Mnyika: Mapambano yamewezesha Faye kushinda Uchaguzi wa Rais Senegal, November 2023 nilikuwa Senegal kusaidia Harakati za Upinzani!

johnthebaptist

JF-Expert Member
May 27, 2014
84,012
142,046
Katibu mkuu wa Chadema mh John Mnyika amesema Mapambano yamewezesha mh Faye kushinda Uchaguzi wa Rais Senegal

Mnyika anasema November 2023 alikuwa Nchini Senegal kama sehemu ya Ujumbe kutaka kiongozi wa Upinzani mh Sonko na mwenzake waachiwe Huru

Mnyika ameeleza ukurasani Kwake X

Mlale Unono 😄
---
1711393729682.png
Katika ukurasa wake wa X Mnyika anaandika yafutatyo:

Mapambano yamewezesha Bassirou #Diomaye Faye (44) kushinda uchaguzi wa urais kwenye vituo vingi #SenegalElections .

Mwezi Novemba 2023 nilikuwa #Senegal kama sehemu ya ujumbe wa kutaka Kiongozi wa Upinzani Ousmane Sonko ambaye pamoja na mwenzake Diomaye waachiwe huru na chao Chao cha #PASTEF ambacho wakati huo kimefutwa na Serikali kirejeshwe na wote wapewe haki ya kushiriki uchaguzi wa 2024.

Nilichobaini wakati huo ni kuwa yalikuwepo mapambano toka mwaka 2021 wakati Rais Macky Sally alipoonyesha mwelekeo wa kutaka kugombea muhula wa tatu kinyume na katiba ya nchi hiyo.

Uamuzi huo na ugumu wa maisha kwa wananchi, ukosefu wa ajira kwa vijana, madai ya mikataba mibovu ya mafuta na gesi, matumizi ya CFA frank na ufisadi Serikali vikawa kichocheo mapambano kupitia maandamano. Uamuzi wa Rais wa Senegal kuzima maandamano hayo kwa vyombo vya dola kuua raia, kuwaweka Sonko na wenzake gerezani na kufuta Chama chao ukaamsha mapambano zaidi na kusambaza moto wa mabadiliko kwa wadau wengi zaidi ya Chama cha PASTEF.

Mwezi Februari mwaka huu Rais Wa Senegal akataka kusogeza mbele uchaguzi, hata hivyo Baraza la Katiba la nchi hiyo likamkatalia na kuelekeza uchaguzi ufanyike kabla ya muhula wake kuisha tarehe 2 Aprili 2024. Uamuzi huo ilitanguliwa na maandamano mengine ya umma kupinga uamuzi wa Rais na kutaka uchaguzi ufanyike sanjari na wafungwa wa kisiasa kuachiwa huru.

Rais akalazimika kufanya mambo mawili kwa haraka: kutangaza uchaguzi na kupeleka Bungeni amnesty bill.

Hapo ndio ikaendelea safari ya mapambano kwa #OusmaneSonko na #Diomaye kutoka na kujitokeza kwa umma tarehe 15 Machi 2024 kuanza kampeni na hatimaye #DiomayePresident kupigiwa kura 24 Machi 2024. Imekuwa ni mapambano na kampeni ya miaka takribani mitatu kama utaanzia 2021, ama zaidi ya hiyo kama utaanzia Sonko alipogombea mara ya kwanza 2019 au wawili hao na wenzao walipounda Chama cha PASTEF 2014 baada ya kutoka Serikalini wakiwa wakaguzi wa kodi.

Mgombea wa coalition Yao iliyoundwa baada ya PASTEF kufutwa alipaswa kuwa Sonko. Hata hivyo tofauti na mwenzake ambaye alikuwa mahabusu, Sonko alishapatikana na hatia kwenye kesi kadhaa za kisiasa na mojawapo ikasababisha aondolewe kwenye orodha ya wagombea urais. Haraka akamuunga mkono mwenzake ambaye alikuwa Katibu Mkuu wake kwenye Chama. Na Bassirou D. Faye maarufu kama Diamaye akaogelea kwenye mawimbi ya mapambano na mabadiliko yaliyofunguliwa na Sonko. Ndio maana kauli mbiu ya waSenegal katika uchaguzi huu imekuwa kwa lugha yao ya kiWolof #DiomayemMooySonko yaani Diomaye ni Sonko.


Nimeshuhudia nguvu ya pamoja ya wawili hawa sio tu katika mabango, bali katika vituo vya kupigia kura nilivyotembelea jana asubuhi mpaka wakati wa matokeo jioni. Sasa kinachusubiriwa ni Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kukamilisha mchakato wa majumuisho na kumtangaza mshindi. Mapambano yameshinda Senegali, ni vyema nchi hiyo sasa ikajifunza kwenye mapito ya Marais Wade na Sally na kizazi hiki kipya kilete mabadiliko kwenye maisha ya watu. Kwetu Tanzania tuendeleze mapambano ya kikatiba na kisheria kuwezesha chaguzi huru na haki. Tujiandae kwa #WikiYaMaandamano 22 mpaka 28 Aprili 2024.

Pia soma:
- Senagal imechagua Rais kijana kuliko nchi yoyote Africa
 
Back
Top Bottom