna urembo wowote. Lakini kwa kuwa ulikuwa ni msalaba, basi sikuwa na cha kusema.
Hata hivyo, mama yangu alinikuta nikiushangaa msalaba ule. Akaniuliza, “Unashangaa nini baba yangu (kwa mila za kichaga, mtoto wa pili wa kiume anachukua jina la baba wa mama yake),” Nikamuuliza, “Mama, kwa nini huu msalaba msiupige rangi walau upendeze. Hamuoni unaondoa urembo wa sebule?”
“Mwanangu,” alianza kusema mama, “Huo msalaba unanikumbusha mbali sana”
1977, Dodoma
Nilikuwa nimemaliza chuo na kupangiwa kwenda kufanya kazi Dodoma chini ya RTC (Regional Trading Company). Nilikuwa binti mdogo bado, yaani sijaolewa, hivyo nyumba niliyopewa tulikuwa tukiishi na mwenzangu, Asteria. Alikuwa ni binti aliyeokoka sana, yani ni wale tunawaita kwa kimombo ‘smoking hot Christians’. Ndiye aliyenifundisha kuomba kwa ajili ya mume unayemtaka. Na ndiye aliyenifanya nikapenda kwenda kanisani. Simaanishi nilikuwa binti mbaya, ila nilikuwa makini na Mungu wangu zaidi baada ya kukutana na Asteria.
Tulikuwa tukienda kanisa la Kilutheri huko.
Mwaka 1978 mwanzoni alikuja Mchungaji mwanafunzi kutoka chuo cha uchungaji Makumira. Alikuwa kijana wa umri wetu na nakumbuka tulizoeana naye haraka kwa kuwa Asteria ndiye aliyempeleka kununua vifaa vichache kwa ajili ya nyumbani kwake. Alikuwa pia akimsaidia kununua mahitaji ya jikoni kila aendapo sokoni. Asteria alijitoa sana kwa kanisa na kumfanya mchungaji ajisikie kuwa yuko nyumbani.
Hivyo, tukawa tumezoeana naye na mara nyingi alikuwa akija kwetu kwa ajili ya sala ya jioni kwani nyumba yake ilikuwa upande wa pili wa barabara kutoka kwetu. Baada ya miezi michache alituambia kuwa mkewe angekuja kumtembelea na kwamba angekaa na yeye kwa miezi sita iliyobaki kabla ya yeye kurudi chuoni Makumira kumalizia mafunzo yake.
Alitueleza kuwa mwezi mmoja kabla ya kuja Dodoma alikuwa ametoka kufunga ndoa. Tulimsaidia kufurahi na zaidi hasa kwa kuwa mke wake angekuja tumwone maana alikuwa ni kijana mpole mno. Akiongea kama humfahamu vyema unaweza kuhisi analalamika.
Hata siku mama mchungaji anawasili Dodoma mjini, sisi ndio tuliompokea. Tulijitahidi kumfanya ajisikie yuko nyumbani kwani mara nyingi tukitoka kazini tulikuwa tukienda kwake kupiga naye soga. Ila hatukuweza kumzoea sana maana tulijua ni mama mchungaji, si vizuri kumuuliza mambo mengi.
Jumapili iliyofuata, ilitangazwa kwenye matangazo ya kanisa kuwa tutatambulishwa mama mchungaji. Kila mtu alikuwa na hamu ya kumuona huyu mama mchungaji mwanafunzi. Nakumbuka vyema alikuwa amekaa siti ya nyuma kabisa. Baada ya mahubiri mchungaji alisimama mbele ili amwite mkewe washarika wamsalimie lakini hakuonekana, alikuwa ametoka kanisani. Tuliporudi nyumbani hatukuweza kumuuliza alienda wapi maana nimama mchungaji.
Wakati huo huo, Asteria rafiki yangu alikuja nyumbaji jioni moja, akaniambia, “Mama Mentor (alitumia jina langu la kwanza), leo nimekutana na jaribu.” Nikamdodosa aniambie ni nini kimemtokea.
Ndipo akanieleza alikutana na mtu wakati akitoka kazini. Mkaka mrefu, mzuri, mwanajeshi. Alimsimamisha na kumuambia kuwa amemuona mara kadhaa eneo lile na angependa kumfahamu zaidi.
“Umeokoka?” ndiyo swali la kwanza nililomuuliza huku moyoni nikitamani anijibu ‘ndiyo’.
“Nilikuwa nimeshaanza kujiona mke wa askari mwenzangu,” aliendelea kuelezea Asteria.
“Alinijibu hapana ila yeye ni Mkristo. Moyo uliniuma lakini nilijikaza nikamwambia, ‘ukitaka kunifahamu njoo kanisani’.”
Basi tukaachana naye ndipo nikaja nyumbani. “Hivi mama Mentor, kwa nini hawa vijana wazuri hivi hawajampokea Yesu? Nitamuombea aokoke”
Nilijaribu kumuonya kuwa makini na hisia zake lakini aliniambia atahakikisha anamuombea mpaka aokoke.
Jumapili iliyofuata, baada ya ibada kwisha na kama kawaida Mama mchungaji kututoroka nilishangaa navutwa mkono. Kuhamaki ni Asteria ananipeleka upande ambao wanaume huwa wanasimama.
“Huyu anaitwa kaka Masatu, ndiyo yule askari niliyekuambia nilikutana naye, amekuja kanisani!” Nilishindwa kujua niseme nini nikaishia tu kumuambia, “Bwana Yesu asifiwe kaka” naye akaitikia kisha nikarudi kuendelea na mambo yangu.
Niliwaacha pale nikarudi nyumbani na Asteria aliporudi akaniomba nimruhusu Masatu aje kututembelea kwa chakula cha mchana siku moja.
Tulikuwa tumekubaliana kuwa hakuna wanaume kuja nyumbani kwetu na kwamba akija ni lazima sote tuwepo, hivyo ombi lile ni ili nisipange ratiba yeyote siku hiyo waliyokuwa wamekubaliana niwepo. Nilikubali ingawa niliona kama ni haraka sana.
Siku, wiki zikasogea na hatimaye kuwa miezi mitano na kaka Masatu akampokea Yesu, akaokoa. Alimtamkia Asteria kuwa anampenda na kwamba angependa kumuoa. Asteria kwa hamu ya kuweka ushuhuda wa kuolewa na kijana aliyemsaidia kuokoa akamkubalia ila Masatu alimwambia wafanye harusi ndogo tu na kwamba watafanya harusi kubwa siku akienda kwao Mwanza. Kipindi kile alikuwa Makutopora kwa kozi maalum na mafunzo ya utayari.
Jumatatu moja jioni, alikuja nyumbani kwetu mchungaji mwanafunzi akiwa analia machozi. Ni vigumu kuelezea kwa maneno ila alikuwa akilia kama mtoto. Tulijitahidi kumbembeleza lakini ilikuwa kazi bure. Mwishowe tuliamua kusubiri hadi atakaponyamaza atuelezee ni nini kilimsibu. Alikuwa anatia huruma sana!
Baada ya kunyamaza alianza kutusimulia kuwa, usiku wa kuamkia siku hiyo, mkewe aliumwa sana tumbo. Alimshauri waende hospitali – maana ilikuwa karibu tu na tunapoishi – lakini mkewe alikataa. Hivyo aliamua kutulia mpaka asubuhi ili ampeleke hospitali ila hawakuweza kulala kabisa.
Asubuhi na mapema aliamka na kumwambia mkewe waende hospitali ila alikataa bado. Hivyo kwa uoga aliamua kutoka na kwenda kumuita mama wa makamo wa jirani amsaidie baada ya kumuelezea mkasa mzima. Mama yule akamuambia ampeleka hospitali bila hata ya kutoka ndani kwenda naye kwake.
Mama yule alimwambia, “usisahau kwenda na kadi ya kliniki, si mlikuwa mnaenda? Usisahau kumchukulia na khanga na nguo chache” Mchungaji alibaki anashangaa asijue cha kujibu kwani ni miezi mitano tu iliyopita ndiyo mkewe alimwambia kuwa haoni siku zake hivyo alijua mama yule hataki tu kumsaidia na kwamba mkewe hajafikia muda wa kujifungua.
Alirudi nyumbani kwake bila msaada ila alipoingia ndani hakumkuta mkewe.
Akamfuata tena yule mama kumueleza kuwa hajamkuta mkewe ndani. Yule mama akamwambia aende hospitali, atangulie yeye anakuja nyuma.
Mchungaji akatoka mbio kwenda hospitali akaanza kuzunguka kwenye wodi tofauti tofauti akimtafuta mkewe bila mafanikio. Ni hadi anatoka wodi ya mwisho ndipo alipokutana na yule mama wa makamo wa jirani aliyemwambia atangulie hospitali. Yule mama alishangaa kumuona mchungaji anatoka wodi za wagonjwa wa kawaida ndipo akamshika mkono na kumpeleka wodi ya wazazi. Kabla hata mshangao wake haujaisha, alipokelewa na manesi wa pale wakimwambia, “hongera mchungaji, umepata dume.” Akazimia!
Alipoamka bado wakaendelea kumpa hongera kwani walihisi alizimia kwa furaha ya kupata mtoto. Kumbe yeye anatafakari mtoto kapatikanaje. Akawauliza kama mtoto amezaliwa akiwa katimiza muda wote – yaani miezi tisa - jibu ambalo lilimchosha zaidi. Akaingia wodini akamkuta mkewe na mtoto anamnyonyesha.
Hapo ndipo ukweli ulipomuingia na ndipo alipoanza kulia na kwamba ameshindwa kuelewa ilikuwaje.
Sisi nasi ndipo tukaanza kufunguka macho kukumbuka yale maongezi aliyokuwa akitueleza yule mama mchungaji, “Nyie ombeni tu Mungu lakini ujue wakati mwingine unaweza kuolewa na mtu tofauti kabisa na unayempenda. Mimi kuna mkaka nilikuwa nampenda jamani…” Na kwa ushamba wetu hatukujua kuwa yule dada alikuwa na ujauzito. Kumbe wakati anakuja Dodoma alikuwa ana ujauzito wa miezi takribani minne tayari.
Muda ule ule wazee wa usharika wakaja na kuanza kuongea na mchungaji mwanafunzi huku wakimuuliza maswali. Mchungaji yule alizidi kulia na kushindwa kuongea nao. Siku iliyofuata mama mchungaji akaruhusiwa kurudi nyumbani baada yaa mtoto kupewa chanjo za kwanza na mchungaji alienda kumchukua mke wake wakarudi nyumbani. Jumapili iliyofuata mchungaji alitangazwa kuwa ametengwa na kanisa kwa kitendo alichokifanya.
Ni hadi baadaye ndipo alipokiri kuwa kabla ya ndoa hakuwahi kumfahamu mkewe kimapenzi. Hivyo wiki iliyofuata tena mchungaji alirudishwa kanisani ila mkewe akatengwa. Wazee wa kanisa na mwinjilisti waliwa na parish worker wakaanza kufurika wakipokezana kila siku kwenda kwake kumpa neno kuwa amsamehe mkewe na kwamba hayo ndiyo majaribu yatupatayo Wakristo na kwamba inatupasa kuyashinda.
Alirudi tena kwetu akilia akatueleza hasa kilichokuwa kikimliza maana alikuwa akilia karibu kila siku hasa akikutana na sisi.
Wakati anafika pale Dodoma, kazi yake ya kwanza aliyopewa ilikuwa kwenda kuwapatanisha wanandoa watu wazima sana kwake ambao mke wa bwana huyo aligundulika kuwa mtoto wake wa pili kati ya watatu aliozaa na huyo bwana, sio wa mume wake wa ndoa. Mume alishindwa kumsamehe na hivyo alitaka waachane.
Mchungaji alimsihi sana yule mzee amsamehe mkewe maana wao ni Wakristo na kwamba tumefundishwa kusamehe saba mara sabini. Alitusimulia alivyomhubiria yule bwana kuwa amri pekee tuliyoachiwa na Bwana Yesu ni upendo, na kwamba ni jinsi gani utakuwa umeonesha upendo wa dhati kama kumsamehe na kumpokea tena mkewe.
Alimhubiria jinsi gani Mungu alitufananisha sisi na mwanamke malaya, aliyetolewa kwenye madanguro na kuolewa kisha akamtoroka mumewe usiku na kwenda kwenye umalaya wake. Lakini bado mume – Mungu – alirudi na kumtafuta mkewe, kumfuata na kumrudisha nyumbani huku akiwa amemsamehe. Alimueleza hata kwenye habari hiyo Mungu alisema tumezaa watoto katika uasherati wetu lakini bado anatuita na anatupenda. Je, si zaidi sisi tunawiwa kusamehe tunapokosewa na wapendwa wetu?
Aliumia maana aliona ilivyo ngumu kusamehe katika hali ile na kwamba yeye alikuwa akimlazimisha mzee yule kumsamehe mkewe.
Baada ya wiki mbili tangu tukio lile, mchungaji alikuja kutuaga kuwa anarudi Makumira kuendelea na mafunzo yake.
Alikuja na msalaba mmoja akatuachia akasema, “Dada zangu, huyu Mungu mnayemtegema msimuache.”
Asteria alisikitika sana mchungaji kuondoka maana angekosa harusi yake na Masatu lakini hakuwa na budi kurudi chuoni. Asteria aliolewa mwezi uleule mchungaji alioondoka na baada ya ndoa alihamia kwenye nyumba kambini alimokuwa akiishi Masatu, mumewe mpya.
Mwaka huo huo, 1978, ndipo kulipotokea vita vya Kagera wakati Idd Amin alipotuvamia. Masatu na wenzake iliwabidi wajikusanye kuelekea vitani.
Hapo ilibidi Asteria afungashe naye vitu vyake aende kijijini kwa Masatu mpaka vita vitakapoisha ndipo arejee na yeye Dodoma. Hivyo ndivyo alivyoambiwa na Masatu, mumewe. Hapo Asteria alikuwa na ujauzito tayari.
1979 Dodoma
Nilishtuka nilipoufungua mlango wangu asubuhi ya saa kumi na mbili baada ya kusikia mtu akigonga maana sikuwa nategemea kupata mgeni yeyote siku ile, hasa asubuhi yote ile. Nilishtuka zaidi nilipokutana na sura ya mdada aliyekondeana na tumbo limejaa kama vile ana utapiamlo; alikuwa Asteria! Nililia machozi tukakumbatiana tukalia pamoja. Nakumbuka palepale kwenye ngazi za kuingia kwangu tulikaa akanihadithia kilichotokea.
Kumbe, Masatu alikuwa ameoa huko kijijini kwao hivyo alipofika alimkuta mke mkubwa na watoto wawili tayari. Mke mkubwa hakufurahishwa kabisa na ujio wake hivyo alimtesa sana. Ni hadi alipoweza kwenda kanisani na kukutana na mchungaji ambaye aliwahi kuja kuhudumu pale kanisani Dodoma akamhadithia mkasa wote. Mchungaji yule akajikusanya akampa nauli akatoroka na treni usiku ule ambapo ilimbidi kulala stesheni kwani treni ilipita pale usiku sana. Alisafiri bila kula chochote kwani pesa aliyopewa ilitisha tu kwa nauli na ndiyo amefika asubuhi ile baada ya safari ya siku mbili.
Nilimkaribisha ndani na kumuandalia uji mwepesi maana hata maji niliyompa aliyatapika. Wakati huo ujauzito wake ulikuwa umefikisha miezi nane. Alikuwa amekonda sana na mwili haukuwa na nguvu. Nadhani hiyo ndiyo iliyopelekea yeye kujifungua kabla ya tarehe iliyotarajiwa ya kujifungua kwake. Kwa bahati mbaya Asteria alifariki wakati akijifungua mtoto wake na mtoto wake pia alifariki.
“Sasa mama huo msalaba?” Niliuliza, maana niliona mama ameshanipoteza kwenye mtiririko.
Ooh! Alirudi nao Asteria hivyo nilibaki nao baada ya yeye kufariki. Huu msalaba ulinitesa sana maana sikutaka kuolewa kwa muda mrefu sana. Na nikasema siufanyii chochote, ndiyo maana unaona uko hivyo hivyo kama tulivyopewa na yule mchungaji mwanafunzi!
Wasalaam wapendwa,
Mentor.