Mposaji kamroga mshenga wake huku jamani

mpasta

JF-Expert Member
Jan 17, 2011
917
1,998
MHH! MSHENGA YAMEMKUTA MAMBO HUKU USWAHILINI KWETU!

Kuna ubuyu ukiupata hata kulala nao huwezi mpaka uumungu'nye ndio roho kwatu, itatulizana!

Kuna barobaro mmoja bwana, ana kiduka chake anachambikia maisha siku zinasonga. Sasa kuna Binti mmoja, shungi kwa sana, Mzenji kwa asili yake, anakuja dukani kwake jamaa kununua mazagazaga kila uchao.

Jamaa akatokea kumtapia rohoni Binti wa watu uzalendo ukamshinda, akamsomesha weeh, durusu ikaeleweka na Binti kwa kiwango cha muntazi. "Kama kweli unanipenda niwe mahabuba wako, peleka barua nyumbani, mie sina kipingamizi. Binti aliroroma kwa jamaa, ashindwe yeye tu. Jamaa huba limemfika mpaka kooni, haoni wala hasikii la mchotea maji msikitini wala la mnadi swala, himahima akajichanga, akamtafuta Mshenga, fundi bomba wa kuunganisha laini maji yaweze kutoka.

Sasa hapo ndipo hekaheka yenyewe inapoanzia sasa, mshenga na kanzu yake ile nyeupee pee ya kuswalia swala ya Ijumaa, kichwani anakofia yake nyekundu ya tarabushi, chini ana makubazi, kiguu na njia mpaka na barua yake mkononi mpaka kwa wazazi wa Binti akawakabidhi mzigo wao. Akrabu wa Binti wa kikeni na kuumeni wamejazana kochokocho kwenye manzili kusubiria barua ya posa isomwe.

Baba mzazi akairarua bahasha, na kuanza kuidurusu barua hiyo kwa sauti ya juu. Najua msomaji hujui namna barua ya posa inavyoandikwa hilo somo lingine, siku nyingine. Basi bwana, mpaka ibara ya mwisho ya barua hiyo ikamalizikia, "Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuiona nyumba yako, na ninasubiri kusikia kutoka kwako.

Mwenyezi Mungu akujaalie afya njema wewe pamoja na familia yako. Basi hapo shangwe, nderemo, na vigeregere vya furaha sheshe vikalipuka, tayari Binti yao kaposwa. Kumbe Bwana, Mshenga yule kumbe "Mshenga Kichefuchefu", kuona uzuri tu wa yule mwali, akapandwa na raghba ya mapenzi juu yake, akawa anatapikia sandani kimoyomoyo.

Akajiapiza Yasini Mkubwa nafsini mwake kuwa hawezi kukubali kuwa kitoroli kwa binti mrembo kama yule, lazima abadilishe gia angani amtwae yeye. Kutoka pale akiwa ameshapewa jibu la kiasi cha mahari, kufika kwa kijana wa watu aliyemtuma anaanza kugeuza kauli.

Kijana anamjibu mara "Ooh...usratu ya Binti sijawakuta nitaenda siku ingine kuipeleka barua". Kule Ukweni kapiga simu ya kifatani kabisa "Ooh, huyu kijana muoaji tabia zake kabihu kabisa, kwanza ni mlevi, mwasherati, sipo tayari kumsimamia tena!"

Baba wa Binti mtu swalihina, vipindi vitano vya swala havimkauki, kusikia kuwa muoaji ni karubandika tena paka shume, akaitia na kama posa yenyewe hamtaki tena muuaji. Mshenga Kichefuchefu kusikia kuwa posa imepigwa mkasi, moyoni mwake sasa furaha fokofoko.

Haraka haraka akaenda kwao huko Rufiji kuuza mashamba yake ya urithi, karudi Jijini hapa na ngwenje za kutosha tu, akitembea anatembea kwa mwendo wa tunga mikono anaitupa tupa yamini wa shimari kwa madaha usicheze na pesa wewe, Tafuta pesa kijana!

. Naikatisha tu stori hii, Basi kwa kupitia mlango wa nyuma, yule Mshenga kajifanya Dr. Mwaka kapeleka posa yake mwenyewe, Binti hana jinsi kwa shinikizo la wazazi na nguvu ya pesa kakubali kuolewa na Mshenga kwenye ndoa ya mitala kama mke wa pili.

Kijana kwa hasira kasema usinitanie wewe Mshenga Kichefuchefu, kamsafiria kwa Bibi Kisiju huko kwenda kumtengeneza adabu imvae vizuri.

Unaambiwa, umesagwa mkungu, ola ola za kutosha, tahamaki mshenga yamemkuta mambo. Akiingia uwanjani na mkewe, anapasha mazoezi vizuri tu, mpira tuweke kati mchezo uanze, mguu wa tatu wa kuchezea mpira unapotea hauonekani. "Mtume weeeeh! Mtume weeeeeh!" Kelele mtindo mmoja.

Majirani wa Uswahilini kama uwajuavyo hawana dogo, wakajaa tele, wengine mpaka madirishani, kulikoni kelele hizo!

Kwa sura iliyojaa soni, tahayuri na fedheha, machozi yanamtiririka kama ngamia anayetaka kuchinjwa, inabidi aeleze mkasa mzima dhahiri shahiri.

Hivi sasa kijana anatafutwa ili akategue tego lake, haonekani na duka mtaani kafunga.


Jamani pesa zenu hizo tumieni vizuri, msifanye kuwa ni fimbo ya kuwachapia wanyonge, ona sasa Udokta Mwaka umemtokea puani, anahangaika sasa pasina sababu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Wanaume akili zetu bwana. Sasa vitamu vilivyokuwa vingi mtaani mpaka mkachukuliane papuchi kweli
 
BAKITA,TUKI na Wataalam wa kiswahili tupeni maana ya misamiati hii:-

Tahayuri
Shahiri
Mkungu
Ola ola
Swalihina
Paka shume
Usratu
Kabihu
Raghba
Sandani
Tarabushi
Akrabu
Manzili
Durusu
Muntazi
Barobaro
Chambikia
Kochokocho
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom