Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 671
Cairo. Mpango wa Diplomasia ya Afya kwa Wanafunzi wa Tiba umezinduliwa nchini Misri kwa udhamini wa Muungano wa Kimataifa wa Wanafunzi wa Tiba wa nchi hiyo na tawi lake katika Chuo Kikuu cha MTI.
Mpango huo unaolenga kuwawezesha madaktari chipukizi na wanafunzi wa tiba kutoka Misri na wa Sudan kupata mazingira bora ya kujifunza yaliyo jumuishi na ya haki kwa wakimbizi yakichanganya nadharia na uzoefu wa vitendo, umefadhiliwa na Jumuiya ya Kisayansi ya Wanafunzi wa Tiba wa Chuo Kikuu cha Kisasa, na Mpango wa Afromedia wa Uandishi wa Habari na Mawasiliano.
Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo Julai 9, 2025 jijini Cairo, mtafiti wa Anthropolojia, Hassan Ghazaly na mwanzilishi wa Mtandao wa Mshikamano wa Kimataifa na Mwanachama wa Umoja wa Waandishi wa Habari wa Afrika, amesema kuna umuhimu wa daktari kujifunza anthropolojia ili kumsaidia kuelewa jamii zinazohitaji miradi ya maendeleo katika sekta ya afya.
“Vilevile dhana ya diplomasia ya umma na aina zake, pamoja na fursa zinazotolewa na Serikali ya Misri kwa madaktari wa Kiafrika na fursa zinazotolewa na Umoja wa Afrika kwa ajili ya kujitolea katika taasisi za kiafya barani Afrika,” amesema.
Ghazaly ametoa shukrani zake kwa Profesa Mohy El-Din Ragab El-Banna, Mkuu wa Chuo cha Tiba na Upasuaji wa Chuo Kikuu cha Kisasa, na Profesa Hisham Mohamed Omran, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia masuala ya wanafunzi, kwa kutambua ushirikiano wao na juhudi zao katika kuwaunga mkono wanafunzi wa chuo hicho, hasa wanafunzi wa Kiafrika.
Mpango huo uliandaliwa kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa tiba nchini Misri, huku ukitoa fursa sawa na za haki kwa wanafunzi na madaktari wa Kiafrika wasio Wamisri wanaoishi nchini Misri, ili kupata uelewa wa kina kuhusu nyanja mbalimbali za afya na muktadha wake wa Kiafrika na kimataifa, pamoja na mahusiano ya kimataifa, sera za afya, na kuwapa ujuzi wa kufanya utafiti.
Watoa mada mbalimbali walishiriki katika uzinduzi huo, wakiwamo Mostafa Magdy, Msaidizi wa Waziri wa Vijana na Michezo, na Dk Samah Kamel, Mkuu wa Kikundi cha Vijana na Watoto wa Umoja wa Mataifa, na Dk Mahmoud Al-Qally, mkufunzi wa maendeleo endelevu, na Dk Ahmed Al-Rifai, mtaalamu wa sayansi ya siasa
Wengine walioshiriki ni Dk Dalia Ghazlan, mtaalamu wa uelimishaji wa afya, na Hamada Qaoud, mtaalamu wa maendeleo endelevu kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Utawala na Maendeleo Endelevu, na Ahmed Abu Douma, Mwenyekiti wa Kamati ya Kisheria ya Jukwaa la Vijana wa Kiarabu kwa Maendeleo Endelevu, na Dk Rumaila Shahir, mshauri wa maendeleo ya biashara na maendeleo endelevu na Mkuu wa Chuo cha Kijerumani cha Cairo.