Mukama: Chadema kiache ubabaishaji
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuacha kile alichodai kuwadanganya wananchi kwamba CCM kujivua gamba si kitu akisema hatua hiyo imefikiwa kukiimarisha chama baada ya kutambua kuwa bila hivyo nchi itayumba.
Mukama alisema hayo kwa nyakati tofauti juzi na jana katika Kijiji cha Kibara, wilayani Bunda na katika Kijiji cha Kaburabura, wilayani Musoma katika mikutano ya hadhara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nane mkoani Mara.
Alisema CCM kimetumia dhana hiyo ya kujivua gamba ili kiweze kurudi kwenye misingi imara, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa, hali ambayo itakiweka kwenye mstari unaotakiwa ambao lengo lake ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo na huduma zote muhimu.
Alisema anawashangaa wapinzani wanaotumia muda mrefu kujadili falsafa ya kujivua gamba na kuhoji uwezo wao katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema amesikitishwa na kauli ya viongozi wa Chadema kwamba kuna uwezekano Rais Kikwete kuondoka madarakani kabla ya 2015 kwa kutolea mfano wa Waziri Mkuu wa Japan aliyeondolewa madarakani.
Alifafanua kuwa viongozi wa Chadema wanatakiwa kufanya uchunguzi kabla ya kutoa matamko kwa maelezo kuwa Waziri Mkuu wa Japan hawezi kufananishwa na Rais Jakaya Kikwete kwa vile aliwekwa madarakani na Bunge wakati Rais alichaguliwa na wananchi.
Alisema kuwa, hata Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kutamka kuwa, bila CCM ya kweli nchi itayumba na kwamba ndiyo maana chama hicho kimeamua kutumia dhana hiyo ya kujivua gamba ili kiweze kuwa imara na kinachoweza kusimamia maendeleo ya wananchi.
"Tunakiweka katika misingi ya kukiimarisha ili kiwe chombo imara ambacho kweli kinaweza kusimamia maendeleo katika maeneo yetu tunayoishi. Sasa hawa Chadema wameichukua dhana hiyo ya kujivua gamba visivyo kabisa," alisema.
Alisema hiyo inatokana na viongozi wa Chadema kuwa na tabia ya kurukia mambo bila kuyafanyia uchunguzi na kwamba wameichukua dhana hiyo visivyo na kuendelea kuwarubuni wananchi ili wakichukie CCM na serikali yao... "Hawa wanataka kwenda Ikulu kwa maneno ya udanganyifu kabisa na maandamano yasiyokuwa na msingi wowote."
Pia alisema kuwa CCM haiwezi kufa kama upinzani wanavyoendelea kuwaambia wananchi, kwani ni chama kikubwa, taasisi na si kampuni ya kibiashara.
Aidha, Mukama amekiponda Chadema ambacho kimekuwa kikidai kwamba CCM imekumbatia wafanyabiashara na kueleza kuwa Chadema ndicho kinayofanya hivyo."Sasa watu wanaokumbatia sera ambazo mwalimu alikuwa anazipinga, eti ndio wanakwenda kwenye kaburi pale wanasema tunakuomba leo utusikilize tuweze kutawala nchi hii kidogo," alisema.
Alisema CCM kina matajiri wachache ambao wanataka kukitumia kwa ajili ya kujinufaisha na kuonya kuwa wafanyabiashara ambao maadili yao hayaendani na chama chao wataondolewa na kuwekwa pembeni mara moja.
Amewataka wakuu wa wilaya nchini na viongozi wa CCM, kusimama imara na kuhakikisha fedha za miradi mbalimbali zinazoletwa na Serikali katika halmashauri husika, zinafanya kazi iliyokusudiwa na si kuishia kwenye mikono ya wajanja wachache.
Alisema kuwa ni lazima wakuu wa wilaya pamoja na viongozi wa chama hicho watekeleze wajibu wao ipasavyo wa kusimamia fedha za Serikali zinazopelekwa kwenye halmashauri.Habari hii imeandaliwa na Boniface Meena, Njombe; Ahmed Makongo na Christopher Maregesi, Bunda na Beldina Nyakeke, Musoma Vijijini.