Hans Mloli na Martha Mboma
MCHEZAJI mpya aliyetinga katika mazoezi ya Yanga juzi kwa ajili ya majaribio ya kusajiliwa kwenye timu hiyo, Said Kundenda, aliibua jambo baada ya kushindwa kuonyesha uwezo kiasi cha Kocha Msaidizi wa Yanga, Felix Minziro kutamka kuwa alikuwa akiwakaba wenzake wa timu moja huku Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts akisema aende Simba.
Mchezaji huyo aliyejitambulisha kwa Brandts kuwa ni Mtanzania aliyekuwa Msumbiji akicheza ligi kuu ya huko, alifika mapema kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola, Dar na kuomba kupewa nafasi ya kuonyesha uwezo.
Brandts alimpa majukumu ya kucheza kiungo mkabaji kama alivyojinadi, lakini baada ya dakika tano, Minziro alianza kulalama kuwa mchezaji huyo anawategea wenzake na kwamba hana msaada kwa sababu tangu mazoezi yaanze hajagusa mpira zaidi ya kukimbia tu uwanjani.
Licha ya kuutafuta mpira lakini alishuhudia dakika 15 za kwanza mazoezini hapo zikikatika bila kuugusa mpira, alipobadilishwa namba na kuwa beki wa kulia, ndipo akaugusa mpira mara saba kabla ya kuomba kutoka akidai kuwa hayupo fiti na kueleza kuwa nyama za paja zinamsumbua.
"Ana miaka 28, ni mingi sana halafu mtu mwenyewe ndiyo anacheza vile, kwa kweli hataweza kuwa na nafasi hapa, nina vijana wengi wadogo ambao ni wazuri sana kikosini na kila siku wanagombana kutafuta namba.
"Lakini bado kuna timu nyingi Tanzania, pengine labda akajaribu Simba au Azam, anaweza kupata nafasi," alisema Brandts huku akicheka na kumfanya Minziro naye kuvunjika mbavu kwa kicheko.
source:
Kiungo mpya Yanga kituko, Brandts ampeleka Simba - Global Publishers