Brightman Jr
JF-Expert Member
- Mar 22, 2009
- 1,224
- 237
BAADA ya kubainika kwamba tuhuma zilizotolewa na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini dhidi ya baadhi ya wabunge kuwa walipokea rushwa hazikuthibiti na viongozi hao kukemewa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema hajaridhika na uamuzi wa Spika Anne Makinda kuhusu uongozi wa wizara hiyo.
Kutokana na kutoridhika huko, sasa ameamua kukata rufaa ili anachokiona kinafaa kuchukuliwa dhidi ya viongozi hao kichukuliwe.
Mnyika jana alilazimika kutoa taarifa yake nje ya Bunge baada ya mkutano wa Bunge kuahirishwa juzi na yeye kukosa fursa ya kusema jambo hilo bungeni.
Mbunge huyo alisema katika taarifa yake kwamba anakusudia kukata rufaa, dhidi ya uamuzi wa Spika kwa madai kuwa maudhui yake hayazingatii Katiba ya nchi, sheria za nchi, kanuni za kudunmu za Bunge, uamuzi wa awali wa maspika wa Bunge na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu kama wa Bunge la Tanzania.
"Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa rufaa huchukua muda kusikilizwa, nilitaka niombe mwongozo wake kabla ya Mkutano wa Bunge kuahirishwa, kwa kuwa katika uamuzi wake hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini ilivyovunjwa. "Hivyo Spika anapaswa bado kueleza kwa umma iwapo Kamati hiyo inarejeshwa au inaundwa nyingine au kuelekeza kamati nyingine ya kudumu ya Bunge inayopaswa kuisimamia Serikali wakati huu ambao nchi inakabiliwa na matatizo mengi kwenye sekta za nishati na madini yenye athari kwa maisha ya wananchi," alisema Mnyika.
Alisema katika uamuzi wake, Spika alieleza kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliackim Maswi walitoa maelezo yasiyokuwa na ukweli hivyo uwepo wa Kamati ya Bunge kwa ajili ya kuisimamia Wizara hiyo kwa niaba ya Bunge ni suala linalohitaji uamuzi wa haraka.
Alisistiza kusudio lake la rufaa ili taarifa kamili ya Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iwasilishwe kwa ukamilifu kwenye kamati husika ya kudumu ya Bunge na hatimaye taarifa kamili kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili ‘mbivu na mbovu' zijulikane na masuala yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada na vyombo vingine vya nje ya Bunge yaendelee kwa hatua zaidi.
Aidha, alisema atakata rufaa kwa kuwa kiwango cha ‘adhabu' kilichotolewa kwenye uamuzi wa Spika hakilingani na ‘makosa' ambayo yameelezwa kuwa na uzito wenye kuathiri "kwa kiasi kikubwa hadhi ya Bunge kama taasisi na heshima ya wabunge waliohusishwa".
"Spika amefanya uamuzi wake chini ya Kanuni ya 5(1) na 72 (1) lakini hakuzingatia kuwa kanuni ya 72 (3) inaeleza kuwa iwapo mbunge ameshindwa kuthibitisha ukweli Spika amepewa fursa ya kumsimamisha mbunge huyo kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi vitano," alisema.
Aliongeza kuwa atakata rufaa, kwa kuwa waliodaiwa kutoa tuhuma bila ushahidi, walipaswa kujieleza kuhusu tuhuma hizo kabla ya kuhukumiwa kwa misingi ya kanuni za haki ya asili zilizopo pia katika Katiba ya Nchi na kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za kudumu za Bunge.
Pia alisema atakata rufaa kwa kile alichokieleza kuwa ni adhabu aliyopewa Maswi kutolingana na ukubwa wa makosa anayodaiwa kufanya.
"Iikiwa ni kweli amevunja haki za Bunge kwa kuzusha tuhuma za uongo dhidi ya wabunge kwa ajili ya kujihami dhidi ya baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliokuwa wanahoji kuhusu utendaji wa wizara yake. "Kwa kosa hilo ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Kamati ni sahihi anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na kupewa adhabu ya zaidi ya onyo ikiwamo hata faini au kifungo au walau kutakiwa kuwajibika," alisema Mnyika.
Waziri Muhongo na Katibu Mkuu Maswi walishasema hawana lolote la kuzungumza juu ya suala hilo na kuomba waachiwe wananchi waamue wenyewe na wao wanasonga mbele kutumikia wananchi kuondokana na kero zinazowakabili.
SOURCE: Habari leo