Mkutano Mkuu 2019: Hili ndilo chimbuko la SADC

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
Kuanzia leo tutawaletea mfululizo wa makala na habari za mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) ambazo zitazungumzia maeneo mbalimbali ya maendeleo na historia hasa tukio muhimu la mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi na serikali ambalo Rais John Magufuli atakabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya.

Mkutano ujao wa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) utakaofanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia Agosti 17 hadi 18, 2019 utamkabidhi uenyekiti Rais John Magufuli kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Rais Magufuli atapokea uenyekiti kutoka kwa Rais Hage Geingob wa Namibia anayemaliza muda wake. Uteuzi huo ni baada ya Rais Magufuli kushikilia nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa mafanikio katika kipindi cha mwaka mmoja unaoishia mwezi ujao.

Sadc ilianzishwa kupitia mkataba uliosainiwa Agosti 17, 1992 na wakuu wa nchi na serikali kumi na moja Tanzania ikiwamo na makao makuu yake yakiwa Gaborone, Botswana.

Tangu wakati huo, idadi ya nchi wanachama imeongezeka hadi kufikia 16 (Angola, Botswana, Comoro, DR-Congo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe) na kuunda soko la bidhaa na huduma la takribani watu 330 milioni.

MTANGAMANO WA NCHI ZA SADC
Chimbuko la Sadc ni mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na utawala wa mabavu wa makaburu nchini Afrika Kusini. Mapambano hayo yaliongozwa na Kundi la Nchi za Mstari wa Mbele (Frontline States) lililoanzishwa mwaka 1970, Tanzania ikiwa taifa kiongozi wa kundi hilo. Pamoja na Tanzania, nchi nyingine zilikuwa Angola, Botswana, Lesotho, Msumbiji, Swaziland (Hivi sasa inaitwa Eswatini) na Zambia iliyojiunga miaka 10 baadaye.

Tanzania ilichukua jukumu la uongozi wa mapambano Kusini mwa Afrika kutokana na ukweli kwamba, nchi nyingi zilizounda Kundi la Nchi za Mstari wa Mbele, kijiografia, kiuchumi na kijeshi hazingeweza kuhimili vishindo vya serikali ya kibaguzi na mabavu ya Afrika Kusini bila ushiriki wa dhati na makini wa Tanzania.

Baadaye kundi hilo lilijizatiti zaidi kwa kuanzisha Jukwaa la Kuratibu harakati hizo (Sadc) ili kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi na hatimaye kujigeuza tena kuwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc). Kwa mantiki hiyo, Sadc ya sasa na siku zijazo dhima yake kuu ni maendeleo na ustawi wa jamii miongoni mwa nchi wanachama.

Kinadharia, Mtangamano wa Kikanda (Regional Integration) una hatua tano, ambazo ni eneo huru la biashara, umoja wa forodha, soko la pamoja, umoja wa kiuchumi na umoja wa kisiasa. Utekelezaji wa hatua hizo za mtangamano hutofautiana kutokana na hali ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya nchi washiriki.

Aidha, baadhi ya jumuiya huinyambulisha hatua ya nne katika makundi madogo zaidi. Mathalani, umoja wa kifedha na sarafu moja au kuruka baadhi ya hatua kama ilivyofanyika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyoanzia hatua ya umoja wa forodha.

Dhamira ya nchi za Sadc ilikuwa kuifikia hatua ya eneo huru la biashara ifikapo mwaka 2008, ikifuatiwa na umoja wa forodha (2010), kisha soko la pamoja (2015), umoja wa fedha (2016) na hatimaye sarafu moja mwaka 2018. Hali halisi ya utekelezaji inaonyesha kuwa Sadc iko hatua ya kwanza sawia na utekelezaji wa baadhi ya vipengele vya hatua ya pili. Kwa mfano, uondoaji wa viza kwa wasafiri wa nchi wanachama.


FAIDA ZA USHIRIKI WA TANZANIA SADC

Sera ya Taifa ya Biashara ya Tanzania inaainisha kuwa miongoni mwa nyenzo zake kuu za ukuzaji na uendelezaji mauzo nje ni mtangamano wa kikanda. Nyenzo zingine katika muktadha huu ni ushirikiano kati ya Tanzania na nchi nyingine mojamoja (bilateral co-operation) na Mikataba ya Shirika la Biashara Duniani (WTO Agreements).

Kimsingi, nyenzo hizo tatu, ikiwamo ile ya mtangamano wa kikanda, hujumuisha kuondolewa vikwazo vya kiforodha na visivyo vya kiforodha miongoni mwa nchi husika jambo ambalo huhamasisha uzalishaji, ufanyaji biashara na uwekezaji kwa jumla.

Kwa kutambua dhana hiyo, takriban nchi zote za Sadc ziliondoleana ushuru wa forodha ilipofika mwaka 2012, isipokuwa kwa bidhaa chache zilizoonekana nyeti katika mapato ya kodi na ulinzi wa viwanda vichanga ambazo ushuru wa forodha uliondolewa taratibu hadi kufikia zero hivi sasa.

Sambamba na kuondoa vikwazo vya kiforodha miongoni mwa nchi wanachama, hatua zimechukuliwa pia kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha. Kwa mfano, taratibu za kiforodha zimerahisishwa ikiwamo uanzishwaji wa vituo vya forodha vya pamoja (one stop border posts) kama kile kilichopo Tunduma; mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Hatua hiyo imeifaidisha Tanzania kibiashara. Mathalan, takwimu za sekretarieti ya Sadc zinaonyesha kuwa mauzo ya Tanzania katika Jumuiya yaliongezeka kwa zaidi ya maradufu, kutoka Dola za Marekani 432 milioni kwa mwaka 2007 hadi Dola 1,013 milioni mwaka 2016. Aidha, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa Tanzania imeendelea kuwa na urari chanya wa biashara kati yake na Sadc, ikimaanisha kuwa mauzo yake ni makubwa kuliko ununuzi.

Vilevile, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imeingia mkataba na Sadc wa kuuza na kusambaza dawa, vifaa tiba na vifaa vya maabara katika nchi zote 16 wanachama.

Fursa hii inatoa mwanya pia wa kuvutia uwekezaji katika sekta hii jambo ambalo litachangia uendelezaji viwanda na teknolojia nchini katika tasnia ya dawa, vifaa tiba na maabara.

Uledi Mussa ni mstaafu ambaye amekuwa katika utumishi wa umma kwa nyadhifa mbalimbali. Alistaafu akiwa katibu mkuu ofisi ya Waziri Mkuu.

Kesho soma jinsi vita ya ukombozi ilivyozaa Sadc.



credit: Mwananchi
 
Back
Top Bottom